Mwili wa Frateri anayedaiwa kujinyonga kukabidhiwa kwa ndugu Ijumaa

Lushoto. Uongozi wa Shirika la Roho Mtakatifu la Kanisa katoliki, umesema utakabidhi mwili wa Frateri Rogassion Massawe kwa ndugu zake Ijumaa Mei 24, 2024 baada ya taratibu mbalimbali kukamilika.

Uongozi wa shirika umesema shughuli ya kuuaga mwili wa Massawe anayedaiwa kujinyonga, itafanyika siku hiyo jimboni Tanga.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Mei 22, 2024 na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa shirika hilo, Padri Gaudence Kimbori alipozungumza na Mwananchi kwa simu.

Amesema baada ya shirika hilo kukamilisha taratibu zake, mwili utakabidhiwa kwa familia ili iendelee na taratibu nyingine kwa ajili ya maziko.

“Tutashirikiana na familia kwa maeneo fulani lakini kuhusu maziko, utaratibu utatolewa na familia baada ya makabidhiano ya mwili,” amesema Padri Kimbori.

Frateri Massawe anadaiwa kujinyonga Jumatatu wiki hii akiwa kwenye nyumba ya malezi ya Magamba iliyoko wilayani Lushoto.

Inadaiwa kuwa, kabla ya kujinyonga kwa kutumia mshipi, aliacha ujumbe wa maandishi kwa mama yake mzazi unaosomeka, “mama usilie nimeshindwa kufikia malengo, ninajua nimewakwaza wengi.”

 Padri Kimbori amesema mwili wa Frateri Massawe uligunduliwa na wenzake.

Amesema Frateri Massawe alikuwa akiandaliwa kuwa mmisionari na mwezi ujao ilikuwa ahitimu na aingie daraja linalofuata.

“Kipindi chao cha kumaliza kilikuwa kinakaribia, mwezi ujao tu hapa wangekuwa wamemaliza, kwa hiyo walikuwa kwenye hizo hekaheka za maandalizi ya kumalizia mpito wa kuingia kwenye hatua inayofuata, bahati mbaya ndiyo yametokea haya yaliyotokea,” amesema Padri Kimbori.

Kuhusu chanzo cha kifo, Padri Kimbori amesema taarifa itatolewa rasmi na shirika, “kwa sasa hatuwezi kusema kitu, kwa sababu uongozi wa shirika unaendelea kufuatilia, utatoa taarifa rasmi.”

Katika tukio kama hilo, Mei 16, 2024, Askofu Mkuu wa Makanisa ya Methodist, Joseph Bundala alikutwa amefariki dunia chooni ndani ya ofisi yake kwa madai ya kujinyonga eneo la Meriwa, jijini Dodoma.

Juzi, akizungumza na Mwananchi kwa simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi alisema chanzo cha kujinyonga kwa Frateri huyo kinadaiwa ni kufeli mtihani wake uliokuwa unampeleka kwenye daraja la upadri.

“Taarifa za awali, tulizozipata zinadai sababu ya kujinyonga kwa mwanafunzi huyo, walikuwa na mitihani ya kuvuka kutoka ngazi moja, kwenda nyingine, peke yake ndiye amefeli. Hivyo, kutokana na msongo wa mawazo ndiyo akafikia uamuzi huo wa kujinyonga,” amedai Kamanda Mchunguzi.

Amesema polisi wanaendelea na uchunguzi wa kifo hicho na ukikamilika, taarifa kwa umma itatolewa.

Jana, Mwananchi ilifika nyumbani kwa marehemu Kijiji cha Umbwe Onana wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro kujua nini kinaendelea kuhusu msiba huo.

Hata hivyo, ndugu wa marehemu waligoma kutoa ushirikiano, huku mmoja wao akisema wanasubiri taarifa rasmi kutoka Jeshi la Polisi.

Related Posts