Sababu madini ya vito kuporomoka

Dar es Salaam. Kubadilika kwa soko, hali ya kiuchumi na mvua nyingi, zinatajwa kuwa sababu za kushuka kwa thamani ya madini ya vito.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya tathmini ya hali wa kikanda ya Desemba 2023.

Ripoti inataja almasi, tanzanite na madini mengine ya vito kuwa  mauzo yake yameshuka kwa zaidi ya asilimia 40, huku dhahabu ikipaa.

Ripoti hiyo inayoishia Desemba 2023 iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), inaonyesha kuwa thamani ya madini halisi yaliyouzwa kwa ujumla imeshuka kwa asilimia 4.5.

Kupungua kwa fedha zinazotokana na uuzaji madini ndani ya kipindi hicho hakuchangiwi tu na madini ya vito, bali makaa ya mawe na limestone nazo zimetajwa.

Uchambuzi unaonyesha, mauzo ya makaa ya mawe yalishuka kwa asilimia 15, huku kupungua kwa mahitaji yake katika soko la dunia ikiwemo Ulaya ikitajwa kuwa sababu.

Hata hivyo, kwa upande wa almasi na madini mengine ya vito, kushuka kwake kunatajwa na BoT kuchangiwa na kupungua kwa shughuli za uchimbaji kulikochochewa na mvua kubwa zilizokuwa zikinyesha.

Wakati mauzo yakizorota, Kanda ya Ziwa imeendelea kubeba asilimia 60.2 ya fedha yote ya madini, ikifuatiwa na nyanda za juu kusini na Kusini Mashariki ambazo zilikuwa na asilimia 15.4 na asilimia 15 mtawalia.

Ripoti hii ya BoT inafafanua thamani ya almasi ilishuka kwa asilimia 53.4 kutoka Sh61.696 bilioni Desemba mwaka jana hadi Sh28.65 bilioni Desemba, mwaka jana.

Tanzanite nayo ilitoka Sh6.7 bilioni Desemba mwaka jana hadi kufikia Sh4.144 bilioni mwaka uliofuatia

Madini mengine ya vito thamani yake ilishuka kwa asilimia 48.3 kutoka Sh36.3 bilioni Desemba 2023.

Akizungumzia suala hilo, Katibu Mkuu wa Chama cha Wanawake Wachimbaji Tanzania (Tawoma), Salma Ernest, anasema madini ni kama fedha za kigeni ambazo thamani yake hushuka na kupanda kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo za kiuchumi.

Anasema jambo hilo lipo pia hata kwa madini, kwani kuna wakati ambao soko linakuwa juu na thamani yake kuongezeka na kuna wakati ambao soko linashuka na kufanya thamani yake kushuka.

“Kwa mfano, kuna madini kama tourmaline,  kuna wakati kilo moja yananunuliwa kwa Sh70,000 hadi Sh100,000 na kuna wakati yanafika hadi Sh200,000, inategemeana na soko,” anasema.

Pia anasema kufungwa kwa baadhi ya viwanda kupisha sikukuu nchini China huwa ni moja ya sababu za kuwapo kwa hali hiyo.

“Nafikiri kuanzia Februari soko la China huwa wanafunga na kwenda katika sikukuu zao, hii hufanya soko kukosekana,” anasema Salma.

Kushuka kwa mauzo haya kuligusa kanda zote nchini, huku Kusini Mashariki wakiwa katika kiwango kikubwa zaidi.

Kanda hiyo ilikuwa na pungufu ya mapato yatokanayo na madini kwa asilimia 20.8, ikifuatiwa kwa ukaribu na Kanda ya Kaskazini iliyokuwa na asilimia 13.2.

Kanda ya Ziwa ambayo inaongoza kwa kuwa na kiwango kikubwa cha mapato katika madini nayo ilishuhudia upungufu wa asilimia 3.8 ikilinganishwa na fedha walizopata Desemba 2022.

Nyanda za juu kusini wao walikuwa na asilimia 1.2 ya anguko katika fedha zilizotokana na madini.

Lakini wakati madini ya vito yakijikongoja katika uingizaji wa fedha, dhahabu iliendelea kufanya vyema kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Mauzo yake yalifikia thamani ya Sh1.61 trilioni Desemba 2023 ikilinganishwa na Sh1.59 trilioni mwaka uliotangulia. Mauzo hayo yalibeba takribani asilimia 76.6 ya mauzo yote ya madini katika mwaka ulioshia Desemba 2023.

Akizungumzia suala hilo, Profesa Aurelia Kamuzora anasema mahitaji na usambazi ndiyo yanaweza kufanya biashara yoyote kushuka na kupanda kulingana na wakati.

Anasema huenda mahitaji ya dhahabu ni makubwa zaidi duniani kuliko madini ya vito, lakini ni vyema utafiti ukafanyika kujua sababu kwa kina.

“Kuuza kuna namna mbili, kwanza kuwepo na uhitaji na uzalishaji, ukizalisha bila kuhitajika sokoni inaweza kufanya madini mengi yabaki nchini au tuangalie kama uzalishaji umepungua,” amesema Kamuzora.

Hata hivyo, anasema dhahabu ina soko kubwa kutokana na kutumika kama njia mbadala ya kulinda uchumi wa nchi na mara nyingi hununuliwa na watu wenye kipato kikubwa, huku wakiwa na malengo tofauti, ikiwemo kuuza baadaye zitakapohitajika.

Anasema kingine kinachofanya dhahabu uzalishaji wake kuwa juu ni kutokana na kupatikana maeneo mengi, kuwa na watu wengi wanaojihusisha na uchimbaji wa madini hayo ukilinganisha na madini mengjne.

“Utafiti uendelee kufanyika kujua kitu gani kinachotumika katika uzalishaji dhahabu, kwa nini wachimbaji wa dhahabu wanaweza wengine washindwe, huenda dhahabu iko mlimani zaidi ambako hakuathiriwi na mvua, inachimbwa sehemu nyingi zaidi kuliko madini mengine, hivyo ni vyema utafiti zaidi kufanyika,” anasema Profesa Kamuzora.

Mchumi, Oscar Mkude anasema kabla ya fedha kuwapo, utajiri katika nchi ulikuwa ukiangaliwa kwa wingi wa dhahabu walizonazo, jambo ambalo linafanya madini hayo kuendelea kuwa na thamani.

Hata sasa, baadhi ya nchi zimekuwa zikihifadhi dhahabu kwa ajili ya matumizi ya baadaye, ikiwa inatajwa kuwa moja ya njia inayotumika kulinda thamani ya fedha.

“Dhahabu ni tofauti na madini mengine, yenyewe haiongozwi na upatikanaji wake, inaweza kuwa haipatikani kwa wingi, lakini watu wanayo katika stoo zao wakatoa kuuza, pia dhahabu ni tofauti na almasi, kwani yenyewe inaweza kutumika zaidi ya mara moja,” anasema Mkude.

Mkude anasema raha ya almasi ni mtu kuvaa na kupendeza, lakini hawezi kuibadilishia matumizi, tofauti na dhahabu inayoweza kuyeyushwa na kuleta kitu kingine.

“Mtu anaweza kuwa na pete yake ya dhahabu au hereni akiuza mnunuzi anaweza kuitumia kwa namna nyingine ikiwemo kuyeyusha ili kupata kitu kipya,” anasena Mkide.

Naye mhadhiri wa Chuo Kikuu   Huria Tanzania (OUT), Dk Yohana Lawi anasema pamoja na mapato yanayopatikana katika mauzo ya madini,  mpaka sasa bado Serikali haina njia nzuri ya kushughulikia biashara za madini.

“Serikali haina njia madhubuti ya kubaini kilichozalishwa. Mifumo hii wakati mwingine kila kitu kinachoendeshwa kiko chini ya sekta binafsi na wageni huenda hata dhahabu tunayoona inafanya vizuri ingeweza kufanya vizuri zaidi kama kungekuwa na mfumo mzuri wa kudhibiti upotevu wa madini.

 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo aliomba kupewa muda kujiridhisha juu ya kile kilichosemwa kabla ya kuzungumza chochote.

“Hapa nilipo siwezi kuzungumxia kwa ufasaha sana, sitaki kukosea kama mtendaji wa wizara ukinipa muda ntakua na jibu zuri,” Alisema Mbibo alipozungumza kwa njia ya simu.

Related Posts