Sakata la umri wa kuolewa latua tena bungeni

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema imekamilisha uandaaji wa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ndoa na hivi sasa muswada huo upo katika hatua za ndani za Serikali.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sajini amesema hayo leo Jumatano Mei 22, 2024 wakati akijibu swali la msingi la mbunge wa viti maalumu, Dk Thea Ntara.

Mbunge huyo amehoji ni lini Serikali itapeleka bungeni Muswada wa Sheria ya Ndoa ili iendane na vita dhidi ya ndoa za utotoni.

Si mara ya kwanza swali hilo au hoja hiyo kuibuliwa bungeni kwa kuwa limekuwa likijitokeza mara kadhaa.

Akijibu swali hilo, Sagini amesema baada ya uamuzi wa Mahakama ya Tanzania, Serikali iliwasilisha bungeni muswada wa marekebisho ya Sheria ya Ndoa kupitia tangazo Na 1. Vol 102 la Februari 5, 2021 kwa kupendekeza umri wa kuoa au kuolewa uwe miaka 18.

Pia, Bunge kupitia Kamati ya Uongozi ilielekeza Serikali kukusanya maoni ya wananchi kuhusu suala hili.

Sagini amesema baada ya maelekezo hayo, Serikali ilikusanya maoni ya wananchi.

Amesema vilevile, Aprili 26, 2023 Serikali ilifanya kongamano la Sheria ya Ndoa, Mkoa wa Dodoma ili kupata maoni zaidi kuhusu umri wa kuingia kwenye ndoa.

Amesema katika kongamano hilo, lililokuwa na ushirikishwaji mpana wa wadau wakiwamo wazee wa kimila, viongozi wa kidini, wanataaluma, wanafunzi wa ngazi mbalimbali, watu mashuhuri na wabunge.

Sajini amesema kongamano hilo lilikuwa mubashara kupitia Televisheni ya Taifa na wananchi waliruhusiwa kupiga simu na kutuma ujumbe na maoni yao.

”Wizara imekamilisha uandaaji wa muswada wa marekebisho ya Sheria ya Ndoa na hivi sasa muswada huo upo katika hatua za ndani za Serikali. Mara hatua hizo zitakapokamilika, muswada huo utawasilishwa bungeni kwa utaratibu wa kawaida,” amesema.

Katika swali la nyongeza, Dk Ntera ameomba hatua zilizoelezwa na Serikali kwenda kwa kasi kama alivyosema ili sheria hiyo ifanyiwe marekebisho.

Oktoba 23, 2019, Mahakama ya Rufani ilitamka kuwa vifungu vya 13 na 17 vya sheria ya Ndoa, sura ya 29 marejeo ya 2002 ni kinyume cha Katiba, hivyo Serikali kupewa mwaka mmoja, kurekebisha vifungu hivyo vya sheria.

Mahakama ilimwelekeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kurekebisha masharti ya kifungu cha 13 na 17 cha Sheria ya Ndoa badala yake kuweka miaka 18 kama umri unaostahili kuoa na kuolewa kwa wavulana na wasichana.

Related Posts