Akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) amefafanua kuwa, uenyeji huu umekuja kufuatia maamuzi ya Mkutano wa 37 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika mwezi Februari 2024 jijini Addis Ababa, Ethiopia.
“Ikumbukwe kuwa, mwezi Machi 2022 Tanzania ilichaguliwa kuhudumu kwenye nafasi ya Mjumbe wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika kwa miaka miwili hadi mwezi Machi 2024 ambapo muda wa kuhudumu ulifikia kikomo. Hivyo Tanzania imechaguliwa tena kuhudumu kwenye Baraza hilo kwa muhula mwingine wa miaka miwili hadi mwaka 2026,” alisema Mhe Waziri.
Amesema Baraza la Amani na Usalama ni chombo cha juu cha maamuzi kuhusu masuala ya amani na usalama kwenye Umoja wa Afrika likiwa na jukumu la kuzuia kutokea kwa migogoro, kusuluhisha au kukabiliana nayo pale inapojitokeza.
Amesema Nchi 15 tu kati ya nchi 55 wanachama wa Umoja wa Afrika ndio wajumbe wa Baraza hilo na kuongeza kuwa wajumbe wa sasa ni pamoja na; Tanzania, Uganda na Djibout (Ukanda wa Afrika Mashariki); Cameroon, DRC na Equatorial Guinea (Kanda ya Kati); Afrika Kusini, Angola na Botswana (Kanda ya Kusini); Cote d’Ivoire , Gambia, Nigeria, na Sierra Leone (magharibi) na Misri na Morocco (Ukanda wa Kaskazini).
‘’Hivyo, Tanzania kuwa Mjumbe kwenye Baraza hili ni ishara ya kuheshimika na kuaminika kwa nchi yetu, ambapo heshima hiyo inaifanya nchi yetu kupewa jukumu jingine kubwa zaidi la kuwa mwenyekiti wa Baraza hilo kwa mwezi Mei. Katika nafasi ya Uenyekiti Tanzania inajukumu la kusimamia shughuli zote zinazohusu Baraza, ikiwemo kufuatilia kwa karibu hali ya ulinzi na usalama kwenye Bara la Afrika, kutoa miongozo ya kushughulikia na masuala ya kiusalama pale inapobidi na pia kuandaa ratiba na kuongoza vikao vya Baraza,’’ alisema Waziri Makamba.
Pia Mhe. Makamba ametumia fursa hiyo kumshukuru na kumpongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya ya kuimarisha Diplomasia ya Tanzania katika kutoa kipaumbele kwenye masuala ya ulinzi na usalama barani Afrika na dunia kwa ujumla.
Katika maadhimisho hayo Tanzania kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Baraza imeandaa ratiba ya shughuli mbalimbali kwa kuifanya kila wiki katika mwezi Mei kubeba dhima mahsusi ambazo ni: Usuluhishi na majadiliano; masuala ya mahitaji ya kibinadamu,amani na usalama; ulinzi kwa Watoto na kusaidia misheni za amani.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ya Miaka 20 ya Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika ni; ‘’Miaka 20 ya Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika ikiwa chombo cha Maamuzi: Miongo miwili ya Afrika ya Amani na Usalama tunayoitaka (20 years of the AU PSC as a Standing Decision-Making Organ: The Next Decades of the Peace and Security We Want in Africa)’’
Maadhimisho haya, yanatoa fursa kwa Waafrika wote wenye kuitakia mema Afrika kutoa maoni yao ya kuliimarisha Baraza ili liweze kushughulikia changamoto za kiusalama barani Afrika. Hivyo, wageni takriban 120 kutoka nchi mbalimbali wanatarajiwa kuhudhuria.
Kadhalika, Miongoni mwa watu mashuhuri watakaoshiriki ni pamoja na; Mhe. Jesca Alupo, Makamu wa Rais Uganda, Mhe. Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Rais Mstaafu wa Nigeria, Mhe. Olesegun Obasanjo, Rais Mstaafu wa Burundi, Mhe. Domitien Ndayizeye, Rais Mstaafu wa Msumbiji, Mhe. Joachim Chissano na Rais wetu Mstaafu, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete.
Mhe. Waziri Mkamba ametoa rai kwa watanzania kushiriki kwa wingi katika siku ya tarehe 24 Mei, 2024 ambako kutakuwa na mjadala wa wazi utakaofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na siku ya kilele cha maadhimisho hayo ili kumuunga mkono Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa heshima kubwa aliyopewa na Umoja wa Afrika.
Maadhimisho ya miaka 20 ya Baraza yatahitimishwa kwa kutolewa kwa Tamko la Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) akiongea na waandishi wa habari kwenye mkutano uliofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam tarehe 22 Mei, 2024.