Ujumbe wa Eswatini wafika HESLB kujifunza

Ujumbe wa watu watano kutoka Jamhuri ya Kifalme ya Eswatini umeanza ziara ya mafunzo ya siku tano nchini inayolenga kujifunza kuhusu uchini ya uenyeji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).

Katika siku ya kwanza ya ziara hiyo, ujumbe huo  (Jumanne, Mei 21, 2023) umefika katika ofisi za HESLB zilizopo eneo la TAZARA jijini Dar es salaam na kukutana na Menejimenti ya HESLB ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Bill Kiwia.

Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Kiwia amewakaribisha wageni hao na kupongeza uamuzi wa kujifunza katika moja ya nchi za Afrika ambazo changamoto na fursa zinafanana.

Ujumbe huo unajumuisha Bw. Brian Vilakati, Mwenyekiti wa Bodi ya Elimu na Mafunzo (PTET) iliyo chini ya Wizara ya Kazi na Hifadhi ya Jamii ya Eswatini; Bi. Sifisosethu Bhembe, Meneja Ruzuku; Bi. Qondile Zwane, Mwanasheria; Bi. Nokuthula Dlamini, Mchambuzi wa Sera; na Bi. Nompilo Mncina, Ofisa Mawasiliano. PTET ndiyo taasisi inayosimamia ruzuku ya elimu kwa wanafunzi.

Akizungumza katika kikao kazi cha kwanza, Bw. Vilakati amesema uamuzi wa kuja Tanzania kujifunza unatokana uzoefu ambao HESLB inao katika usimamizi wa mikopo na ruzuku kwa takribani miaka 20 tangu ilipoanzishwa mwaka 2004.

Kwa upande wake, Bi. Bhembe, Meneja Ruzuku katika ziara hiyo, pamoja ba HESLB na wadau wengine, pia wanatarajia kukutana na uongozi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) ili kushauriana kuhusu maeneo ya ushirikiano.

“Tunafahamu kuwa utoaji mikopo na ruzuku huzingatia kipaumbele kwa kozi za sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM), lakini tungependa kujua undani kuhusu upatikanaji wa kozi hizo na wanafunzi,” ameongeza Bi. Bhembe.

Katika ziara hiyo, ujumbe wa Eswatini unatarajia kujifunza kuhusu taratibu za upangaji na urejeshaji wa mikopo, matumizi ya mifumo ya TEHAMA na miongozo ya jumla inayosimamia ugharimiaji wa elimu ya juu.

Related Posts