WATENDAJI WIZARA YA NISHATI NA TAASISI WAPATA MAFUNZO YA MFUMO WA PEPMIS NA PIPMIS

-Wakurugenzi, Wakuu wa Idara watakiwa kusimamia vema mfumo wa PEPMIS

Dodoma

Watendaji wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake leo 22 Mei,2024 wamepata mafunzo ya upimaji utendaji kazi kutoka kwa Wataalam wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma ili kuboresha utendaji kazi kupitia mfumo wa PEPMIS na PIPMIS.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Utumishi Bi. Felister Shuli ameitaka Wizara kuhakikisha inafuata miongozo ya mifumo ya upimaji wa utendaji kazi na kutatua changamoto zilizoko kwenye mfumo ili kuleta ufanisi kwenye utendaji kazi.

Alisema kwa majibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma kifungu 6A sura 298 inawataka watumishi wote wa umma kuhakikisha wanatumia mifumo hiyo kwa weledi na Wizara inatakiwa kuongeza juhudi kwenye matumizi ya mifumo hiyo.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Bi.Ziana Mlawa amewataka watendaji wa Wizara na taasisi kuhakikisha wanatumia mifumo hiyo ipasavyo na kuhakikisha Wizara inafanya vizuri kwenye eneo hili.

Amesema mifumo hii ni muhimu kwa utendaji kazi wa Wizarani na taasisi zake kwani ndio inampa nafasi Mtumishi kuboresha utendaji wake wa kazi na kutoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu.










Related Posts