Dar es Salaam. Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (Dart), umesema Julai 2024, utaanza matumizi ya mageti ya mfumo wa kuchanja kwa kadijanja kwa ajili ya abiria watakaopanda usafiri huo.
Kwa mujibu wa Dart, hatua hiyo itakuwa ni baada ya kukamilika kwa shughuli ya kufunga mfumo wa mageti katika vituo mbalimbali vya mabasi yaendayo haraka, inayoendelea sasa.
Wakala huo umeeleza kuwa mpango huo unalenga pamoja na mambo mengine, kudhibiti upotevu wa mapato katika ukusanyaji wa nauli za abiria wa usafiri huo.
Hii si mara ya kwanza kwa Dart kutumia mfumo huo, uliwahi kutumika mwaka 2016 wakati mradi unaanza na huduma hiyo ikisimamiwa na mampuni ya Max Malipo.
Baadaye mwaka 2018 kadi za kuchanja zilizokuwa zinatumika, zilisitishwa kwa madai kuwa zilikuwa zinavujisha mapato na mfumo wa tiketi ukachukua nafasi.
Hali bado iliendelea kuwa mbaya licha ya mabadiliko hayo, katika mfumo wa tiketi ulibainika wizi wa fedha, kama ilivyowahi kuelezwa na Mohamed Mchengerwa, waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Kutokana na hayo, uamuzi wa matumizi ya kadijanja kupitia mfumo wa mageti umeonekana kuwa mwarobaini.
Hatua hiyo mpya imetangazwa na Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Dart, Ng’wanashigi Gagaga katika moja ya taarifa zake mbele ya waandishi wa habari.
Kwa mujibu wa Gagaga, kadi hizo ni salama na haitakuwa rahisi kudukuliwa.
“Kadi hizi ni salama zaidi si rahisi kudukuliwa zimedhibiti mianya zaidi na zina kitu kingine muhimu ndani yake, kuna vyumba vingi vya kuweka kadi nyingine kama usafiri wa reli au mabasi yaendayo mikoani,” amesema.
Amesema bei ya kadi hiyo itakuwa kubwa tofauti na zile za awali, ambazo moja iliuzwa kwa Sh500.
“Bei yake hatujaipanga lakini tulishashauriwa na mkaguzi mkuu wa ndani ziuzwe bei juu kidogo badala ya kuuza kwa bei rahisi, ili kuzuia watu wasizipoteze kirahisi, bado hatujapata bei elekezi,’’ amesema.
Mbali na kuweka salio kwenye kadi hiyo kupitia wahudumu wa mabasi hayo, Gagaga amesema hata kwa simu yako unaweza kuijaza au kwa wakala wa huduma za kifedha.
“Hatutatumia tena kadi za zamani kwa kuwa ni rahisi zaidi kudukuliwa. Tutatumia mpya kwa waliokuwa nazo tutawawekea utaratibu mpya,” amesema.
Awali, akizungumza Dar es Salaam, wakati anafunga mafunzo ya siku tano ya timu ya wataalamu 10 wa mfumo wa kadijanja hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa Dart, Dk Athumani Kihamia alisema tayari wameshaingiza mageti janja zaidi ya 300 yenye thamani ya Sh11 bilioni.
“Mageti haya 300 yamekuja yakiwa na gharama kubwa zaidi ya Sh11 bilioni na wakandarasi wako saiti sasa hivi na asilimia 67 ya kazi imeshakamilika,” alisema.
Dk Kihamia alisema mbali na kudhibiti mapato, mageti hayo yatasaidia kuokoa muda kwa abiria na kuweka mazingira safi baada ya kuacha kutumia karatasi.
Mmoja wa wataalam waliokuwa wanatoa mafunzo hayo kutoka Kampuni ya AdvanIDe, Duncan Chege alisema teknolojia hiyo itakuwa na tija ikianza kutekelezwa kwani ina usalama wa kutosha.
“Tanzania ni nchi ya ambako wametoa mafunzo ya teknolojia hiyo lakini kwa Afrika Tanzania ni nchi ya tatu,” amesema Dakan
Katika hatua nyingine Dk Kihamia amesema kunzia Oktoba 2024 wakala huo utakuwa umepata mabasi mapya 177 ya awamu ya kwanza na kwamba tayari mzabuni ameshapatikana.
“Ifikapo Oktoba mwaka huu tunatarajia kuwa na mabasi mengine 177 mapya, mzabuni ameshapatikana na mkataba tunategemea kusaini mwezi huu na tunaamini baada ya miezi mitano utakuwa umetekelezwa,’’ amesema.
Dk Kihamia amesema katika mageuzi hayo bado wanaendelea na mchakato wa awamu ya pili kwa ajili ya barabara inayotokea Mbagala Rangi tatu hadi Mjini kati.
“Mchakato wake umeanza na kufikia mwishoni mwa mwaka huu tunaamini huduma hiyo itakuwa inatolewa kwa barabara ya Mbagala Rangi tatu hadi maeneo mbalimbali ya mjini,” amesema.