MAMBO yamebadilika ghafla ndani ya Simba na sasa inaonekana kuwa vizuri tofauti na wiki kadhaa zilizopita pindi ilipokuwa chini ya kocha aliyeondoka, Abdelhak Benchikha.
Juma Mgunda anaonekana kuibadilisha ndani ya muda mfupi aliokaa kwa kuifanya icheze vizuri na kutawala mchezo huku ikipata matokeo yanayoridisha tofauti na ilivyokuwa siku za mwishoni za Benchikha ndani ya timu hiyo.
Ninachokiona, Benchikha sio kocha mbaya kama baadhi ya watu wanavyombeza, hasa baada ya kuona chini ya Mgunda, Simba inampiga mtu nyingi huku bolu likitembea, tofauti na ilivyokuwa kwenye mechi nyingi chini ya kocha wao waliyepita kutokea huko Algeria.
Kocha ambaye hadi anajiunga na Simba alikuwa ametoka kuiongoza timu kuchukua ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika na kisha lile la Caf Super Cup anakuwaje ghafla mbaya na hafai tena kwenye ligi yetu?
Kwa anachokifanya Mgunda hivi sasa, inatoa picha ya wazi tatizo la Benchikha ndani ya Simba halikuwa linahusu mbinu na badala yake ni namna alivyokuwa akiishi na kuwasimamia wachezaji wa timu hiyo, kambini, mazoezini na kwenye mechi.
Inaonekana Benchikha alipoteza imani kwa kundi kubwa la wachezaji wa Simba, kwanza kutokana na ukali wake kwao, pia namna alivyokuwa anatoa nafasi ya kucheza kwa wachache mara kwa mara na wengine kutowapa vya kutosha.
Kunapotokea hali kama hiyo, kuna kundi litajiona halina thamani ndani ya timu na wengine wataona wao ndio wana nguvu kikosini na wanaweza kuanza kujiamulia wanachokitaka wao na hivyo kupoteza umoja na kupelekea timu ifanye vibaya.
Pia inasababisha baadhi ya wachezaji kubweteka na hata kuporomoka viwango vyao kwa vile wanajua hata wakifanya vibaya wataendelea kupata nafasi ya kucheza na wengine kutojituma kwa sababu watajiona hawawezi kuaminiwa hata kama wanaonyesha kitu.
Sasa Mgunda anawafanya wachezaji wote kama watoto wake na anajaribu kutoka nafasi kwa kila mmoja jambo linalosababisha wengi wajikute na deni la kumpambania wakiamini wakimwangusha wanaweza kurudi walikotoka.