KUNA matumaini finyu kwa Mtibwa Sugar kusalia katika Ligi Kuu Tanzania Bara wakati huu ambao imebakiza raundi mbili kumalizika.
Mabingwa mara mbili wa zamani wa taji la ligi hiyo, kwa sasa iko mkiani mwa msimamo na pointi 21 na hakuna uwezekano wa kubakia moja kwa moja kwenye ligi kwani hata ikishinda mechi mbili ilizobakiza haiwezi kufikisha pointi za timu iliyo katika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi.
Hata kubaki kwa kupitia mechi za mchujo (play off), nafasi iliyobakiza ni moja tu na ina matumaini kiduchu kuipata kwa vile kwa idadi ya pointi ilizonazo na michezo iliyobakiza inaweza kufikia pointi za timu moja tu kati ya mbili zilizo katika nafasi ya 13 na 14 ambayo ni Tabora United.
Mechi mbili ilizobakiza Mtibwa ni dhidi ya Mashujaa na Ihefu ambazo zote itakuwa ugenini, hivyo kitendo cha kutoka angalau sare tu kinamanisha itashuka daraja.
Hapana shaka kinachoishusha daraja Mtibwa msimu huu ni safu yake ya ulinzi ambayo imekuwa na mwendelezo wa kufanya vibaya katika idadi kubwa ya mechi za Ligi Kuu msimu huu kulinganisha na ile ya ushambuliaji ambayo kitakwimu imetimiza vyema wajibu wake hadi leo hii wakati zikibaki raundi mbili tu.
Katika raundi 28 za ligi msimu huu, safu ya beki ya Mtibwa ndio inaongoza kwa kuruhusu idadi kubwa ya mabao na timu hiyo imefungwa mabao 46 wakati safu yake ya ushambuliaji imefunga mabao 27 yanayoifanya iwe timu inayoshika nafasi ya nne kwa kupachika idadi kubwa ya mabao ligi kuu hadi sasa.
Jambo la kushangaza, dirisha dogo la usajili, Mtibwa huku ikifahamu fika eneo ambalo linaigharimu ni beki, yenyewe ikajaza idadi kubwa ya wachezaji kwenye safu ya kiungo na ushambuliaji ambazo hazikuwa na tatizo sana.
Matokeo yake tatizo la msingi likaendelea na leo hii zimebaki saa chache tu kabla ya wakata miwa hao kwenda kuungana na ligi ya Championship.