Dodoma. Mtandao wa Madeni na Maendeleo Tanzania (TCDD) umeshauri mikopo yote inayokopwa na Serikali kwa shughuli za maendeleo ipitishwe na Bunge badala ya jukumu hilo kuachiwa kamati zinazomshauri Waziri wa Fedha.
Ushauri huo umetolewa leo Jumatano Mei 22, 2024 na Mkurugenzi wa mtandao huo, Hebron Mwakagenda kwenye mkutano mkuu wa mtandao huo ulioandaliwa kwa kushirikiana na Jukwaa la Afrika na Mtandao wa Madeni na Maendeleo (Afrodad) jijini Dodoma.
Mwakagenda amesema madeni ambayo Serikali huingia yanalipwa kwa fedha za wananchi, hivyo Bunge ambalo ni uwakilishi wa wananchi ni lazima lipitie na kujiridhisha kama mkopo una tija kwa Taifa ndipo liidhinishe au likatae mkopo husika kama litaona hauna tija kwa wananchi.
Amesema kwa kuliacha jukumu hilo kwa kamati ya kumshauri Waziri wa Fedha, deni la Taifa litazidi kupanda na litakuwa siyo stahimilivu, mwisho wa siku kuacha mzigo wa madeni kwa viongozi wanaokuja.
Amesema kwa hali ilivyo sasa, kwa mujibu wa sheria mkopaji mkuu wa Serikali ni Waziri wa Fedha ambaye ana kamati zinazomshauri ambazo zikikamilisha kumshauri anaenda kukopa.
Mwakagenda amesema mashirika yasiyo ya kiserikali yanatamani mfumo huo ubadilishwe, Bunge liwe sehemu ya usimamizi wa ukopaji.
“Waziri anapomaliza mchakato wake aende kwenye kamati ya Bunge na andiko lake, hapa tunazungumzia mkopo mmojammoja aende aeleze anataka kukopa nini kwa ajili ya nini, anataka kukopa wapi kwa masharti gani, kamati ya Bunge itafakari na ikiona yafaa basi imkubalie au ikiona haifai ikatae,” amesema.
Amesema suala la kukopa fedha kwa niaba ya wananchi ni dhamana kubwa, hivyo chombo cha uwakilishi wa wananchi ambacho ni Bunge kiwe sehemu ya usimamizi wa ukopaji.
Amesema Bunge kwa asili yake linaweza likaleta wataalamu huru wa kuangalia ombi la mkopo likawashauri kwa utaalamu zaidi kuliko wataalamu wa Serikali ambao alidai mawazo yao yanaishia kukopa tu.
Amesema mwaka 2021 Tanzania ilipata mkopo wa Sh1.3 trilioni kutoka IMF kwa ajili ya ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Uviko-19, taarifa ziliwekwa wazi na uwazi huo ulisaidia mashirika yasiyo ya kiserikali yaliyopo kwenye maeneo tofauti kufuatilia kuhakikisha utekelezaji unakuwa mzuri.
“Kwa hiyo uwazi ni muhimu sana, kuna wakati wanakopa hela hatujui wanakopa za nini tunakuja kujua baadaye likishakuwa deni kwenye ripoti za madeni kwa hiyo kwa mfano ule tuliokopa Sh1.3 trilioni zilikuwa za uwazi kwa hiyo ziliwapa nafasi mashirika ya kiraia kufuatilia kile walichokopea kinafanyika kama kilivyokusudiwa,” amesema.
Kuhusu hali ya deni la Taifa Mwakagenda amesema ni kubwa na kiwango chake ni kati ya Sh80 trilioni na Sh90 trilioni kwani takwimu zinatofautiana.
Ofisa mtafiti wa utetezi wa sera kutoka Shirika la Afrodad, Diana Muchoge amewataka wananchi kuanza kufuatilia bajeti ya Taifa na kuhoji ili wajue fedha zinazotengwa kwa ajili ya bajeti zinakwenda wapi.
Amesema washiriki kwenye mchakato mzima wa kutengeneza bajeti ya Taifa na wasione kuwa ni kitu kigumu kwa kuwa wana haki ya kujua fedha zao zinatumikaje kwenye masuala ya nchi.
Mshiriki wa mkutano huo, Pili Msengi ametaka kujua fedha zinazokusanywa kama kodi za mapato na kwa wafanyabiashara nchini zinatumika vipi kwani kila siku deni la Taifa linaongezeka na hakuna dalili ya kupungua.
Pia ameitaka Serikali kutoa msimamo wa uchumi wa nchi kama bado upo kwenye kiwango cha juu, cha kati au umeshuka kutokana na mtikisiko wa uchumi kutokana na ugonjwa wa Uviko-19 na vita vinavyoendelea kwenye baadhi ya mataifa duniani.