Biteko awataka makatibu mahsusi kujiendeleza, kuwa kielelezi cha huduma bora

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko ametoa wito kwa makatibu mahsusi nchini  kujiendeleza kitaaluma ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia sambamba na kuboresha utendajikazi wao. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Ameyasema hayo leo Alhamisi Jijini Mwanza wakati akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kufungua Mkutano wa 11 wa Kitaaluma wa Makatibu Mahsusi.

“Kama mnavyofahamu kuwa dunia ya leo ni kijiji kutokana na mabadiliko ya teknolojia na utandawazi ambayo kwa kiasi kikubwa unachochea maendeleo ya teknolojia hususan Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

“Ni jukumu lenu kama chama cha kitaaluma kuwa na mkakati  wa kushawishiana  kujiendeleza kitaaluma kwenda sambamba na mabadiliko ya TEHAMA.  Dunia ya leo haitumii tena teknolojia ya ‘type writer’ kama zamani ambavyo wachache wenu mliomo humu mlishatumia”, amesema Dk. Biteko.

Amefafanua “Mfumo wa kisasa wa matumizi ya kompyuta na vishikwambi ambao kwa pamoja unarahisisha utendaji kazi wenu, ni jukumu lenu kwa kada yenu waandishi waendesha ofisi kuhakikisha kuwa mnabobea katika fani hii na matumizi ya  vifaa hivi kwenye kada yenu na hivyo ni muhimu mkafahamu matumuzi yake sahihi,” amesema.

Aidha, Dk. Biteko ametoa rai kwa makatibu mahsusi hao kutoa huduma bora kwa wateja wanaofika katika ofisi zao.

“Fanyeni kila mmoja anayekuja ofisini kwenu atoke na furaha akiamini kuwa kodi anayolipa inamlipa mwenyewe katika kupata huduma bora, jinyimeni na kujizuia sana kuwa na kauli za kuvunja moyo kwa wateja wanaokuja kwenu na wakati wote mkiona miongoni mwenu mmoja wenu awe kwenye ofisi kubwa au ndogo mwenye tabia isiyofaa basi mkemeeni”.

Vilevile amewataka kusaidia wengine katika kutatua changamoto mbalimbali katika maeneo yao ya kazi.

Sambamba na hayo, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali itayafanyiakazi yale yote yaliyopendekezwa na TAPSEA.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema kuwa Serikali imefanya maboresho kadhaa katika kada ya makatibu mahsusi kwa lengo la kuboresha taaluma hiyo nchini.

“Awali taaluma hii ilikuwa inaitwa uhazili na kada yao hawa walikuwa wanaitwa makatibu mahsusi, tangu mwaka jana muundo umebadilika na sasa kwa kada yao wanaitwa waandishi waendesha ofisi  na kiutumishi wamepanda  kwa ngazi ya mshahara hadi kufikia TGSH. Hivyo ni maafisa hawa sasa wanasoma kufikia shahada  hadi ngazi ya ubobevu”, amesema Simbachawene.

Amesisitiza “ Wizara yangu ina jukumu la kuhakikisha inatoa waraka wa kuelezea majukumu haya mapya kwa waajiri ili nao wajue jambo hili”.

Mwenyekiti wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania(TAPSEA), Zuhura Maganga amesema kuwa lengo la mkutano huo ni kudumisha taaluma, kukuza uwajibikaji, kuipa hadhi taaluma yao, kuboresha maslahi yao pamoja na kutoa huduma bora kwa waajiri na wananchi.

Ametaja baadhi ya mafanikio ya chama hicho kuwa ni kuishawishi Serikali kuanzisha shahada ya uhazili katika Chuo cha Uhazili Tabora na Chuo cha Utumishi wa Umma pamoja na kuboresha muundo wa maendeleo wa kada ya waandishi waendesha ofisi hadi kufikia daraja la afisa mwendesha ofisi mkuu.

Pamoja na mafanikio hayo, Zuhura ameiomba Serikali na waajiri nchini kuruhusu makatibu mahsusi kushiriki katika mikutano hiyo ya kitaaluma pamoja na kuwalipia ada za ushiriki.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema kuwa Serikali kupitia Mamlaka ya Usambazaji Umeme Vijijini (REA) imetoa fedha za kiasi cha shilingi bilioni 56 kwa ajili ya mradi wa  usambazaji umeme vijijini na shilingi bilioni 12 kwa ajili ya mradi wa ujazilizi  wa umeme. Hata hivyo kwa sasa mkoa huo unatumia kiasi cha megawati za umeme  73 ikilinganishwa na uzalishaji wa  megawati 183.

Mkutano huo wenye kaulimbiu;“MAFANIKIO HUANZA NA UAMUZI BORA WA UTENDAJI, TUTUMIE MUDA VIZURI KWA KUFANYAKAZI NA KULETA TIJA” ulioanza Mei 20, 2024  umehudhuriwa na washiriki zaidi ya 5000 kutoka mikoa yote  nchini.

Related Posts