Dar es Salaam. Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Albert Chalamila amesema Serikali itajenga kituo kikubwa cha Polisi Mbagala ili kudhibiti matukio ya kihalifu katika eneo hilo.
Kauli hiyo ameitoa jana Jumatano Mei 22, 2024 kwenye uzinduzi wa tawi jipya la Benki ya Maendeleo, lililopo eneo la Mbagala.
“Jambo kubwa ambalo lilinitesa miaka mingi ni usalama na tunashukuru Jeshi la Polisi na tutafungua kituo kikubwa cha Polisi, tunaangalia upande huu kwa jicho kubwa hasa wakati huu tunapojipanga kufanya biashara kwa saa 24,” amesema.
Mbali na kujenga kituo hicho cha Polisi, Chalamila amesema Serikali itajenga kituo kikubwa cha biashara inayofanana na ya Kariakoo ili kurahisisha huduma za biashara kwa mikoa ya kusini, hivyo huduma za kibenki ni muhimu katika eneo hilo.
Awali, Mkurugenzi wa Maendeleo Menki, Dk Ibrahim Mwangalaba amesema tawi hilo limeanzishwa kutoa huduma kwa watu wote zikiwemo huduma za mikopo kwa wamachinga, vikundi, mikopo ya kuku, mikopo ya nisharti jadidifu na mikopo ya nufaika na biashara.
“Kuna mikopo ya uboreshaji makazi na huduma zingine kama utunzaji wa amana za wateja, ubadilishaji wa fedha za kigeni, elimu na ushauri wa biashara na fedha,” amesema Dk Mwangalaba.
Kwa upande wake, Msaidizi wa Askofu Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dean Lwiza amesema sasa Maendeleo Menki ina matawi matano na amana ya Sh90.7 bilioni.
Alisema miaka iliyopita hawakuwa na hizo takwimu, hivyo inaonyesha benki hiyo inayomilikiwa na kanisa hilo inakua, inaaminika na haijaangalia rangi, kabila na imani za watu, badala yake inatoa huduma kwa wote,” amesema.