Dar es Salaam. Dereva bodaboda, Mbwana Kamote (30) na mfanyabiashara Nyatko Ngusi (47) wamehukumiwa kifungo cha miezi sita jela, baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa kilo 120 za korosho, zenye thamani ya Sh2.1milioni.
Kamote na Ngusi, wamehukumiwa kifungo hicho, katika Mahakama ya Mwanzo Kariakoo, jijini Dar es Salaam jana Jumatano, Mei 22, 2024 na Hakimu Gladness Njau, baada ya kuwatiwa hatiani kwa kosa hilo.
Baada ya kutiwa hatiani washtakiwa wameomba mahakama iwape adhabu nafuu kwani hawatarudia tena kutenda uhalifu.
Hakimu Njau ametupilia mbali ombi hilo na kuwahukumu kifungo hicho.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Njau amesema anawahukumu kutumikia kifungo hicho bila faini kwa kuwa washtakiwa hao wameshafikishwa mahakamani zaidi ya mara mbili wakikabiliwa na mashtaka ya wizi.
Amesema ili iwe fundisho kwao, washtakiwa hao watatumikia kifungo cha miezi sita jela.
Katika kesi hiyo, washtakiwa kwa pamoja walidaiwa Februari 22, 2024 saa mbili usiku katika Soko Kuu la Kisutu lililopo Wilaya ya Ilala, waliiba kilo 120 za korosho zenye thamani ya Sh2.1 milioni, mali ya Mpudi Rashid.
Baada ya kusomewa mashtaka yao kwa mara ya kwanza, walikana kutenda kosa hilo lakini upande wa mashtaka ukathibitisha hatia dhidi yao.
Katika hatua nyingine, Kubo Mwandege (26) ambaye ni mlinzi, amefikishwa katika Mahakama hiyo na kusomewa shtaka moja la wizi wa simu yenye thamani ya Sh500,000.
Karani wa mahakama hiyo, Aurelia Bahati amedai mbele ya Hakimu Gladness Njau kuwa Mei 13, 2024 eneo la Upanga katika mtaa wa Seaview Wilaya ya Ilala Dar es Salaam, Mwandege aliiba simu aina ya Samsung J7 yenye thamani ya Sh500,000, mali ya Mathew Urio.
Mshtakiwa amekana kutenda kosa hilo na yupo nje baada ya kutimiza masharti ya dhamana ambayo ni kuwa na wadhamini wawili waliosaini bondi ya Sh200,000 kila mmoja.
Hakimu Njau ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 4, 2024 kwa ajili ya kutajwa.