Raisi anazikwa leo katika eneo Takatifu zaidi kwa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini humo la Imamu Reza lililoko katika mji huo wa Mashhad. Mamia kwa maelfu ya waombolezaji walijipanga barabarani kushuhudia jeneza lake likipitishwa kwenye mitaa.
Wawakilishi wa ngazi za juu kutoka mataifa rafiki na Iran wanaohudhuria ni pamoja na kiongozi wa Bunge la Urusi, Duma, Vyacheslav Volodin.
Kabla ya kuwasili Mashhad, maelfu ya watu wa mji wa Birjand walimuaga kiongozi huyo katika shughuli iliyoandaliwa na serikali. Raisi alikuwa mwakilishi wa Birjand, kwenye Baraza la Wataalamu, linalojumuisha viongozi wa kidini na lenye ushawishi mkubwa nchini Iran.
Mwili wa Raisi uliwasili Mashhad pamoja na miili mingine miwili, ambao kwa pamoja walikufa kwenye ajali ya helikopta siku ya Jumapili.
Shughuli ya leo inatanguliwa na ile ya jana iliyoongozwa na kiongozi wa juu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei mjini Tehran, iliyohudhuriwa pia na maafisa 40 wa ngazi za juu ambao ni pamoja na kutoka Iraq, Pakistan, Qatar, Uturuki, Misri, Tunisia, Kuwait, Urusi, China, Armenia na Azerbaijan, hii ikiwa ni kulingana na shirika la habari la serikali.
Soma: Amir wa Qatar, mawaziri wa nje wa Ghuba waenda Iran kumzika Raisi
Mbali na hayo yaliyojiri huko Mashhad, mjini Tehran maelfu ya waombolezaji pia wamejitokeza kumzika aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amirabdollahian, aliyekufa kwenye ajali hiyo pamoja na Raisi.
Waziri anayekaimu nafasi hiyo Ali Bagheri Kani aliyehudhuria pia mazishi, amemtaja Amirabdollahian kama shahidi aliyejitoa kuhakikisha kunakuwepo na mapinduzi ndani ya wizara yake.
Mmoja ya raia wa Iran ambaye hakutaka kutambulishwa alipoulizwa ikiwa anahisi kifo hicho kinaweza kuleta sintofahamu kwenye wizara hiyo alisema “Ni wazi kwamba hakutakuwa na mabadiliko, nikimaanisha kwamba sera zetu zote za nje zitaendelea kama kawaida kama katiba inavyoelekeza pamoja na maagizo ya kiongozi wa juu.”
Ikumbukwe, Raisi alichaguliwa kuwa rais mwaka 2021, akimrithi Hassan Rouhani aliyekuwa na misimamo ya wastani. Alirithi taifa hilo likiwa linakabiliwa na hali mbaya kiuchumi kutokana na vikwazo vya Marekani kutokana na shughuli za nyuklia za Iran.
Soma pia: Iran yaomboleza kifo cha Rais wake
Pembezoni mwa haya yote, viongozi wa kile kinachojulikana kama “muhimili wa upinzani” unaoongozwa na Iran wamekutana mjini Tehran na kujadiliana masuala kadhaa kuanzia hali ya sasa ya kisiasa, kijamii na vita vya huko Gaza.
Kundi hilo linawakutanisha washirika wa kikanda wa Iran katika vita dhidi ya Israel, ambao ni pamoja na Hamas, Hezbollah wa Lebanon, Houthi wa Yemen na makundi ya Shia yaliyoko Iraq na kulingana na vyombo vya habari wametilia mkazo kuviendeleza vita hivyo hadi ushindi kamili utakapopatikana.