Na Chalila Kibuda,Michuzi TV
Kampuni ya Kijapan ya Saint Parts ya kutengeneza magari nchini imeipatia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) injini Nne za kufundishia fani ya ufundi magari kwa ajili ya kuimarisha utoaji mafunzo katika vyuo vya VETA.
Akizungumza wakati wa kupokea vifaa hivyo, leo tarehe 24 Mei, 2024, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema vifaa hivyo vitachangia kuimarisha utoaji mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi kuendana na ukuaji wa teknolojia ya magari inayobadilika kila mara huku Tanzania ikiwa ni watumiaji wakubwa wa magari ya Kijapan.
CPA Kasore amesema VETA kupitia vyuo vyake nchini imejidhatiti katika kutoa mafunzo yanayoendana na mahitaji ya soko la ajira na kuishukuru kampuni hiyo kwa kuwezesha vifaa hivyo muhimu kwa mafunzo ya ufundi wa magari.
Meneja Masoko wa Kampuni ya Saint Parts, Kanya Phiri, amesema kuwa wameguswa kutoa vifaa hivyo kwa lengo la kuongeza wigo wa utoaji mafunzo ya ufundi magari kwa vijana wa Kitanzania.
Phiri amesema kuwa kutokana na uwepo wa magari mengi ya Kijapan hapa nchini, uhitaji wa mafundi wa kuhudumia magari hayo ni mkubwa na kwamba ni fursa ya kuongeza ajira kwa vijana kwenye eneo la ufundi magari.
Aidha amesema kuwa Kampuni hiyo itashirikiana na chuo cha VETA Dar es Salaam na Vyuo vingine vya VETA nchini kwa kutoa fursa ya mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi na walimu ili kuwawezesha kubobea kwenye eneo la ufundi wa magari.
Mwanafunzi wa Fani ya Umeme wa Magari, Halima Mabrouk amesema kuwa msaada huo ni muhimu kwao katika kuendeleza ujuzi wa utengenezaji wa magari katika mifumo yote.
Amewahamasisha wasichana kutumia fursa ya mafunzo ya ufundi stadi yanayotolewa na vyuo vya VETA kujipatia ujuzi.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, akiwa katika picha ya pamojà mara baada ya kupokea msaada wa Injini Nne za kujifunzia wanafunzi wa mafunzo ya ufundi Fani ya Ufundi Magari kutoka Kampuni ya Kijapan ya Saint Parts nchini katika hafla iliyofanyika Chuo cha VETA Chang’ombe jijini Dar es Salaam.
Meneja Masoko wa Kampuni ya Kijapan ya Saint Parts ya Utengenezaji magari nchini Kanya Phiri akizungumza dhamira ya kutoa msaada katika Chuo cha VETA Chang’ombe jijini Dar es Salaam.
Mwanafunzi wa Fani ya Umeme wa Magari wa Chuo cha VETA Chang’ombe Halima Mabrouk akitoa shukurani kwa msaada uliotolewa katika Chuo hicho,jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, akizungumza mara baada ya kupokea msaada wa Injini Nne za kujifunzia wanafunzi wa mafunzo ya ufundi Fani ya Ufundi Magari kutoka Kampuni ya Kijapan ya Saint nchini katika hafla iliyofanyika Chuo cha VETA Chang’ombe jijini Dar es Salaam.