Kanuni mpya za rufaa za ununuzi wa umma kuanza kutumika 2024/25

Dodoma. Kanuni mpya za Rufaa za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2024, zitaanza kutumika katika mwaka ujao wa fedha wa 2024/25.

Inaelezwa zitapunguza muda wa kushughulika na malalamiko ya rufaa za michakato ya ununuzi wa umma.

Kanuni hizo zinazotokana na kupitishwa kwa marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023, zitapunguza muda wa kazi wa siku saba kwa ajili ya kusubiri malalamiko ya wazabuni kabla ya kutoa tuzo hadi siku tano za kazi.

Katibu Mtendaji wa Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA), James Sando amesema hayo leo Mei 12, 2024 wakati wakipokea maoni kutoka kwa wanunuzi kuhusu uandaaji wa kanuni.

“Tunatarajia kanuni hizi pamoja na sheria yote yakienda vizuri mwaka wa fedha unaokuja 2024/25 zitakuwa zinatumika,” amesema.

Amesema anaamini kanuni hizo zitapunguza changamoto kwenye rufani za manunuzi ambazo awali zilikuwa zikilalamikiwa na wazabuni nchini.

Kamishina wa Sera ya Ununuzi wa Umma, Wizara ya Fedha, Dk Frederick Mwakibinga aliyekuwa mgeni rasmi katika kikao hicho amesema sheria hiyo mpya ya ununuzi wa umma imeboresha masuala kadhaa yakiwemo kupunguzwa muda wa kushughulikia malalamiko na rufaa zinazotokana na michakato ya ununuzi wa umma.

Ametoa mfano muda wa siku saba za kazi kwa ajili ya kusubiri malalamiko ya wazabuni kabla ya kutoa tuzo umepunguzwa na kuwa siku tano za kazi.

“Muda huo hautajumuisha njia za ununuzi ambazo hazihitaji ushindani. Muda wa ofisa masuuli kushughulikia malalamiko ya zabuni umepunguzwa kutoka siku saba za kazi hadi siku tano za kazi pale ambapo hataunda jopo,” amesema.

Amesema endapo ofisa masuuli ataunda jopo la mapitio ya malalamiko atakuwa na siku saba za kazi na atatakiwa kuwajulisha washiriki wote wa zabuni juu ya uundwaji wa jopo hilo.

Amesema sambamba na hilo muda wa PPAA kushughulikia malalamiko au rufaa umepunguzwa kutoka siku 45 hadi siku 40.

Mwakilishi wa Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA) katika kikao hicho, Lipu Rweyemamu amesema kanuni hizo zitaboresha ushughulikiaji wa rufani zinazotoka kwa wazabuni na wanunuaji kwa sababu ya mabadiliko yaliyofanyika katika sheria mpya ya manunuzi iliyopitishwa na Bunge mwaka jana.

Amesema mabadiliko hayo yataathiri pia vyombo vingine kama vile Mamlaka ya Manunuzi ya Umma (PPRA), PPAA na taasisi za ununuzi zote.

“Kama sheria mama imeshawekwa pale inalazimisha sheria nyingine zibadilishwe ili kwenda sambamba na mabadiliko hayo kwa ajili ya ufanisi na uwajibikaji kwa pande zote mbili,” amesema.

Sheria ya Ununuzi wa Umma ilipitishwa na Bunge Septemba, 2023.

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amesema itaweka masharti bora ya usimamizi wa ununuzi wa umma, ugavi na uondoshaji wa mali kwa njia ya zabuni.

Related Posts