Makipa watavyoiweka katika wakati mgumu Stars kuelekea AFCON

IMESALIA miezi saba kabla ya kufika mwaka 2025 ambapo Tanzania itashiriki fainali za mataifa ya Afrika mwakani nchini Morocco.

Tanzania ni miongoni mwa timu nane zilitakazo cheza michuano hiyo ikiwemo Somalia, Djibouti, Sao Tome, Chad, Mauritius, Sudan Kusini, Liberia na Eswatini.

Asilimia kubwa ya wachezaji wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’ ina mabeki wengi wenye ubora wa kushindana kimataifa, Mohamed Husein wa Simba, Lameck Lawi wa Coastal, Lusajo Mwaikenda wa Azam FC, Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Dickson Job na Bakar Mwamnyeto wa Yanga.

Shida inakuja eneo la makipa ambalo kwa kiasi fulani makipa wazawa wamekuwa wakipata wakati mgumu mbele ya wageni jambo linaloipa wakati mgumu Stars kama halitabadilika.

Timu zenye ushindani ligi kuu yaani Simba, Yanga na Azam zote makipa wanaocheza na kupewa nafasi ni wageni jambo linaloiweka hatiani Stars.

Kikosi cha Simba kina makipa wanne, mmoja wa kimataifa, Ayoub Lakred na watatu wazawa, Aishi Manula, Ali Salim na Hussein Abel.

Hakuna asiyejua ubora na makubwa yaliyofanywa na Tanzania One, Manula ambaye amekuwa msaada mkubwa kwenye kikosi cha timu ya taifa.

Manula aliumia Machi 22 akiwa kwenye majukumu ya timu ya taifa, kwenye mechi ya kirafiki ya michuano ya FIFA Series kati ya Tanzania na Bulgaria na atakuwa nje ya uwanja akiuguza majeraha kwa miezi sita.

Tangu aumie ilitabiriwa kuwa, Ally Salim ndie angekuwa mbadala wa kipa huyo lakini kwa sasa Mmorocco, Lakred ndio anaonekana kuziba pengo hilo.

Salim amecheza dakika 630 dhidi ya Mtibwa Sugar, Dodoma Jiji, Coastal Union, Tanzania Prisons, Singida Fountain Gate na Ihefu nyumbani na ugenini tangu hapo hajacheza mechi ya ligi.

Hadi sasa makipa wazawa hawana muendelezo mzuri kwenye michezo ya ligi kwani ukiachana na Ali Abel hadi sasa hajacheza mechi yoyote kwenye michezo 27 ya ligi hivyo ni jambao litakalo igharimu Stars kuelekea Afcon 2025 na 2027.

Ubora wa kipa wa Yanga, Djigui Diara kwenye kikosi hicho unawapa wakati mgumu wazawa, Metacha Mnata na Abuutwalib Mshery ambao mara kadhaa wamekuwa wakipata namba.

Yanga imecheza fainali Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita ikimtumia zaidi Diara na hadi inafika hatua hiyo Metacha alicheza dakika 90 pekee kwenye mechi ya kumalizia makundi dhidi ya TP Mazembe.

Kama ilivyo msimu uliopita, mwaka huu Yanga ilicheza robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika na Metacha alifanikiwa kucheza dakika 90 tu dhidi ya CR Belouzdad ugenini timu hiyo ikipoteza kwa mabao 3-0.

Metacha ndio aliyecheza dakika 180 kwenye michuano ya kimataifa na kwenye msimu huu amecheza dakika 238, KMC na Kagera Sugar (90) na Prisons akicheza dakika 58.

Kwa Mshery hadi sasa ameitumikia klabu hiyo kwa dakika 122, dhidi ya Coastal Union (90) na Tanzania Prisons (32).

Wazawa wote wawili ambao ndio sehemu ya kikosi cha Stars wamekosa muendelezo wa kucheza jambo ambalo kama hawatapata nafasi wanaweza kuisababishia mtihani mkubwa timu ya taifa. 

Imesalia miezi saba kumaliza mwaka 2024 na mwakani ndio Tanzania inaandaa mashindano ya Afcon 2025 lakini kwa Azam FC hadi sasa hakuna matumaini kwa makipa wazawa.

Azam ina makipa wanne watatu wa kigeni, Mohammed Moustafa, Ali Ahmada, Abdulai Idrisu na mzawa Zuberi Foba ambaye alipandishwa msimu uliopita kwenye kikosi cha vijana.

Licha ya Foba kupandishwa hajawa na muendelezo mzuri wa kupewa namba mbele ya Msudan Mustafa ambaye anafanya vizuri.

Wakusanya kodi wa Manispaa ya Kinondoni, KMC wana utajiri wa makipa wazawa wakiwa nao wanne lakini Wilbol Maseke ndio amekuwa akipewa nafasi kubwa ya kucheza.

Maseke bado hana uzoefu na mashindano ya kimataifa na kwenye ligi ameruhusu mabao 38 sawa na wastani wa kuruhusu bao moja kwa kila mchezo.

Kama ilivyo kwa Simba, Yanga na Azam wachezaji wa kigeni kuonekana na nafasi kubwa ya kupata namba ndivyo ilivyo kwa Namungo ambao wana makipa watatu.

Mrundi Jonathan Nahimana anapewa nafasi kubwa ya kucheza na hadi sasa ana clean sheet saba lakini makipa wengine, Deogratius Munishi ‘Dida’ na Lucas Chembeja ambapo kutopata namba kunaidhohofisha Stars eneo la makipa.

Makipa wote wawili wa Mashujaa uwezo wao unafanana, Eric Johora na Patrick Muntary wakiosajiliwa msimu huu.

Licha ya kusajiliwa msimu huu lakini bado hawajaonesha ushindani kwa makipa wengine, kwa Johora ambaye msimu uliopita alitemwa na Yanga baada ya kuambulia benchi.

Mkongomani, Ley Matampi ambaye ndio kinara wa cleansheet akigongana na Diara wenye nazo 13 jambo linalompa kibarua kigumu mtanzania Chuma Ramadhani nafasi ya kucheza.

Hadi sasa ukitaja makipa wazawa wanaofanya vizuri ligi kuu huwezi acha jina la Khomein Abubakar ambaye wakati anasajiliwa msimu huu hakuna aliyedhani kama ataisaidia timu hiyo.

Licha ya kuwa hayupo kwenye 10 bora ya makipa wenye clean sheet nyingi lakini amekuwa na msaada mkubwa kwa Ihefu.

Mbali na Khomein kuna wazawa wengine Fikirini Bakari na Shaaban Kado ambao licha ya kucheza pia lakini hawana uzoefu mkubwa na michuano ya kimataifa.

Kitendo cha Yona Amos kufanya vizuri akiwa na Tanzania Prisons tetesi zilisemekana Yanga ipo mawindoni kuinasa saini ya kipa huyo kupisha nafasi ya Metacha ambaye ataachana na mabingwa hao msimu huu.

Amos ana clean sheet nane na kuisaidia timu hiyo ikibaki nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi na pointi 33.

Kama ataendelea kucheza na kuwa na muendelezo wa kiwango chake basi anaweza kuleta ushindani kwa makipa wazawa.

Singida ina makipa wawili, Benedict Haule na Beno Kakolanya ambaye ana uzoefu wa baadhi ya mechi za kimataifa tangu akiwa Simba, Yanga na Stars

Ukiachana na Manula kuna Kakolanya ambaye ana uzoefu alioupata kwenye timu kubwa kwa muda aliocheza lakini kama ataendela kukaa nje ni wazi litakuwa pigo lingine baada ya lile la ‘Tanzania One’.

Licha ya Geita kutofanya vyema ligi kuu lakini kipa wake, Constantine Malimi anafanya vizuri na ana clean sheet tisa akiwa kwenye orodha ya makipa bora watatu na akiwa anaongoza kwa wazawa.

Kwa Geita, Ramadhan Chalamanda mwenye clean sheet tano na Allen Ngereka ndio wazawa waliopewa dhamana ya kuliweka salama lango la timu hiyo salama lakini badala yake ndio timu ambayo kama haitabadilika basi inaweza kushuka daraja.

Ukiachana na timu hizo kuna Mtibwa Sugar, Tabora United, Dodoma Jiji na JKT Tanzania ambao licha ya kuwa na makipa wazawa lakini wamekosa uzoefu na muendelezo.

Related Posts