WAFUASI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wanaharakati hivi karibuni wamekuwa wakifanya maandamano wakishinikiza kupatikana Katiba Mpya iliyotokana na wananchi wenyewe. Anaandika Elvan Stambuli… (endelea).
Chama Cha Mapinduzi (CCM) hawataki na wameendeleza ubabe kwani kuanzia ya Uhuru Katiba ya mwaka 1961 (Tanganyika) hadi ya mwaka 1977, zimetokana na ubabe wa watawala na chama chao.
Katiba ya Uhuru ya 1961 ndiyo ya kwanza na ilijulikana pia kama “The Tanganyika (Constitution) Order in Council” kwa lugha ya Kiingereza, ilitiwa sahihi na Malkia wa Uingereza na kuletwa kwetu bila kuwa na mjadala wowote na wananchi. Iliweka muundo wa Serikali na Bunge kwa mfumo wa Serikali ya Uingereza ujulikanao kama Westminster.
Katiba hiyo haikutambua haki za binadamu. Kwa hiyo, ukatili wa vyombo vya dola ulikuwa mkubwa. Chini ya ibara ya 46 (1) ya Katiba hiyo, Gavana wa Tanganyika (Sir Richard Turnbull), ambaye aliendelea kutawala kumwakilisha Malkia wa Uingereza kwa ombi maalumu la Waziri Mkuu wa kwanza, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hadi mwaka 1962.
Katiba hii iliwakilisha kufikia kikomo cha utawala wa Kikoloni, na sifa yake pekee ni kwamba, ilisimika uhuru na ukuu wa Bunge lenye kuwakilisha wananchi kuwa juu ya mihimili yote ya dola na kwa Bunge kusimamia Serikali.
Katiba ya Jamhuri ya 1962 ilipatikana kwa mapambano kati ya tabaka la viongozi wachache ndani ya chama tawala cha Tanganyika African National Union – TANU, waliotaka Mwafrika pekee ndiye ashike madaraka yote ya nchi, na kwamba uraia uwe ni kwa Waafrika tu.
Hii lilisababisha mjadala mkali bungeni, huku Mwalimu Nyerere ambaye wakati huo alikuwa Waziri Mkuu akiwatuhumu wenzake kugeuka “makaburu wabaguzi wa rangi”.
Katika Bunge hilo Muswada wa Uraia ulipita kwa shida na kuanzia hapo, Serikali ikaingiwa hofu ya mfumo wa demokrasia aina ya Westminster na kutafuta njia ya kuwaziba midomo wabunge.
Januari 16, 1962, kiliitishwa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya TANU kwa shinikizo la wajumbe waliotaka Gavana aondoke ili Tanganyika iwe Jamhuri.
Katika Bunge kulifutwa viti vya Bunge kwa ajili ya watu wa mataifa yasio Waafrika (minority races) na kukaharakishwa zoezi la kujaza nafasi zilizoshikiliwa na Wazungu ili zishikwe na Waafrika. Nyerere hakutarajia mashambulizi kama hayo yaliyomkumbusha mtafaruku kama huo bungeni juu ya Muswada wa Uraia, Oktoba 1961.
Mwalimu alibaini mara moja kwamba nafasi yake na ile ya TANU ilikuwa katika rehani; akaamua kujiuzulu Uwaziri Mkuu na kumwacha Rashidi Mfaume Kawawa kushika nafasi hiyo.
Unafanyika upotoshaji kwamba Mwalimu Nyerere aliachia ngazi ili akaimarishe chama. Gazeti maarufu la New York Times la Februari 3, 1962 (safu ya mhariri) liliandika ukweli: “Inaonekana kwamba Nyerere amekumbwa na mkasa unaowapata viongozi wa Kiafrika wenye siasa baridi/ wasio wanamapinduzi. Jinsi alivyobanwa na kupewa shinikizo na wanamapinduzi, ameng’olewa!
Hatua hiyo ilifungua mlango kwa mchakato wa Katiba kuifanya Tanganyika kuwa Jamhuri. Januari 16, 1962, NEC ya TANU ilikutana na kutoa pendekezo kwa Serikali, Tanganyika iwe Jamhuri ndani ya Jumuiya ya Madola, Desemba 9, 1962.
Akiwasilisha bungeni muswada juu ya hili, wakati huo Nyerere akiwa kwenye viti vya nyuma bungeni, Kawawa alitaja sababu kuu mbili: kwanza ilikuwa ni kuanzisha nafasi ya mtawala (Rais Mtendaji) mwenye nguvu na uwezo wa kutenda. Pili, kuiwezesha Serikali kuingilia kikamilifu maisha ya wananchi na sekta za kijamii na kiuchumi bila kuhojiwa; Serikali yenye mamlaka hodhi na isiyowajibika kwa chombo chochote.
Madhumuni ya Muswada huo yalikwenda kinyume na mfumo wa Westminster unaotambua ukuu wa Bunge katika kusimamia Serikali.
Ulizaa mtawala “Rais mbabe” (Imperial Presidency) asiyehojika na ndiyo sababu ya Kamati ya Mabadiliko ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba iliwasilisha mapendekezo Rais apunguziwe madaraka.
Katiba hii nayo haikutokana na wananchi, bali ilitokana na kikundi cha wanasiasa wachache ndani ya chama waliokuwa na uroho wa madaraka.
Na ili kudhibiti uhuru wa kisiasa na wa kujieleza, vyama vyote vya siasa, mbali na TANU, vilitoweka kwani viongozi wake ama walifukuzwa nchini au walitiwa kizuizini; haki ya kusajili vyama na kuendesha mikutano ilidhibitiwa.
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulianzishwa kwa njia ya dharura mwaka 1964. Hapakuwa na muda wa kuandaa Katiba na ili kuupa Muungano uhalali, iliazimiwa, chini ya Mkataba wa Muungano, ibara ya (ii), (iii) na (iv), kwamba Kwamba katika kipindi cha mpito hadi Bunge la Katiba litakapoitishwa kupitisha Katiba Jamhuri ya Muungano, Katiba ya Muungano itakuwa ndiyo hiyo hiyo Katiba ya Tanganyika itakayorekebishwa kuingiza mambo ya Muungano.
Mkataba haukutaka kuingilia mambo ya Serikali za Tanganyika na Zanzibar na Sheria zake zinazosimamia mambo yasiyo ya Muungano.
Tanganyika na Zanzibar kuungana kuunda dola moja, ilitamkwa kuwa “Sheria za Tanganyika zilizopo na Sheria za Zanzibar (kwa mambo yasiyo ya Muungano) zitaendelea kuwa na nguvu katika nchi hizo”, kwa maana ya nchi zisizokuwa dola.
Kwa tafsiri hii, wanaosema Zanzibar ni nchi isiyo dola hawajakosea. Lakini swali la kujiuliza ni je, Tanganyika ilikwenda wapi baada ya kudumu kwa jina tu bila matendo hadi mwaka 1965?
Katiba ya mwaka 1977 iliundwa na inasimama kwenye mafiga matatu iliyorithi kutoka Katiba ya 1962 na ya 1965 ambayo ni katiba inayomuuingiza rais mbabe na inatambua muundo wa serikali mbili; na tatu, inatambua serikali ya chama kimoja.
Kuingia kwa mfumo wa Vyama vingi vya Siasa mwaka 1992 na marekebisho yaliyofanyika hakujairekebisha Katiba ya mwaka 1977.
Iliundwa Tume ya watu 20 kupendekeza Katiba, wote kutoka CCM. Tume hiyo ndiyo ilipendekeza kuunganishwa kwa TANU na ASP kuunda CCM. Mapendekezo yaliwasilishwa kwenye kikao cha siri cha NEC.
Siku tume hiyo ya Katiba ilipoteuliwa, ndiyo siku hiyo Bunge la Katiba (Constituent Assembly) ambalo wajumbe wake walikuwa wabunge wote wa Bunge la Muungano bila mwananchi hata mmoja lilipoteuliwa.
Mapendekezo ya Tume/NEC yaliwasilishwa kwenye Bunge la kawaida, Aprili 25, 1977 na kujadiliwa kwa muda chini ya saa mbili kutokana na kile kiongozi wa shughuli za serikali bungeni, Makamu wa Pili wa Rais, Rashidi Kawawa, alisema “Maamuzi ya NEC hayajadiliwi”.
Alisema, “Kwa kuwa mapendekezo haya yamekwisharidhiwa na NEC, Bunge hili halina mamlaka ya kwenda kinyume na kile kilichoridhiwa na NEC isipokuwa kupitisha tu”. Hivyo katiba ikapita na ndiyo maana tunasema haikuwa na ridhaa ya wananchi!
Akifungua Bunge la Katiba mjini Dodoma, Machi 21, 2014, Rais Jakaya Kikwete ambaye aliunda tume ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu katiba mpya, aliiponda hadharani Tume hiyo ya Katiba aliyoiteua yeye mwenyewe kwamba mapendekezo mengi yaliyotolewa na Tume hiyo hayafai.
Rais aliendelea kusema kwamba, baadhi ya mapendekezo ya Tume hatayavumilia na kwamba wanaotaka yatekelezwe wasubiri aondoke madarakani.
Kwa kauli hii kutoka kwa Mwenyekiti wa chama tawala ni mwendelezo wa “ubabe” wa michakato ya Katiba za 1962, 1965 na 1977.
Mchakato huu ulianza vizuri, na kwa Rais, baada ya kupokea Rasimu ya Tume, kuwaasa wananchi kujiandaa “kisaikolojia” kupokea muundo wowote wa Serikali utakaopendekezwa na Tume kutokana na maoni ya wananchi.
Kwa hali ilivyo, Katiba itakayotokana na kupuuzwa kwa mapendekezo ya Tume iliyokusanya maoni ya wananchi haiwezi kuwa ya kidemokrasia; itakosa uhalali wa kijamii.