Unguja. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameeleza kukerwa na kutotekelezwa baadhi ya mipango inayopelekwa barazani kila mara na baadaye kurejeshwa kama mipya.
Pia, wawakilishi hao wakati wakichangia bajeti ya Wizara ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ, wameeleza kukerwa na halmashauri kushindwa kuzoa taka, kitendo kinachotia doa mji huo wa kitalii.
Sababu inayotajwa kuchangia uchafu wa mji huo ni manispaa na halmashauri zake kukosa uwezo kuondosha taka kwa sababu ya kukosa vitendea kazi, yakiwemo magari.
Mwakilishi wa Fuoni, Yussuf Hassan Iddi alisema hali za ofisi za mikoa zinatia aibu na haziendani na hadhi ya viongozi hao.
Alihoji sababu za kushindwa kuzijenga, kwani hata katika bajeti ya mwaka jana walielezwa zingejengwa, lakini wanashangaa kuona hakuna utekelezaji uliofanyika, badala yake zimepangwa kujengwa katika bajeti hii ya mwaka 2024/2025.
Hata hivyo, wamesema licha ya kupanga kuzijenga, hakuna kiwango cha fedha kilichotengwa kwa ajili hiyo.
“Mwaka jana tuliletewa taarifa za kuboresha ofisi hizi, lakini tumerejeshewa tena mwaka huu, wataalamu wanasema ili uweze kutekeleza, tusitegemee njia moja, tuwe na njia mbadala,” alisema Yusuf.
Katika hatua nyingine, mwakilishi huyo alisema ipo haja ya halmashauri kuongeza kasi katika ukusanyaji wa mapato, kwani inaonekana yapo chini na bajeti zinazopangwa ni ndogo kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake.
Mwakilishi wa Kikwajuni, Nassor Salim Ali alisema kuna changamoto kubwa ya usafi, hasa katika maeneo ya mjini ambako kuna karo zinatiririsha majitaka kutokana na kukosa vitendea kazi katika halmashauri.
“Serikali iweke mikakati kuondoa hilo na shida kubwa ni fedha, leo unafika wakati hata fedha za mafuta hakuna, hawa watu watafanyaje kazi, hili linatakiwa kuangaliwa kwa umakini,” alisema.
Aliyezungumzia jambo hilo pia ni mwakilishi makundi maalumu, Saada Ramadhan Mwendwa ambaye amesema suala la usafi bado changamoto.
“Kiukweli taka bado haziendi vizuri, zinasambaa ovyo, kwa hiyo lazima kuziwezesha manispaa ziweze kufanya usafi.
Awali, akiwasilisha bajeti, Waziri Masoud Ali Mohammed alisema katika bajeti ya mwaka huu wataaanza utaratibu ujenzi wa Ofisi za wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya Unguja na Pemba, kazi ambayo alisema itasimamiwa kwa pamoja na Ofisi ya Rais Fedha na Mipango.