Bangkok. Abiria 211 wamenusurika kifo baada ya ndege waliyokuwa wakisafiria kupata msukosuko angani, ikiwa ni saa 10 tangu iliporuka, huku abiria mmoja akifariki dunia jana Jumanne Mei 21, 2024.
Abiria hao waliokuwa wakisafiri na ndege ya Shirika la Singapore Airlines kutoka London, Uingereza kwenda Singapore, walijawa na hofu kwenye tukio hilo ambapo abiria 30 wamejeruhiwa.
Inaelezwa purukushani ndani ya ndege zilidumu kwa dakika kadhaa zikiwaacha watu wakigonga vichwa vyao na kusababisha majeraha. Aliyefariki dunia ametambulika kwa jina la Geoffrey Kitchen (73), ambaye inaelezwa huenda alipatwa na mshtuko wa moyo kutokana na hofu.
Tukio limetokea wakati ndege hiyo ilipofika Myanmar na baadaye ikalazimika kwenda kutua jijini Bangkok nchini Thailand. Mashirika ya habari ya AFP, AP na The Guardian yameripoti taarifa hiyo.
Pia, ripoti kutoka kituo cha kufuatilia safari za ndege FlightRadar24 zimeonyesha ndege hiyo ilishuka ghafla kwa mita 1,800 katika anga la pwani ya magharibi ya Myanmar.
Ndege hiyo aina ya Boeing 777-300ER iliondoka London Jumatatu na ikakumbwa na msukosuko mkali ikiwa njiani, ikiwa na abiria hao na wafanyakazi 18.
Abiria wengi miongoni mwao wametoka Australia, Uingereza, New Zealand na Singapore.
Shirika hilo la ndege limetoa rambirambi kwa familia ya abiria aliyekufa na limesema linashirikiana na maofisa wa Thailand kutoa msaada wa matibabu huku timu yake ikiwa njiani kuelekea Bangkok mahali ndege hiyo ilipotua.