Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi amekutana na kufanya mazungumzo na wataalam kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania kwa lengo la kujadiliana na kuangalia eneo maalum litakalofaa kwa ajili ya kushuka helikopta zitakazo leta wagonjwa watakaokuja kutibiwa hospitalini hapo.
Kwa mujibu wa Prof. Janabi Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila ni hospitali ya kisasa yenye miundombinu rafiki na kuongeza kwamba Muhimbili ni Hospitali ya Taifa hivyo ni muhimu kuwa na eneo kama hilo ili ikitokea wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura kunakuwepo na mazingira rafiki zaidi ya kufika hospitalini ukilinganisha na kutumia usafiri wa barabara.
Kwa upande wake Bw. Pius kazeze ambaye pia ni Meneja Uendeshaji Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere amesema wameridhika na eneo ambalo wameliona kwani ni kubwa na linafaa ingawa kuna vitu vya kitaalam ambavyo vitafanyiwa kazi.