RAIS wangu mama Samia, wiki iliyopita baada ya kuwa nimekuandikia kuhusu upandaji holela wa bei za mafuta ya nishati, mwana mwema mmoja kati ya wengi walioniandikia, alisema; “kwema ndugu mwandishi?
Binafsi nakuombea Mungu akulinde na akutete dhidi ya watesi wenye lengo la kuihujumu kalamu yako, maana nijuavyo haya uyaandikayo hawayapendi. Wanapenda tuendelee kuwa mbumbumbu ili tuwe mtaji wao. Nasema nuru ya Bwana ikufunike.” Haya ni maombi mazito sana kwangu kutoka kwa wananchi wako unaowaongoza.
Rais wangu mama Samia mwana mwema mwingine akaniandikia namna hii “nakushukuru huchoki kumlalamikia Mheshimiwa Rais, ila kuhusu hili la bei ya mafuta ni kweli wanyonge wanaumia ila wale walioko karibu naye hawana habari maana wao wanaishi kama wako peponi. Wengi ni matajiri kupindukia.”
Rais wangu hii ni sehemu ya mrejesho wa wananchi wako kwa kile wanachokiona. Wanatamani ufanye kitu kwenye bei za mafuta maana zinawaumiza. Kimya chako kinawafanya waone kama huna uwezo wa kufanya chochote. Unakosaje uwezo wakati wewe ndiye rais wa nchi?
Wewe ndiye mwenye sauti ya mwisho yenye mamlaka juu ya kila jambo linalofanyika hapa nchini kwa mujibu wa katiba yetu, hivyo huwezi kushindwa kuamuru bei za mafuta kushushwa. Hamu ya watu wako ni kuona unatoa sauti juu ya uswahili unaofanyika kwenye mafuta na mambo mengine ambayo yanaliumiza taifa kwa maslahi ya wachache.
Rais wangu mama Samia, leo naomba usikilize kilio cha daktari Peter Phissoo ambaye ni mwathirika wa sakata la vyeti feki lililowaondoa wafanyakazi lukuki katika utumishi wa umma enzi za mtangulizi wako, hayati John Pombe Magufuli.
Huyu ni daktari wa watu mwenye taaluma kamili ya udaktari. Hajawahi kughushi vyeti vya taaluma yake ya udaktari. Huyu si kanjanja katika tiba kwa sababu alikaa darasani akasoma akahitimu kwa ufaulu mzuri. Ni daktari aliyetokea darasa la saba na kujiendeleza mpaka kufikia elimu ya stashahada ya juu (Advanced diploma) kwenye masuala ya tiba (Clinical Medicine), aliyoipata katika chuo cha madaktari wasaidizi kilichoko Bombo, Tanga.
Rais wangu mama Samia, leo hii daktari huyu mbobevu katika tiba, amefukuzwa kazi kwa kile kilichoelezwa kukosa cheti cha kidato cha nne. Kwamba kwa miaka yote aliyoajiriwa serikalini tangu mwaka 1987, alikuwa anamwibia mshahara mwajiri wake. Amefukuzwa kazi kwa kilichoitwa ‘wizi wa mali za umma’ yaani anaitwa mwizi kwa taaluma aliyoisomea.
Rais wangu, huyu daktari anastahili kweli kuitwa mwizi? Daktari msomi aliyefanya kozi mbali mbali za utaalamu katika vyuo mbali mbali kikiwemo Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Muhimbili (MUHAS), leo hatakiwi serikalini akidaiwa ni mwizi. Hivi kama mtumishi wa aina hii anaweza kuitwa mwizi wa mali za umma, vipi wale wanaoisababishia serikali hasara ya mabilioni kulingana na taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)?
Rais wangu mama Samia, suala la huyu daktari linahitaji hekima, busara na utu ili kuliamua, kwa sababu linaonekana kugubikwa na hila na roho mbaya ya kukomoana. Watesi wake wanadai kwenye taarifa za utumishi wake alidai amehitimu elimu ya kidato cha nne katika mojawapo ya shule za sekondari hapa nchini, kitu ambacho sio kweli na hicho ndicho kikawa kigezo cha kumfukuza kazi na kufuta kabisa thamani ya taaluma yake aliyoisomea kwa uhalali miaka nenda rudi.
Rais wangu watu wenye hila na roho mbaya ni rahisi sana kuchukua maamuzi ya fukuzafukuza. Hawa wanapenda kukomoana kuliko kujengana. Mchakato wa kumfukuza kazi daktari Phissoo, ni kama vile umegubikwa na utata kwa kiasi ambacho anahisi kutokutendewa haki.
Anasema alichunguzwa na kamati iliyoundwa na mamlaka yake ya nidhamu kuhusu utata wa tuhuma zake lakini hakuwahi kupewa taarifa ya uchunguzi dhidi yake na badala yake alikabidhiwa barua ya kutimuliwa kazi.
Yaani mtu hakuitwa kusikilizwa katika tuhuma, hakupewa taarifa ya uchunguzi kwa wakati, na zaidi hata baada ya kufukuzwa, hakupewa mwenendo wa shauri lake ili kuona namna ambavyo maamuzi ya kumfukuza yalivyofikiwa kwa ajili ya kumwezesha kukata rufaa. Huku kama sio kukomoana ni nini?
Rais wangu mama Samia, hivi kama wenzetu wenye mamlaka hawakulenga kumkomoa daktari Phissoo ilikuwaje tume ya utumishi wa umma ikajikanganya katika maamuzi yake kwa mhusika katika kutekeleza amri ya mahakama kuu?
Tume iliamriwa na mahakama kuu kanda ya Dar es Salaam kusikiliza rufaa ya daktari huyu ambayo awali ilikuwa imetupwa kwa kisingizio cha kuwa nje ya muda. Tume ya Utumishi wa Umma ilisikiliza rufaa siku ya tarehe 07/12/2023 lakini majibu ya rufaa hiyo yanaonekana yalishaandaliwa kabla hata ya rufaa yenyewe kusikilizwa kwa kuwa yaliandikwa tarehe 05/12/2023.
Lakini mama yangu na rais wangu ukirudi katika shauri la msingi, unajiuliza, hili suala la cheti lililotumika kumfukuza kazi huyu daktari, lina mchango gani katika elimu yake ya utabibu? Mbona cheti hakihusiani kabisa na utaalamu wake alioupata kwa kukaa darasani na kuhitimu? Kwamba kwa kukosa cheti cha kidato cha nne miaka yote takribani 32 aliyoitumikia serikali huku akiokoa maisha ya Watanzania ndio imehesabika sifuri na kufukuzwa kazi?
Rais wangu mama Samia kama nilivyosema, hili suala la huyu mtaalamu wetu wa afya, linahitaji busara kuliko hasira. Wewe unaweza kuamuru daktari huyu akarejeshwa kazini kwa sababu hajaghushi cheti cha taaluma.
Amekuwa akilipwa kulingana na taaluma yake. Waambie wasaidizi wako wamrejeshe kazini ili aendelee na kazi. Kama ni hatua nyingine za kumwajibisha kutokana na kujaza taarifa za kuhitimu kidato cha nne wakati hakuwahi kufanya hivyo, ni bora zikafanyika lakini huyu daktari akiwa kazini kuliko kumkomoa kwa kumfukuza kazi kwa namna alivyofanyiwa.
Leo kaka yangu huyu amekosa pa kuishi kwa kuwa ameondolewa kazini bila maandalizi. Watoto wake wanaishi maisha ya kuungaunga na mwingine amekatisha masomo kutokana na hali ngumu ya maisha.
Rais wangu haya kweli ndiyo malipo ya mtumishi huyu? Tafadhali ingilia kati suala hili ili kuokoa maisha ya daktari Phissoo kwa sababu nyaraka anayodaiwa kughushi haina uhusiano wala mchango wowote katika kumpatia ajira, kumpandisha daraja kazini wala kumwongezea mshahara. Msaidie huyu ili jasho lake lisipotee. Makala hii imeandaliwa na Leonard Manyama. Anapatikana kwa simu namba 0756888896.