Serikali mbili ni sera ya CCM, si mkataba wa Muungano

MUUNGANO kati ya Tanganyika na Zanzibar uliotimiza miaka 60 tangu kuundwa kwake, tarehe 26 Aprili 1964, umekumbana na changamoto nyingi na mafanikio mbalimbali. Anaandika Alfred Gwakisa… (endelea).

Sehemu kubwa ya changamoto hizo, zinahusiana na utekelezaji wa sera ya Serikali mbili.

Muundo wa Muungano wa serikali mbili ni matokeo ya sera na uamuzi wa chama cha Tanganyika African National (TANU) na Afro Shirazi Party muda mfupi baada ya mkataba wa makubaliano ya muungano kusainiwa.

Mfumo wa serikali mbili haukuwa sehemu ya makubaliano ya mkataba wa Muungano (1964).

Mfumo wa serikali uliokusudiwa na mkataba wa Muungano, ni ule ulioweka mgawanyiko wa wazi wa madaraka baina ya pande mbili yaani serikali kuu na sehemu ziundazo serikali kuu.

Awali, serikali za Tanganyika na Zanzibar zilikubali kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; baada ya hapo, na bila ya kushinikizwa, waasisi wa muungano huu, walikubaliana kupunguza baadhi ya madaraka ya serikali zao kwa serikali hiyo mpya.

Madaraka yaliyosalimishwa kwa serikali ya Muungano iliyokuwa na mamlaka ya pekee kwa Jamhuri nzima yamo katika Ibara ya (4) ya Mkataba wa Muungano, ambao nakala yake inapatikana ndani ya kitabu cha Prof. Issa Shivji, kiitwacho “Pan – Africanism or Pragmatism” (2008).

Ibara ya 4 ya mkataba inataja mambo 11 kuwa ndiyo yatakuwa chini ya Bunge na Serikali ya Muungano. Mambo hayo, ni Katiba na Serikali ya Muungano, Mambo ya nchi za Nje, Ulinzi, Polisi na Mamlaka juu ya mambo yanayohusika na hali ya hatari.

Mengine ni Uraia, Uhamiaji, Mikopo na Biashara za nchi za Nje, Utumishi katika Jamhuri ya Muungano, Kodi ya mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika, ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa zinazozalishwa  nchini na kusimamiwa na idara ya forodha na Bandari, mambo yanayohusu usafiri wa anga, posta na simu.

Rais Jakaya Kikwete (kushoto) na Rais wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein (katikati) wakionesha katiba Mpya

Mamlaka mengine yakabakizwa kwa Tanganyika na Zanzibar ambazo serikali zake zilitarajiwa kuendesha na kusimamia masuala yao ndani ya maeneo yao.  Mkataba wa Muungano uliweka wazi kuwa mamlaka ya Tanganyika, kama ilivyo kwa mamlaka ya Zanzibar, hayakuwa chini ya Serikali ya Muungano.

Wanazuoni mbalimbali wanaonesha kuwa ushirikiano baina ya mataifa yanayozidi mawili ni lazima ufuate moja ya sura tatu zifuatazo:

Muundo wa Serikali moja. Hii hutumika pale ambapo ushirikiano huo sio wa hiyari bali kulazimishwa na mwenye nguvu dhidi ya taifa dogo kama ilivyo katika uhusiano kati ya Uingereza na Ireland ya Kaskazini, serikali inayotokea hapa ni ile ya mfumo wa serikali moja, ambapo nguvu zote za mamlaka zinawekwa chini ya serikali moja.

Hakuna ushahidi kuwa dhana hii ndiyo iliyodhamiriwa ndani ya mkataba wa Muungano (1964).

Inapotokea nchi zaidi ya mbili zimeamua kuungana kwa hiyari, zinaweza kukubaliana kuwa mamlaka halisi yabakie katika nchi moja.

Katika mfumo huu, serikali kuu inakuwa haina nguvu na hupewa tu madaraka. Mfumo wa umoja wa Ulaya unafuata utaratibu huu, ambapo nchi moja moja kama vile Ujerumani, Ufaransa, Ureno na nyinginezo, zina nguvu ya kufanya maamuzi ya mwisho na siyo Bunge la Umoja wa Ulaya au watendaji wake.

Vile vile hakuna ushahidi kuwa hii dhana ilidhamiriwa ndani ya mkataba wa Muungano.

 Muundo wa Shirikisho. Hapa serikali kuu na serikali za nchi washirika ndani ya Muungano huo, zinashirikiana katika madaraka kama ifuatavyo:

Kuanzishwa kwa muungano wa kisiasa wa nchi mbalimbali ili kila nchi ibakie na utawala na uendeshaji wa mambo yake ya ndani (yasiyo ya pamoja au muungano).

Mfumo wa kisiasa ambao nchi zinabakisha karibia mamlaka yake yote ya ndani na kubakisha mambo ya nje, ulinzi, fedha n.k kwa serikali kuu au serikali ya shirikisho.

– Kundi la nchi zilizoungana ambapo kuna serikali moja inayoamua mambo ya nje, ulinzi, fedha n.k lakini kila nchi ikiwa na nguvu za kuamua mambo yake yenyewe nje ya muungano.

Kwa kuusoma Mkataba wa Muungano uliotiwa saini na Julius Kambarage Nyerere – aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Tanganyika na Abeid Amani Karume, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya watu wa Zanzibar, ni dhahiri kuwa mkataba huo ulidhamiria kufuata mfumo wa “shirikisho” na siyo mfumo wa serikali moja ambao mamlaka yote yanarundikwa kwa serikali kuu au mfumo wa matangamano ya serikali za majimbo ambao mamlaka hubakia katika serikali za nchi husika.

Mkataba wa Muungano uliweka bayana mfumo ambao serikali kuu na serikali shiriki kuwa na nguvu zinazoendana, yaani mfumo wa shirikisho ambao kuna mgawanyiko wa Mahakama, Bunge na Rais baina ya serikali kuu na serikali mbili au zaidi, na kila serikali ikiwa na nguvu kamili ndani ya mamlaka yake.

Kwa maana nyingine, chini ya mfumo huu, nguvu za serikali zinapaswa kuchangia na kuunganisha upande mmoja na upande mwingine na siyo upande mmoja kuwa juu ya upande mwingine.

Ufafanuzi wa kesi ya Mahakama Kuu nchini Marekani (1872) unathibitisha chini ya mfumo wa shirikisho, kila serikali inatarajiwa kuwa na mamlaka yake kamili.

“Kuna ndani ya mipaka ya eneo la kila jimbo, serikali mbili ambazo zinafungwa katika utendaji wao, lakini kila moja ikiwa huru kutoka nyingine na zenye sauti ya mwisho katika mamlaka ilizo hodhi. Kila moja ina idara zake; sheria zake pekee; na kila moja ikiwa na mahakama zake zenyewe za kukazia sheria hizo. Hakuna serikali inayoweza kuingia katika eneo la mamlaka ya nyingine wala kuamuru uingiliaji wa watendaji wake wa sheria katika matendo ya mwingine”.

Mamlaka za Utawala: Ilikubaliwa kuwa Mkataba wa Muungano (1964) utakuwa msingi wa Katiba yoyote ya Muungano wa Tanzania.

Kwa mujibu wa Prof. Shivji (2001), Mkataba wa Muungano ulikuwa ni Katiba ya kwanza ya Muungano.

Shivji anasema, kwa mujibu wa Mkataba huo, ilikubaliwa kuwa Katiba ya kudumu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ingepatikana ndani ya mwaka mmoja kupitia Tume ya Katiba na kufuatiwa na Bunge la Katiba.

Hata hivyo, yote haya hayakutekelezwa. Tukiendelea kudhihirisha jinsi gani Mkataba wa Muungano (1964) ulidhamiria mfumo wa shikisho la serikali tatu:

Mosi, utangulizi wa Mkataba wa Muungano unaweka wazi kabisa kuwa mkataba huo ni wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya watu wa Zanzibar. Unasema kuwa marais hao wawili ni wawakilishi wa nchi zao.

Pili, ibara ya 3(b) ya Mkataba huo inaelekeza Makamu wa Rais kama “taasisi”. Kwa mujibu wa ibara hiyo. Katika kipindi cha mpito, Katiba ya Muungano itakuwa Katiba ya mpito iliyorekebishwa ili kuweka.

Nafasi za makamu wawili wa Rais mmoja kati yao (akiwa ni mkaazi wa Zanzibar) atakuwa ndiye kiongozi wa serikali iliyotajwa kwa ajili ya Zanzibar na atakuwa msaidizi mkuu wa Rais wa Jamhuri ya muungano katika utekelezaji wa kazi za kiserikali kwa upande wa Zanzibar.

Ibara hii ilitoa nafasi kwa uteuzi wa makamu wa Rais wawili, na kwa utambuzi mmoja atokee kila upande wa muungano – yaani Tanganyika na Zanzibar. Hii inathibitisha kuwa mfumo wa Muungano uliodhamiriwa na Mkataba wa muungano ulikuwa wa serikali tatu, na sio serikali moja wala mbili.

Tatu, kwa mujibu wa Ibara ya 5 ya Mkataba huo, Sheria zote zilizopo za Tanganyika na Zanzibar zitaendelea kutumika katika maeneo yao bila kuathiri:

–  Masharti yoyote na chombo chenye mamlaka ya kutunga sheria.

– Masharti yatakayowekwa kwa amri ya Rais wa Jamhuri ya Muungano ili yatumike Zanzibar juu ya sheria yoyote inayohusu jambo lolote lililotajwa kwenye ibara ya “4” (hapa ikiwa na maana, masuala kumi na moja ya muungano).

– Mamlaka yoyote kama inaonekana yanafaa au kuhitajika ili kufanikisha muungano na mkataba huu.

Ibara hii ya 5 pia ni uthibitisho kuwa mfumo wa serikali uliodhamiriwa ulikuwa ni serikali tatu kwani inaweka wazi kuwa taasisi za nchi mbili zilizoungana (Tanganyika na Zanzibar) zitabakia kama zilivyo isipokuwa kwa yale maeneo yaliyotajwa.

Nne, ibara ya 6 (a) inaeleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano ataendelea na kazi zake za Jamhuri ya Muungano kwa msaada wa maafisa ambao atawachagua kutoka Tanganyika na Zanzibar na hiyo ifuatane na taasisi husika za utumishi wa umma zilizokubalika kutiwa katika muungano na kubakiza zile ambazo si za muungano kwa serikali mbili husika.

Kwa mujibu wa ibara hiyo ya 6: Rais wa Jamhuri ya Muungano atakuwa ni Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na ataongoza serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa kufuata masharti ya mkataba huu na kwa kusaidiwa na makamu wa Rais waliokwisha tajwa na mawaziri na maofisa wengine atakaowateua kutoka Tanganyika na Zanzibar na watumishi toka serikali zao.

Tafsiri sahihi hapa ni kuwa taasisi nyinginezo za serikali za Tanganyika na Zanzibar zilihakikishiwa kufanya kazi bega kwa bega na taasisi za serikali ya Muungano. Pia kazi zilizohusiana na utumishi wa umma za Tanganyika na Zanzibar zilihakikishiwa kuendelea kuwepo kama zilivyokuwa kabla ya Muungano.

Tano, ibara ya 7 inatoa maelekezo juu ya kuitishwa kwa baraza la kutunga Katiba:

Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kukubaliana na makamu wa Rais ambaye ni kiongozi wa serikali ya Zanzibar:

  • Atateua tume kwa ajili ya kutoa mapendekezo kwa ajili ya katiba ya Jamhuri ya Muungano.
  • Ataitisha baraza la kutunga katiba likiwa na wawakilishi kutoka Tanganyika na Zanzibar katika idadi itayoamuliwa likutane katika kipindi cha mwaka mmoja tokea kuanza kwa muungano kwa madhumuni ya kutafakari mapendekezo ya Tume iliyotajwa juu na kupitisha katiba ya jamhuri ya muungano.

Hapa mkataba unaonyesha wazi kuwa uteuzi wa wajumbe wa tume ya katiba utafanywa na Rais wa Muungano kwa “makubaliano”, sio “ushauriano”, na makamu wa Rais ambaye ndiye kiongozi wa Serikali ya Zanzibar. Na baraza hilo litaundwa na wawakilishi kutoka pande mbili za Muungano kwa kiasi kitachoamuliwa.

Sita, kwa mujibu ibara ya 8 ya Mkataba wa Muungano:

Mkataba huu utahitaji kuthibitishwa kwa kutungiwa sheria na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi la Jamhuri ya watu wa Zanzibar kwa kushirikiana na Baraza lake la Mawaziri, na mkataba kupitishwa na kuundwa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na ya Zanzibar kwa kufuata masharti yaliyokubaliwa.

Ibara hii inazidi kuhimiza juu ya usawa wa nchi mbili zinazounda Muungano (Tanganyika na Zanzibar), na pili juu ya idadi ya serikali na mataifa yaliyohusika, kwa maana nyingine, serikali za nchi za Tanganyika, Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano.

Inaonekana kinacho wachanganya watu wengi ni yaliyomo kwenye ibara ya (4) ya mkataba wa Muungano inayosema:

– Bunge na serikali vilivyotajwa vitakuwa na mamlaka ya mwisho juu ya mambo yote yanayohusu Jamhuri ya muungano na kwa kuongezea mamlaka ya mwisho juu ya mambo yote yanayohusu Tanganyika.”

Hapa serikali ya muungano ilipewa mamlaka kusimamia na kuendesha mambo yote ya Tanganyika. Lakini ikumbukwe:

Kwanza masharti haya yalikuwa kwa ajili ya kipindi cha mpito tu, sio ya kudumu.

Kwa mujibu wa ibara ya 3: Katika kipindi cha mpito katiba ya Jamhuri ya Muungano itakuwa katiba ya Tanganyika iliyorekebishwa ili kuweka:

  1. Chombo cha kutunga sheria na serikali kwa ajili ya Zanzibar kwa mujibu wa sheria zilizopo Zanzibar na vitakuwa na mamlaka ya mwisho katika Zanzibar kwa mambo yote isipokuwa yale tu yaliyo chini ya Bunge na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
  2. Uwakilishi wa Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ya Muungano.
  3. Mambo mengine yatayofaa au kuhitajika ili kuipa nguvu Jamhuri ya Muungano na mkataba huu.

Pili, ni kutokana na kuwepo kwa Tanganyika kieneo na kiserikali ndio maana madaraka yakatolewa kwa mtendaji mkuu wa serikali ya Muungano (Rais) kusimamia na kuendesha mambo ya ndani yanayohusu Tanganyika.

Hivyo, kulikuwa na mamlaka tatu – mamlaka ya Zanzibar, mamlaka ya Muungano na Tanganyika, ambayo hata hivyo, kama tulivyoona yalikuwa yamewekwa kwa muda tu chini ya mikono ya mtendaji mkuu wa Jamhuri ya Muungano (Rais).

Kwa hiyo sio sahihi kwa watu kudhani kuwa kwa vile mamlaka ya Tanganyika yaliwekwa kwa muda katika mikono ya mtendaji mkuu wa serikali ya Muungano, basi sheria zenye kujitegemea na tofauti za Tanganyika ziliacha kufanya kazi.

Kisheria serikali ya muungano ilipaswa kufanya kazi zake juu ya Tanganyika kwa njia ya kutumia sheria za Tanganyika tu na mambo yasiyo ya muungano.

Mwisho, Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar ulikuwa ni wa hiyari. Mwalimu Nyerere alinukuliwa na gazeti la Observer la Uingereza (20 Aprili 1968): “Muungano utasita kuwepo pale tu nchi shiriki zitapoamua kujitoa.”

Katika mahojiano mengine, Mwalimu Nyerere alisema kuwa hatawapiga mabomu Zanzibar iwapo wataamua kujiondoa kwenye Muungano.

Leo hii Muungano umeendelea kuwepo kwa sababu nchi washiriki wa Muungano hawajaamua kujitoa licha ya ukweli kwamba Muungano unaendelea kuendeshwa kinyume na makubaliano ya Mkataba wa Muungano (1964), hasa mfumo wa serikali mbili badala ya serikali tatu, kila moja ikiwa na eneo la mamlaka, yani Tanganyika na Zanzibar zikisimamia maeneo yao na ya muungano ikiwa ni ya tatu ikisimamia mambo ya muungano.

Ni upotoshaji mkubwa watu kudai kuwa kilichokubaliwa ilikuwa ni Muungano wa serikali mbili, na kwamba kinachosababisha mgogoro wa muungano ni hoja ya serikali tatu. Cha ajabu zaidi ni kwamba Muungano wa (Tanganyika na Zanzibar) ulizaa watoto wawili – Tanzania bara na Tanzania Visiwani, kabla ya Tanzania Visiwani kupigania haki yake ya asili, na hatimaye kurudishiwa jina lake la Zanzibar.

Hata hivyo, washiriki halali wa Muungano wataendelea kuwa Tanganyika na Zanzibar na wanaungwa mkono na ibara ya 5 ya Mkataba wa Muungano inayosema: “Sheria za Tanganyika na Zanzibar, zitaendelea kufanya kazi katika maeneo yahusikanayo.”

Vile vile mgogoro wa Muungano utaendelea kuhusisha zaidi changamoto za CCM kutekeleza sera yake ya Muungano wa serikali mbili kuliko changamoto za utekelezaji wa Makubaliano ya Mkataba wa Muungano (1964).

Related Posts