Serikali yajitosa kupoza makali Kupaa gharama za usafirishaji mizigo

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiahidi kulitafutia ufumbuzi ongezeko la gharama za usafirishaji wa mizigo kutoka nchi za Ulaya na Asia kwa njia ya meli, baadhi ya kampuni za usafirishaji zimesema bado hazijapata mwafaka.

Ongezeko hilo la gharama za usafirishaji limetajwa kusababishwa na hali ya usalama katika eneo la Suez Canal, ambako kunatajwa kuwa na uharamia, hivyo meli kutoka Asia zimekuwa zikichukua safari ndefu kupitia Afrika Kusini na hivyo kuongeza gharama za usafirishaji.

Pia kuna uhaba wa meli, kwani meli nyingi sasa zinapeleka mizigo Ulaya, badala ya kwenda Afrika, huku pia kukiwa na uhaba wa makontena ya kubebea mizigo.

Kutokana na ongezeko hilo, Watanzania wanatarajiwa kupata maumivu ya kuongezeka kwa bei za bidhaa, zikiwamo za mavazi kama nguo za aina tofauti, mabegi, pochi na viatu.

Pia kuna vipuri vya magari kama matairi, vifaa vya ujenzi vikiwemo vigae, makufuli, vitasa na aluminiamu na bidhaa za kiofisi, yakiwamo makaratasi.

Kutokana na hofu hiyo, jana Jumanne, Mei 21, 2024 akizungumza na kituo cha habari cha Clouds TV jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Profesa Godius Kahyarara, alisema wamekubaliana na wadau wa usafirishaji na taasisi za Serikali kuhusu mambo ya kufanya kwa muda mfupi ili kutafuta suluhu.

“Mojawapo ni kuhakikisha kwamba tunatumia fursa tulizonazo, kwa mfano kampuni zinazoweza kusaidia meli zitakazounganisha ile mizigo na kuja upande wa Tanzania.

“Niwatoe wasiwasi Watanzania, kwamba ni kweli bei zimeongezeka, lakini tutahakikisha kwamba haziathiri bei za mlaji. Tulikuwa na wenzetu wa TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania), tutaangalia namna kodi zinazokadiriwa zisije zikafuata bei inayoongezeka kwa haraka,” alisema.

Alisema pia wameweka mkakati wa kuongeza kasi ya kuondoa mizigo bandarini, ili kupunguza gharama za uendeshaji.

“Tatu ni kuhakikisha tunaongeza miundombinu ya kupakua mizigo bandarini kwenda huko inakokwenda. Walikuwepo wawekezaji waliotuonyesha vifaa vingi vinavyofungwa hivi sasa bandarini, ambapo ndani ya wiki ijayo baadhi vitaanza kutumika ambavyo vina uwezo mkubwa wa kupakua mizigo kwenye meli,” alisema.

 

Wakati Serikali ikisema hayo, Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo (JWK), Martin Mbwana alisema bado suluhisho halijapatikana, licha ya vikao walivyofanya na Serikali.

“Bado hawajatoa mwarobaini wa tatizo, kwa sababu kilichosababisha kupanda kwa bei ya kasha moja, ni gharama na uhaba wa makontena na uhaba wa meli.

“Kwa hiyo pamoja na kwamba TRA wanaangalia ile bei isiwe kubwa, lakini lazima tujue kwamba mizigo imekwama China na meli zimekuwa chache,” alisema.

Alisema walitarajia kuwa wangepata ufumbuzi wa kudumu kama wangeunganisha nguvu na Kenya kubeba mizigo kwa pamoja.

“Ikiwa Serikali ya Kenya ikiweka nguvu kwenye kupakia, biashara itahamia kwao. Kampuni za meli kama Maersk, TIL, Costal ni kampuni binafsi, hivyo tuangalie tutaunganishaje meli kubeba mizigo ya Afrika Mashariki.

“Meli kubwa inatoka kule inakuja kushusha Singapore, ingawa kwa meli ndogondogo zinaweza kushusha Durban, Mombasa, Dar es Salaam na kwingineko. Kwa hiyo tutafute meli yetu tubebe mizigo yetu, hapo itakuwa angalau tumepata suluhisho la muda fulani,” alisema.

Kwa upande mwingine kampuni ya Mo Cargo iliyotangaza ongezeko la bei wiki iliyopita kwa wateja wake wanaosafirisha mizigo kutoka China na Dubai kuja Dar es Salaam, imesema mambo bado hayajaeleweka.

Mwakilishi wa kampuni hiyo, Mayasa Mpangala, alisema chanzo cha ongezeko la bei ni kuongezeka kwa gharama za usafirishaji (freight), hasa kwa nchi za Asia na Ulaya, ambako gharama zimeongezeka karibu asilimia 50.

Alipoulizwa kuhusu hatua hiyo ya Serikali, Mayasa alisema bado hawajapata maelekezo yoyote ya Serikali kuhusu hatua zinazoendelea kuchukuliwa.

“Mpaka sasa (jana jioni) hakuna maelekezo yoyote kuhusu suala la bei, kwa sababu tunachokilipa ni muda ambao makontena yametoka nje kuja huku na ndio muda ambao freight (gharama za usafirishaji) zinatakiwa zilipwe. Mpaka sasa hakuna mwafaka wowote, wala mabadiliko yoyote,” alisema.

Kuhusu kodi, alisema haiwezi kupungua ghafla, akisema hata kampuni za usafirishaji bado hazijapata bei kamili za kutoza wateja wao.

“Tunajaribu tu kuwapa bei ambazo tunakokotoa kuangalia mteja anahusika vipi na kampuni inanufaika vipi kwa makisio yaliyopo, ambayo ni kati ya dola za Marekani 8,000 (Sh20.7 milioni) hadi 10,000 (Sh25.9 milioni) kutoka dola 2,500 (Sh6.4 milioni).

Kampuni nyingine iliyotangaza ongezeko ni Silent Ocean, ikisema bei za usafirishaji mizigo zimebadilika kidogo kuanzia Mei 18, 2024 ili kukabiliana na changamoto hiyo.
Mwakilishi wa kampuni hiyo, Witness Rogasian, alisema bado wanasubiri uongozi wa kampuni hiyo utoe mwelekeo wa bei.

“Bado tunasubiria viongozi wetu watupe gharama ambayo itakuwa nafuu kwa wateja na kwetu sisi. Tukisafirisha mizigo ni lazima tuwe na gharama kamili, ndiyo maana tunawaomba wateja wetu waendelee kusubiri, tukipata gharama kamili itakuwa rahisi kutambua gharama itakayokuwa rafiki,” alisema na kuongeza:

“Tunasafirisha mizigo kama kawaida, kwa mteja ambaye ana haraka huwa tunamwambia awasiliane na kule mzigo unakotoka moja kwa moja,” alisema.
 

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa, alisema msongamano wa meli katika bandari ya Dar es Salaam, hausababishi moja kwa moja gharama hizo, kwani umekuwepo kwa muda mrefu.

“Kitu cha kujua ni kwamba nchi yetu kumekuwa na ongezeko kubwa la biashara ya bandari, kwa sababu kuna shughuli nyingi za kiuchumi zinafanyika na vilevile nchi zinazotuzunguka zimeongeza uzalishaji wa malighafi kama madini na ujue pia tumekuwa na gati zilezile 12 kwa miaka yote,” alisema.

Alisema wako katika hatua za kuhakikisha wanaongeza idadi ya gati kwa Dar es Salaam na ujenzi wa bandari ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.

“Tumeshatangaza zabuni na pia tuko kwenye hatua za juu kabisa za kuongea na wawekezaji, kuna kampuni zimeonyesha nia ya kujenga. Bandari ya Dar es Salaam, tunatarajia kujenga gati 10, tukianza na mbili, baadaye mbili, baadaye sita kulingana na majadiliano tuliyonayo,” alisema.

Pia alisema kuna kazi za operesheni, akiitaja kampuni ya DP World kuwa miongoni mwa mikakati ya kuharakisha upakuaji wa mizigo.

“Kwa hiyo pale ameongeza vifaa, muda si mrefu tunategemea tutawasha mashine zile mbili za kisasa za kushusha makontena ambapo tutapunguza sana muda wa meli kusubiri.”

Mkakati mwingine amesema: “Tumeongea na baadhi ya kampuni za meli ambazo tumesema kama wataleta mzigo kwa bei rahisi watakuwa hawajipangi kwenye foleni kusubiri, zitakuwa zinaingia moja kwa moja, zinashusha mzigo na kuondoka.”

Juhudi za kuwapata viongozi wa TRA hazikufanikiwa baada ya simu ya Kamishna Mkuu, Alphayo Kidata kuita bila kupokelewa

Related Posts