Serikali yaombwa kuhamasisha teknolojia ya kidigiti

Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital

Serikali imeombwa kushirikiana na taasisi zisizo za kiserikali kuhamasisha elimu ya teknolojia ya kidigiti kuanzia ngazi ya chini.

Ombi hilo limetolewa na baadhi ya wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wakati wa Kongamano la Wiki ya Ubunifu liloandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalojishughulikia Masuala ya Wanawake (UN Women), jijini Dar es Salaam.

Wahitimu hao wamesema endapo elimu ya kidigiti itaanzia ngazi ya shule ya msingi itawezesha nchi kukua kiteknolojia.

Annagrace Malamsha ni mmoja wa wahitimu hao ambaye ni wanufaika wa Program ya ujuzi wa kidigiti ya UN Women, amesema ni vyema Serikali ikaanzisha Mtaala wa Elimu ya Teknolojia ya kidijiti kuanzia shule za msingi ili kuwezesha nchi kuwa na maendeleo ya kiuchumi.

“Kupitia Program ya ujuzi wa Kidigiti inayoendeshwa na UN Women imetupa hali ya kujiamini, nigependa Serikali kuanzisha mtaala wa mafunzo ya teknolojia ya kidigiti kwa ngazi ya elimu ya msingi ili tuweze kukua kiteknolojia,” amesema Annagrace.

Amesema kupitia elimu hiyo ya kidigiti ameweza kujiajiri, hivyo ni vyema Serikali na wadau kuwekeza nguvu kubwa katika ukuzaji wa teknolojia.

” Tunajifunza nchi za wenzetu wamekuwa wakihamasisha elimu ya teknolojia kwa ngazi ya chini ya elimu,” amesema.

Naye Mhitimu na mtaalamu wa takwimu kwa njia ya teknolojia ya kidijiti, Suna Salum amesema nchi iweze kukua kimaendeleo inahitaji wataalamu mbalimbali wenye ujuzi wa teknolojia ya kidigiti ili kuvumbua vitu mbalimbali.

Kwa Upande wake Mchambuzi wa Sera na Programu wa UN Women, Michael Jerry, amesema Shirika hilo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameweza kuendesha mafunzo ya watoto 110 katika tasnia ya teknolojia ya kidigiti .

Ameeleza kuwa bado kuna umasishaji mdogo wa ujuzi wa teknolojia ya kidigiti hasa kwa watoto.

Related Posts