Arusha. Kampuni zinazoendesha migodi ya madini hapa nchini zimefanya ununuzi wa zaidi ya Sh3.1 trilioni mwaka uliopita baada ya kuagiza nje ya nchi bidhaa mbalimbali.
Kutokana na ununuzi huo, Waziri wa Madini, Antony Mavunde ameagiza Tume ya Madini nchini kumpelekea orodha ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.
Mavunde ametoa maagizo hayo leo Jumatano Mei 22, 2024, wakati akizungumza kwenye jukwaa la tatu la utelekezaji wa ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya madini lililoanza leo jijini hapa.
Amesema katika mwaka wa fedha ulioisha, zaidi ya Sh3.1 trilioni zimetumika kwa ajili ya manunuzi ya bidhaa mbalimbali katika migodi yote nchini na kuwa endapo fedha hizo zingebaki hapa nchini zingesaidia kubadilisha uchumi.
Mavunde ameielekeza Tume hiyo kumpelekea orodha ya bidhaa ambazo zinaagizwa nje ya nchi ili Serikali iwatafute wazalishaji hao waje kuwekeza hapa nchini ili Watanzania wanufaike na fursa hizo kwani ndiyo njia pekee ya kukuza uchumi wa Tanzania.
“Ndiyo maana eneo kubwa tunalosimamia kwa dhati ni hili la ushirikishwaji wa Watanzania ili wanufaike na sekta hii ya madini, nitoe rai kwa ndugu zangu, tuchangamkie fursa hii ya kipekee na sisi kama Serikali tuko tayari kuona hizo Sh3.1 trilioni zinabaki hapa nchini ili Watanzania wanufaike,” amesema.
Waziri Mavunde amesema Serikali iliamua kutenga eneo la Buzwagi mkoani Shinyanga: “Buzwagi Special Economic Zone” lenye ukubwa wa ekari 1,331 ambapo kutajengwa viwanda vya kuongeza thamani na kuwezesha shughuli za uchimbaji madini.
Amesema eneo hilo kwa sasa linasubiri wawekezaji kwa ajili ya kwenda kuanzisha viwanda mbalimbali na kuwa hadi sasa kuna viwanda vikubwa vinane kutoka nchi mbalimbali ambavyo vimeonyesha nia ya kwenda kufanya uwekezaji na kuwa itasaidia kuifanya Tanzania iwe kitovu cha utoaji wa huduma za sekta ya madini Afrika Mashariki na Kati.
“Tunataka watu wote wapate bidhaa kutokea Tanzania na jambo hili ndugu zangu Watanzania linawezekana, tunayo kampuni ya Rock Solution ambayo wanatengeneza vifaa vinavyotumika kutunza sampuli za miamba na wako asilimia 90 kukamilisha mradi huu. Muda siyo mrefu tutaanza kuona bidhaa nyingi zinazalishwa nchini Tanzania,” ameongeza.
Kuhusu tafiti, amesema Serikali imejipanga hadi kufikia mwaka 2030 itakuwa imefikia asilimia 50 ya kufanya tafiti za kina kwenye sekta ya madini ambapo kwa sasa ni asilimia 16 pekee ya Tanzania imefanyiwa utafiti.
“Kama eneo la nchi yetu lililofanyiwa utafiti kwenye madini ni asilimia 16 tu lakini nchi yetu imeendelea kupata manufaa makubwa. Kwa hali tuliyonayo leo, tuna uwezo wa kujua madini yako wapi, lakini hatujui kwa kiwango gani. Ukijua ni kwa kiwango gani ni rahisi kupanga mipango yetu,” amefafanua.
Waziri huyo amesema kutokana na mazingira wezeshi kwenye sekta hiyo ikiwemo mabadiliko ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010 yaliyofanywa mwaka 2017, yamewezesha kutoa fursa kwa wawekezaji wengi.
Katika sekta ya madini, hadi kufikia mwaka 2023, ajira 18,853 ambazo ni sawa na ongezeko la ajira 2,391 sawa na asilimia 14.5.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo amesema ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya madini umelenga kuhakikisha kipaumbele kinatolewa kwa huduma na bidhaa zinazozalishwa nchini na zinazotolewa na Watanzania katika sekta hiyo.
Amesema majukumu mengine ni kusimamia na kuidhinisha utolewaji mikataba ya manunuzi ya bidhaa na huduma kwa wamiliki wa leseni za madini na watoa huduma katika sekta hiyo, kufanya ukaguzi na kusimamia na kuidhinisha utolewaji wa mikataba ya manunuzi ya bidhaa na huduma kwa wamiliki wa leseni za madini na watoa huduma katika sekta hiyo.