Malinyi. Serikali imetoa Sh800 milioni kwa ajili ya kujenga Daraja la Mto Furua ili kuondoa changamoto ya usafiri na usafirishaji inayowakabili wananchi.
Daraja hilo ni miongoni mwa yaliyoharibiwa na maji ya mafuriko Machi mwaka huu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa ameyasema hayo Jumatano Mei 22, 2024 akiwa wilayani humo akiendelea na ziara yake ya kikazi.
Mchengerwa pia atazitembelea wilaya za Kilombero, Ulanga na Halmashauri ya Mlimba lengo likiwa ni kuona kiwango cha uharibifu wa miundombinu na pia kuzungumza na wananchi kuhusu mipango ya Serikali ya kurejesha miundombinu hiyo katika hali yake ya kawaida.
Waziri Mchengerwa pia amekagua miundombinu ya barabara za Mji wa Malinyi na kujiridhisha kuwa imeharibiwa vibaya na mafuriko na hivyo kusababisha wananchi kupata adha ya usafiri na usafirishaji.
Kufuatia hali hiyo, Mchengerwa amemwagiza Meneja wa Wakala ya Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) Mkoa wa Morogoro, Emmanuel Ndyamukama kutafuta mkandarasi wa kujenga daraja la mto huo, ambalo ndio chanzo kikubwa cha mafuriko yanayotokea mara kwa mara Malinyi.
Amemtaka meneja huyo pia kuhakikisha ndani ya wiki mbili awe amempata mkandarasi ili ujenzi wa daraja hilo uanze.
“Nimeshawaelekeza watendaji wa wizara, mkurugenzi wa ujenzi Tamisemi anayeisimamia Tarura na meneja wa Tarura ambao nao wameniambia wanahitaji Sh800 milioni kukamilisha ujenzi huo na nimewapa wiki mbili nataka barabara hii ipitike,” amesema Mchengerwa.
Pamoja na hilo, Mchengerwa amewataka viongozi wa ngazi zote kushirikiana na kuwa wabunifu ili kuwatumikia wananchi kikamilifu.
Katika hatua nyingine, Waziri Mchengerwa ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha za dharura kukarabati miundombinu mbalimbali ikiwemo ya barabara iliyoathiriwa na mafuriko nchini.
Akizungumza baada ya kusoma taarifa ya Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amewaagiza watendaji wa Serikali kuhakikisha fedha hizo zinafanya kazi iliyokusudiwa.
“Nawaomba asiwepo kiongozi ama mtu yeyote atakayejaribu kufuja fedha za mradi huu, tunataka zitumike kama ilivyokusudiwa ili daraja litakalojengwa lilingane na fedha zilizotolewa,” amesema Malima.