Moshi. Wakati baadhi ya watu wakiitazama biashara ya ndizi mbivu mitaani kama ya kimasikini, ukweli ni kwamba biashara hiyo imekuwa mkombozi kwa wanawake wengi katika Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Biashara hiyo imewapa mafanikio kama vile kujenga nyumba, kusomesha watoto, kusaidia familia zao mahitaji muhimu ya kila siku huku wakijisikia furaha kuifanya kama ajira inayoendesha maisha yao.
Mwananchi limezungumza na wanawake hawa walio katika rika tofauti ambapo wamesimulia kilicho nyuma ya pazia ya biashara hiyo, wakiangazia fursa na changamoto zilizopo.
Jambo la kufurahisha ni kwamba wanawake hawa ni watu wanaojipenda, kila wanaporudi nyumbani baada ya biashara yao, wanapita mahali kunywa bia mbili au tatu kama kujipongeza, kisha hurejea nyumbani kujipanga kwa siku inayofuata.
Kwa kawaida wanatoka majumbani mapema asubuhi na kutembea kwa miguu wakiwa makundi makundi, wamejiwekea vituo kama vitatu vya kupumzikia kabla ya kufika mjini Moshi, huku wakiuza ndizi zao kila wanakopita na mzigo hupungua kadiri wanavyotembea.
Kikongwe ndani ya biashara
Yasinta Mwacha, mkazi wa Kibosho Kirima mwenye umri wa miaka 78, ni miongoni mwa akina mama hao wanaofanya biashara ya ndizi na pembezoni mwa Barabara mjini Moshi.
Mwacha amesimulia kuwa alianza biashara hiyo akiwa na umri wa miaka 28, wakati huo akiwa na watoto wawili na aliamua kujiingiza kwenye biashara hiyo ili kupata fedha za kujikimu na kuihudumia familia yake.
Amesema kwa biashara hiyo, anaweza kupata faida ya Sh5,000 hadi Sh15,000 kwa siku, kulingana na mzigo alionao, na hivyo kujiimarisha kiuchumi na kuihudumia familia yake, ikiwamo kusomesha watoto.
Amesimulia kuwa amefanya biashara hiyo kwa umakini mkubwa na kujiwekea akiba kwenye vikundi vya kuweka na kukopa, hatua ambayo ilimwezesha kupata fedha za kusomesha watoto hadi vyuo vikuu na mahitaji mengine ya nyumbani.
Mbali na kusomesha watoto, amesema amejenga nyumba nzuri ya kuishi na pia anafuga ng’ombe wa maziwa, mbuzi na hata kuku na hadi sasa anaweza kujitegemea bila kusumbua watoto wake.
“Hii kazi si ya kudharau, ukiifanya kwa umakini ina hela, mimi nimeianza nikiwa na watoto wawili na umri wa miaka 28. Sasa nina watoto wanne, nimewasomesha hadi vyuo vikuu, yupo mwalimu, daktari na mwingine anafanya kazi bandarini,” amesema mwanamke huyo.
Amesema kipindi anaanza biashara hiyo, alikuwa anaweza kubeba kibox cha mbao kilichojaa ndizi, lakini kwa sasa anabeba vichane vichache na anapata fedha kwa ajili ya mahitaji madogo ya nyumbani.
Bibi huyo ameeleza kuwa licha ya watoto wake kuwa na kazi, hawezi kukaa nyumbani kuwasumbua wamhudumie kwa kila kitu kwa kuwa anahitaji nao wahudumie familia zao na waweze kujitegemea kimaisha.
“Watoto wamekuwa wakiniambia niachane na kazi hii nikae nyumbani lakini siwezi kuacha, wao waendelee na maisha yao, walee watoto wao ili nao wasimame,” amesema bibi huyo kwenye mahojiano na Mwananchi.
“Wakinipa kidogo naridhika lakini siyo kwamba nikae tu niwategemee kuwa leo sina hiki wala kile, mtu umeshazoea kushika hela yako, leo kukaa kutegemea kupewa ni vigumu sana na nitajisikia vibaya.”
Akifafanua mazingira ya kubeba jukumu la kuhudumia familia, Mwacha amesema mumewe alikuwa na shughuli zake nje ya mkoa wa Kilimanjaro na hivyo alijikuta mzigo wa kulea familia kwa asilimia kubwa anaubeba mwenyewe.
“Unajua mambo ya wanaume, leo yuko huku, mara kule, nimepambana sana na watoto maana huwezi kuishi kwa kutegemea mfuko wa mtu mwingine aliyeko mbali,” anasema Mwacha akisisitiza kuwa ana uhusiano mzuri na mumewe.
“Mume anakutumia Sh20, 000 anaona ni nyingi sana na utakula mwezi mzima, kumbe hata ukiamua kununulia vitu vya nyumbani siku moja haitoshi,”amesema mama huyo.
Changamoto zinazowakabili
Mwanamke mwingine anayefanya biashara hiyo, Genoviva Chuwa (65), mkazi wa Boro Kibosho, amesema kupitia biashara ya ndizi mbivu, pia anahudumia familia kwa mahitaji ya nyumbani na kuwasomesha watoto na wajukuu.
Hata hivyo, amesema moja ya changamoto wanazokumbana nazo ni kutembea umbali mrefu kutafuta wateja, ameiomba Serikali kujenga masoko ya karibu ya ndizi mbivu ili kuwapunguzia umbali wa kutembea.
Kwa upande wake, Paskalina John, mkazi wa kijiji hicho, amesema ameanza biashara hiyo tangu akiwa mtoto na hadi sasa amekuwa mama anaendelea nayo ili kujipatia fedha kwa ajili ya kuhudumia familia yake.
“Umbali mrefu ni kero kwani tunatembea kwa miguu na wakati wa mvua, changamoto ni kubwa zaidi kwa sababu barabara ni mbovu, tunaomba Serikali itusaidie kupata mikopo isiyo na riba ili kuongeza mitaji yetu,” amesema.
Ili kuondokana na adha ya kuzunguka kuwatafuta wateja, Halmashauri ya Wilaya ya Moshi imeanza kujenga kituo cha kukusanya na kuuza ndizi eneo la Kibosho Kirima, ili wakulima wapeleke ndizi zao pale ambako wafanyabiashara watazifuata.
Msichana kutoka Kirima, Agness Chami (23) ambaye amefanya biashara hiyo kwa miaka miwili sasa, ameeleza kwamba inamsaidia kuhudumia familia yake ya watoto wawili kwa mahitaji mbalimbali.
“Kwa siku nauza kuanzia vichane 14 vya ndizi na kuendelea na napata faida ya Sh8,000 hadi Sh15,000. Naendelea kujiwekeza akiba kwani mpango wangu ni kupata mtaji nifungue kibanda cha kuuzia matunda mbalimbali na juisi,” amesema.
Ameongeza kuwa: “Nimejiunga kwenye vikundi vya Vicoba na kupitia biashara hii natamani kujiwekeza ili nijenge nyumba yangu na kuondoka kwenye nyumba za kupanga.”
“Wito wangu kwa vijana wenzangu, wasione tunaofanya biashara hii tunapitia taabu sana, hapana, tumeamua kujituma ili kumudu maisha yetu na kuondoka kwenye utegemezi,” ameeleza binti huyo.
Kwa upande wake, Neema Urota ambaye amefanya biashara ya ndizi kwa miaka sita sasa, anasema mbali na kupata fedha kwa ajili ya kuhudumia familia yake, amefungua duka la vinywaji mbalimbali.
“Mimi binafsi nimezaliwa nikakuta mama yangu akifanya biashara hii na ametusomesha kwa biashara hii, na mimi nimesoma ualimu wa chekechea, lakini baada ya kukosa kazi nimeamua kufanya biashara hii,” amesema.
“Mimi nina watoto wawili na ninalea watoto wangu mwenyewe na kuwasomesha na kwa biashara hii ninamudu mahitaji yao bila kumtegemea mtu,” amebainisha.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Moshi, Shadrack Mhagama amesema wameanza kujenga kituo cha kukusanya na kuuza ndizi eneo la Kibosho Kirima ambacho kitasaidia wakulima kupeleka ndizi eneo moja.
“Tayari tunajenga kituo cha kukusanya na kuuza ndizi zote kwa maana ya mbichi na matunda, hii itasaidia wafanyabiashara kufuata ndizi mahali pamoja badala ya kwenda kununua mashambani kwa wakulima,” amesema.
Amesema kwa wafanyabiashara wa ndizi mbivu ambao wanatembea kwa miguu hadi mjini Moshi kuuza, wanaangalia namna ya kuwakutanisha kwenye vikundi ili kupata mikopo ambayo itaongeza mitaji yao na kuboresha biashara zao.
“Hao kina mama ambao wameonyesha nia ya biashara na kuuza ndizi mbivu, tutawapa elimu na kuwahamasisha wajiunge kwenye vikundi ili kupata mikopo ya halmashauri isiyo na riba na kuongeza mitaji yao.
“Tunaamini mitaji yao ikiwa mikubwa, wataweza kukodi gari kama kikundi kwa bei nafuu na kusafirisha ndizi hadi mjini na hii itawapunguzia umbali ambao hutembea kila siku na mzigo kichwani,” amesema.
Mwenyekiti wa zamani wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Patrick Boisafi amesema akina mama mkoani humo wamekuwa wakichangamkia fursa mbalimbali za biashara, hali iliyowafanya wajiimarishe kiuchumi.
Boisafi amesema wanapaswa kupongezwa, kwa kuwa wameonyesha namna ya kujituma kuchangamkia fursa za kibiashara na kujikwamua kiuchumi.
Katika Mkoa wa Kilimanjaro ndizi zinalimwa kwenye eneo la ukubwa wa hekta 61,892 na kuzalisha jumla ya tani 517,997 za ndizi za aina mbalimbali kwa mwaka.
Mbali na ndizi zinazotumika kwa chakula, pia zipo ndizi zinazotumika kutengeneza pombe ya kienyeji (mbege) na ndizi mbivu aina ya malindi ambazo zinatumika kama matunda.