Tendo la ndoa, marafiki, furaha inavyolinda afya yako bila dawa

Dar es Salaam. Kama unadhani msingi wa uponyaji wa maradhi yoyote yanayokusibu ni kununua dawa katika duka la dawa au hospitali unakosea, wakati mwingine huhitaji kuingia gharama yoyote, ipo tiba uliyoibeba mwilini mwako.

Hivi unajua kuwa kwa kadiri unavyocheka, ndivyo unavyoiweka salama afya ya mwili wako dhidi ya athari za magonjwa?
Kwa taarifa yako, ule usemi wa ‘cheka uongeze siku za kuishi’ unaakisi uhalisia, ipo siri ya maisha marefu ndani ya cheko, kama ilivyoelezwa katika Jarida la Daily Mail la nchini Uingereza.

Kwa mujibu wa jarida hilo, kucheka ni moja ya dawa 20 zilizotajwa na jarida hilo kuwa na uwezo wa kukuponya bila kulazimika kumeza vidonge kutoka duka la dawa.

Kabla hujaathiriwa na usugu wa dawa dhidi ya vimelea kwa kunywa tembe lukuki za vidonge, cheka utapona, kwa mujibu wa Daily Mail.

Kucheka ni jambo moja, lakini kufanya mazoezi ni jambo lingine ambalo kwa mujibu wa Daily Mail, linaimarisha afya ya mwili na akili.

Kadhalika, mazoezi ni dawa kwa magonjwa yasiyoambukiza kama ilivyowahi kuelezwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, Januari mwaka huu alipokuwa katika moja ya maduka ya vifaa vya michezo jijini Dar es Salaam.

“Kumekuwa na ongezeko la kasi la magonjwa yasiyoambukiza, ikiwemo kisukari na shinikizo la juu la damu (presha) Watanzania tunatakiwa kuzingatia mtindo wetu wa maisha, kwa kupunguza mafuta na chumvi katika vyakula pamoja na ufanyaji wa mazoezi,” alisema Waziri Ummy.

Jarida hilo limekwenda mbali zaidi na kutaja hatua ya kuwapenda wengine ni dawa muhimu katika maisha ya kila mwanadamu.
Chuki na uadui ni chanzo kikubwa cha tatizo la afya ya akili na hata kufikia hatua ya kudhoofisha mwili, kwa sababu kutopenda wengine husababisha kusononeka, kunakochangia kuharibu kwa kiasi kikubwa afya ya akili na mwili. Upendo ni dawa muhimu kwa kila mtu, hivyo ni vyema kupenda wengine na kufurahia mafanikio yao, ili kupunguza mzigo wa chuki moyoni.

Chakula cha asili ni dawa

Si ushamba wala umasikini, kula vyakula vya asili kama mihogo, viazi, magimbi, mahindi, korosho na vyinginevyo, ni suluhisho la magonjwa yasiyoambukiza kama vile figo, kisukari, moyo, shinikizo la damu na udumavu.

Kama hiyo haitoshi, Daily Mail linataja kufunga ni dawa pia.  Ingawa wengi wanatekeleza hilo kama takwa la kiimani. Hili  limewahi pia kuelezwa na mbobezi wa magonjwa ya moyo nchini, Profesa Mohammed Janabi.

Kwa mujibu wa Profesa Janabi, kufunga kula chakula mara moja au mbili huwa na faida ya kuongeza kinga za mwili na maisha.

Wapo baadhi ya watu ambao kulala kwao ni dharura. Kwa taarifa yako, kufanya hivyo kunahatarisha afya yako.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, mtu anatakiwa kufunga kwa saa nane.

Picha na Mtandao

lakini pia kuna tiba ya kulala. Kati ya faida zake zinazotajwa  na wataalamu ni kutuliza ubongo. Hali hiyo husaidia kuufanya utunze kumbukumbu na hupata muda wa kufanyia kazi taarifa ulizo nazo.
Pia, kulala husaidia mwili kupumzika na kujijenga upya.

Yapo maneno na majina mengi ya utani ambayo watu huwapatia wanaopenda kukaa juani, lakini kiuhalisia kufanya hivyo kunaongeza vitamin D.

Imeelezwa kuwa tunahitaji vitamini D, kwa ajili ya miili kufyonza madini ya calcium na fosphati kutoka kwenye chakula, madini yote hayo ni muhimu kwa afya ya mifupa, meno na misuli bila kujali umri wa mtu.

Kusoma na kujifunza neno la Mungu ni dawa. Kwa imani mbalimbali watu hufarijika na kujikuta wakiendelea kusonga mbele kutokana na maneno matakatifu ambayo wanayasoma kwenye vitabu vya dini.

Maneno hayo hugeuka dawa kwa afya zao za akili na kufanya wawaze yaliyo mema, hivyo basi faraja na tumaini ambalo hupatikana kutokana na imani ni ngao na dawa kubwa ya afya ya akili na mwili.

Maji ni dawa ambayo husaidia kuponya magojwa mengi, kwani bila maji ni rahisi kupata matatizo ya ngozi, matatizo kwenye mfumo wa umeng’enyaji na mengineyo.

Mbali na matatizo hayo, wataalamu mbalimbali wamekuwa wakieleza faida za kunywa maji ambazo hugeuka na kuwa tiba kwenye mwili wa binadamu kwa kusaidia kuponya magonjwa katika mfumo wa mkojo na kurudisha kumbukumbu.

Aidha, mtaalamu wa masuala ya lishe kutoka Taasisi ya Chakule na Lishe (TFNC), Julieth Shime, amewahi kusema viungo vingi vya mwili ili viweze kufanya kazi vizuri vinahitaji maji na zaidi ya asilimia 60 ya uzito wa mwanadamu ni maji.

Kujisamehe na kusamehe wengine ni dawa. Kila kukicha yanaibuka matukio ya kikatili ya mtu binafsi kujitoa uhai au kudhuru au kuua wengine, hayo yote hutokana na kushindwa kujisamehe na kusamehe wengine, jambo linalosababisha kujenga chuki na kukuza sumu akilini na hapo ndipo yanapoibuka matukio ya kikatili kwenye jamii.

Hivyo dawa kubwa kuepukana na changamoto za afya ya akili ni kuhakikisha mtu binafsi unajisamehe na kisha kuwasamehe wengine waliokukosea.

Marafiki wazuri ni dawa, uliowapa nafasi kuwa karibu kama marafiki ni dawa nzuri kwenye maisha yako, lakini pia ni sumu kali inayoweza kukuangamiza mara moja, uchaguzi wa marafiki kwa makini ni jambo la muhimu ili uwapo nao karibu wawe dawa na siyo sumu.

Picha na Mtandao

Si hayo tu, dawa nyingine zilizotajwa na mtandao huo ambazo hazipatikani dukani na muhimu kwa afya yako ni kujipenda, kutoa shukrani, kuacha kurudia kosa, kutafakari, fikra sahihi, pia kula mboga na matunda.

Mtaalamu wa Afya ya Jamii na aliyekuwa Mkurugenzi wa Kinga, Wizara ya Afya kabla hajastaafu mwaka 2005, Dk Ali Mzige anasema hakuna dawa kwa kila ugonjwa au maradhi.

“Kifanye chakula chako kiwe dawa yako, ifanye dawa yako iwe chakula chako. Waislamu wanafundishwa fungeni mwezi wa Ramadhan mtapata siha, yaani afya na Wakristo hufunga kipindi cha Kwaresma. Unapofunga seli za saratani zinakosa sukari ya kuzifanya ziwe hai,” anasema.

Anafafanua kuwa seli za saratani hazipendi hewa ya oksijeni, kwa mtu anayefanya mazoezi ya kukimbia hewa safi ya oksijeni inaua virusi na bakteria.

Dk Mzige anasema mtu anapofunga lehemu au cholesterol zina pungua, zile mbaya zinazotengenezwa na nyama tunazokula kupita kiasi na kwamba lehemu nzuri hutengeneza homoni na kuimarisha kinga.

“Unapotimiza tendo la ndoa kwa ufanisi, shinikizo la damu hupungua na mwili unapata kupumzika kimwili na kiakili. Unapofanya kitu kizuri moyo wako unakuwa na faraja. Ukinuna unakosa usingizi na utakula zaidi kupunguza msongo wa mawazo, kumbe ndio unazidisha,” anasema Dk Mzige.

Profesa wa sayansi ya neva na ile ya saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha California, Berkeley, Mathew Walker alichunguza takwimu kutoka kwa mamilioni ya watu ambao wamehusika katika utafiti wa tawi la sayansi iliyotafiti visa, usambazaji na udhibiti wa magonjwa na sababu nyingine zinazohusiana na afya.

“Iwapo una hamu ya kutaka kuishi maisha marefu basi utalazimika kuwekeza katika kujipatia usingizi mzuri,” alisema.
Utafiti ulibaini binadamu anapolala, ubongo wake hupata wakati wa kutunza kumbukumbu na kufanyia kazi taarifa ulizonazo ambayo ni matukio ya kutwa nzima au kipindi ambacho binadamu alikuwa ameamka.

“Ni muda ambao sumu au uchovu huondoka katika mwili na kuuruhusu kufanya kazi vizuri utakapoamka,” alisema Profesa Mathew na kuongeza kuwa iwapo hupati usingizi waone wataalamu wa afya.

Related Posts