Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema, kwa sasa hakuna tena tishio la kimbunga Ialy katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Taarifa ya TMA kwa ummya waliyoitoa saa 4:00 usiku wa jana Jumatano, Mei 22, 2024 ilisema wanahitimisha mfululizo wa taarifa za kilichokuwa Kimbunga Ialy zilizokuwa zikizitoa tangu Mei 17, 2024.
“Mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa unaonesha katika kipindi cha saa 6 zilizopita, Kimbunga Ialy kimepoteza kabisa nguvu yake, kikiwa kaskazini mashariki mwa pwani ya Kenya.
“Hivyo, kwa sasa hakuna tena tishio la kimbunga Ialy katika nchi yetu,” amesema.
Aidha, wakati kikipita karibu na pwani na nchi yetu kati ya juzi Jumanne Mei 21 na leo tarehe 22 Mei 2024 kimeweza kusababisha vipindi vya mvua, upepo mkali na mawimbi makubwa katika maeneo ya pwani ya nchi yetu kama ilivyotabiriwa awali.
“Hata hivyo, ikumbukwe japo tunaelekea mwishoni mwa msimu wa Masika, 2024, tunakaribia kuanza kwa msimu wa Kipupwe, na kwasababu hiyo, vipindi vya upepo wa Kusi baharini vinaweza kuanza kujitokeza na kuambatana na mawimbi makubwa kwa baadhi ya nyakati,” imeeleza taarifa hiyo.
TMA imewashauri wananchi na watumiaji wa bahari kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na maelekezo na miongozo inayotolewa na mamlaka husika.