Wananchi wataka kasi ukarabati barabara iliyoharibiwa na El Nino, Hidaya

Lindi.  Wananchi wilayani Kilwa Masoko wameitaka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Lindi kuongeza kasi ya ukarabati ili kurejesha mawasiliano katika Barabara ya Tingi hadi Kipatimo iliyoathiriwa na mvua za El Nino na kimbunga Hidaya.

Mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali ilisababisha baadhi ya madaraja katika barabara hiyo kusombwa na maji, hivyo kuathiri shughuli za kiuchumi na kijamii.

Magari yanayofanya safari kati ya Dar es Salaam hadi Kipatimo yalisitisha huduma, hivyo wananchi kulazimika kutumia fedha zaidi kusafiri wa pikipiki.

Pikipiki pia zimekuwa zinatumika kusafirishaji bidhaa, jambo limeongeza gharama za uendeshaji kwa wafanyabishara na kupaisha bei za bidhaa.

Meneja wa Tanroads Mkoa wa Lindi, Emil Zengo amesema wamelazimika kuweka kambi kwenye maeneo hayo kwa ajili ya ukarabati ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa.

Eneo la kwanza lililokarabatiwa kwa kujaza kifusi ni daraja lililosombwa na maji lililopo kilomita 12.5 kutoka Tingi ilipo barabara ya Dar es Salaam – Mtwara.

Amesema ujazaji kifusi utaruhusu ujenzi kuendelea katika maeneo mengine.

“Tumeanza kwa kufungua njia katika eneo ambalo lilikuwa limekatika ili mitambo iweze kufika kufanya kazi ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha changarawe,” amesema.

Mtumiaji wa barabara hiyo, Abdul Matembo ameitaka Tanroads kuongeza kasi ili barabara hiyo ipitike wa urahisi.

Amesema tangu ilipoharibika magari yamesitisha huduma na gharama za maisha zimeongezeka.

“Kwa gari kutoka Dar es Salaam hadi Kipatimo ni kati ya Sh18,000 hadi Sh20,000 lakini hivi sasa bila Sh70,000 haufiki kwa sababu magari yote yanaishia Tingi, bodaboda kutoka pale zinaanzia Sh40,000 ukionewa huruma na ukijieleza,” amesema Matembo.

Kwa upande wake, Francis Ngonyani amesema: “Huku tuna nazi nyingi, mwanzoni ukibeba kwenye gari unatozwa kila nazi kati ya Sh100 na Sh200 hadi unapofika Dar es Salaam, lakini hivi sasa kuzitoa huku hadi kufika sehemu unayoweza kupata basi la kwenda Dar es Salaam unamlipa bodaboda hadi Sh50,000,” amesema.

Kutokana na hilo, ameishauri Tanroads kuharakisha ujenzi ili maisha yao yarejee kama zamani.

Mwajuma Haji, anasema hali ilivyo imewafanya kuwa kama wakazi wa kisiwani kutokana na shida ya usafiri.

“Hiyo pikipiki yenyewe ukipanda unakuwa na hofu muda wote, Mungu asaidie wamalize kwa wakati,” amesema Mwajuma.

Mhandisi msimamizi wa barabara hiyo, Fredy Sanga amesema awali barabara hiyo iliathiriwa na mvua za El Nino lakini hali ilikuwa mbaya zaidi baada ya Kimbunga Hidaya.

Amesema mvua zilisababisha daraja lililopo Mingumbi kukatika na kusababisha barabara kutokupitika.

Mkandarasi Kasmir Mucadam, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mucadam and Sons Limited inayokarabati barabara hiyo, amesema mvua ilikuwa kikwazo katika utekelezaji wa majukumu.

“Tulisaini mkataba Machi mwaka huu lakini mvua ilikuwa changamoto, kwa sasa imetuachia tunapambana na kazi, madaraja mengi yalibebwa na maji, tunatakiwa kujaza kifusi katika eneo moja baada ya lingine hadi tufike Kipatimo,” amesema.

Related Posts