Wanaopisha Uwanja wa Ndege Musoma walalamika kucheleweshewa malipo ya fidia

Musoma. Wamiliki wa nyumba 49 zilizopo jirani na Uwanja wa Ndege katika Manispaa ya Musoma mkoani Mara, wameiomba Serikali kuharakisha malipo yao ya fidia yanayofikia Sh3.9 bilioni ili waweze kupisha ujenzi na upanuzi wa uwanja huo.

Wamiliki hao wamesema tayari nyumba zao zilishafanyiwa tathmini tangu mwaka jana lakini mpaka sasa hawajalipwa na hawajui nini kinaendelea.

Wakizungumza mjini hapa leo Alhamisi Mei 23, 2024, baada ya kuwafika katika ofisi za Wakala wa Barabara Nchini (Tanroads) Mkoa wa Mara walikokwenda kwa ajili ya kuonana na meneja, baadhi ya wakazi hao wamesema hawana pingamizi na mradi huo, kwa kuwa wanaamini una manufaa kwa wakazi wa Musoma na mkoa kwa ujumla.

“Ila tunachotaka sisi kujua ni lini tutalipwa fidia zetu. Wapangaji wameondoka wote, mazingira yetu ni mabaya, nyumba zimebomoka na hii yote ni kwa sababu hatuwezi kufanya ukarabati wa aina yoyote tumezuiliwa kufanya hivyo,” amesema Florence Jacob.

Amesema wanashindwa kufanya maendeleo ya maeneo yao tangu mwaka jana baada ya timu ya wataalamu kutoka mamlaka mbalimbali za Serikali kufika na kufanya tathmini huku wakiahidiwa kulipwa ndani ya muda mfupi.

“Lakini hadi sasa hatujui nini kinaendelea wakati wenzetu wa Shinyanga na KIA wenye miradi ya uwanja wa ndege kama sisi, tayari wamelipwa,” amelalamika Jacob.

Mkazi mwingine, Nyamsera Malumba amesema mara ya mwisho waliahidiwa kulipwa ndani ya miezi mitatu kuanzia Februari mwaka huu, lakini ahadi hiyo haijatimizwa.

“Tunaomba tulipwe fedha zetu ili tukajenge makazi mengine, sisi huu mradi wa uwanja tumeupokea kwa moyo mmoja kwa nini Serikali inachelewesha malipo yetu,” amehoji Nyamsera.

Meneja wa Tanroad Mkoa wa Mara,  Vedastus Maribe amekiri wakazi hao kudai Sh3.9 bilioni za fedha baada ya kufanyiwa tathmini ya awali Agosti mwaka jana na kuwa  jambo hilo linafanyiwa kazi.

“Ni watu 50 na wanadai zaidi ya Sh3.9 bilioni, jedwali la fidia limekwishasainiwa na mthamini mkuu, kwa hiyo suala hili linashughulikiwa na Serikali, muda wowote likikamilika hawa wote watalipwa fidia kama inavyotakiwa,” amesema Maribe.

Amewaondoa hofu wakazi hao kufuatia kuwepo kwa taarifa kutoka kwa baadhi ya watu kuwa fedha zimeshatumwa ofisini kwake kwa ajili ya kuwalipa, jambo alilosema si la kweli.

“Pesa ya Serikali haiwezi ikaletwa kisha ikakaa kwenye akaunti bila kufanya shughuli iliyokusudiwa, niwaombe ndugu zangu hawa waendelee kuvuta subira, suala lao linajulikana na ni haki yao watalipwa muda wowote, linashughulikiwa ngazi za juu,” amesema Maribe.

Ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh35 bilioni.

Related Posts