Watu 1,673 wamchangia Lissu Sh. 20 milioni kununua gari

WATU 1,673 wamechanga fedha zaidi ya Sh. 20 milioni kwa ajili ya kumuunga mkono Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, Tundu Lissu, ili anunue gari jipya baada ya lile la awali lililoshambuliwa na watu wasiojulikana 2017, kuwekwa makumbusho. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X, leo Alhamisi, Lissu amewashukuru watu hao waliochanga huku akisema kujitoa kwao ni muendelezo wa safari ya ukombozi wa nchi.

Lissu amesema kiasi hicho cha fedha kimefika baada ya kupita siku tano tangu aendeshe zoezi hilo.

“Hadi sasa tumepokea Sh. 20,029,287.00, wastani wa Sh. 3,983,857.40 kwa siku. Idadi ya waliochangia ni 1,673, wastani wa Sh. 11,972.08 kwa kila mchangiaji. Mvua huanza na tone moja, kwa ukarimu wenu, matone yenu yatatengeneza mvua ya ukombozi wa nchi yetu,” ameandika Lissu.

Gari hilo lilishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana tarehe 17 Septemba 2024, jijini Dodoma, tukio lililohatarisha maisha ya Lissu, ambaye alijeruhiwa maeneo mbalimbali ya mwili.

Baada ya kujeruhiwa, Lissu alianza kutibiwa katika Hospitali Kuu ya Dodoma, kisha alikimbizwa katika Hospitali ya Nairobi. Baadae alipelekwa nchini Ujerumani kwa matibabu zaidi ambako alifanyiwa operesheni kadhaa pamoja na kupatiwa matibabu mengine hadi alipotengemaa.

Related Posts