Hilika arudi na bao, JKU hahishikiki Zenji

BAADA ya kuzikosa mechi mbili za Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) kutokana na kuwa na majukumu ya timu ya taifa, Taifa Stars iliyokuwa Saudia kucheza mechi mbili za kirafiki, straika Ibrahim Hamad ‘Hilika’ amerejea katika ligi hiyo kwa kishindo baada ya jana kufunga bao la 15 msimu huu.

Wakati Hilika alifunga bao hilo lililokuwa la pekee katika pambano kati ya Zimamoto na Kipanga likimfanya amfukuzie kinara wa orodha ya wa ligi hiyo, Suleiman Mwalim Abdalla wa KVZ mwenye mabao 19, JKU nayo imeendelea kuusogelea ubingwa wa ZPL baada ya kuifumua Chipukizi kwa mabao 2-1.

Mechi hizo mbili za ligi hiyo inayoelekea ukingoni zilichezwa kwenye viwanja vya Mao A na B, mjini Unguja, na kwa ushindi huo JKU imefikisha pointi 59 kupitia mechi 26 ikiendelea kuganda kileleni, ilihali Zimamoto ikipanda hadi nafasi ya pili na alama 53, ikiwashusha watetezi KMKM yenye 51 kila moja ikicheza mechi 25.

Katika mechi dhidi ya Kipanga, Hilika aliifungia Zimamoto bao hilo la pekee na la ushindi dakika ya 15 na kumfanya afikishe bao la 15, ikiwa ni manne pungufu na aliyonayo Suleiman Mwalim wa KVZ, wakati Suwedi Juma Hussein na Mudrik Abdi Shehe kila mmoja alifunga bao moja,  JKU ilipoizamisha Kipanga.

Suwedi alifunga bao dakika ya 56 kabla ya Mudrik kuongeza la pili katika dakika ya 73, huku bao la kufutia machozi la Kipanga likiwekwa kimiani na Khalfan Abdalla Saleh. Bao la jana kwa Mudrik linakuwa ni la nane msimu huu, wakati kwa Suwedi na Khalfan ni ya pili kwa timu hizo katika Ligi Kuu iliyosaliwa na mechi za raundi nne kabla ya kufunga pazia katikati ya mwezi ujao.

Matokeo ya jana yamezidi kuiweka pazuri JKU katika kuwania taji hilo linaloshikiliwa na KMKM kwa misimu mitatu mfululizo, kwani kwa sasa inahitaji pointi 10 tu katika mechi nne ili kubeba ubingwa huo na kukata tiketi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu ujao.

Iwapo JKU itavuna pointi hizo 10 itafikisha jumla ya alama 69 zisizoweza kufikiwa na timu yoyote ikiwamo Zimamoto iliyopo ya pili kwa sasa ikiwa na pointi 53 kwani hata kama itashinda mechi tano ilizonazo ikafikia 68 tu, huku watetezi yenye pointi 51 kwa sasa ikishinda michezo mitano iliyonayo, itavuna pointi 66 tu.

Mara ya mwisho kwa JKU kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar ilikuwa msimu wa 2018-2019 ilipotetea kwa mara ya pili mfululizo, baada ya KMKM kulibeba kabla ya kulitema kwa Mlandege na baadaye Mabaharia hao kurejesha ufalme kwa kulitwaa mara tatu mfululizo tangu 2021 hadi sasa inapolishikilia.

Ligi hiyo inaendelea jioni ya leo kwa michezo miwili, Uhamiaji ikikwaruzana na Mlandege kwenye Uwanja wa Mao A, huku Mafunzo ikimalizana na Hard Rock zitamalizana Uwanja wa Mao B.

Bingwa wa ligi hiyo hukata tiketi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku nafasi nyingine ya uwakilishi wa visiwa hivyo za Zanzibar katika Kombe la Shirikisho Afrika, hutokea katika michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) ambapo JKU walio watetezi tayari imeshatinga nusu fainali sambamba na Mlandege, Zimamoto na Uhamiaji.

Msimu huu JKU ilishiriki Kombe la Shirikisho la kung’olewa raundi ya kwanza na Singida Fountain Gate kwa kufungwa jumla ya mabao 4-3 baada ya awali kulala ugenini 4-1 na kushinda 2-0 ziliporudiana, japo mechi zote zilipigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.

Related Posts