JKT laita vijana waliomaliza kidato cha sita kambini

Dodoma. Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limewataka wazazi wa vijana wanaoitwa kujiunga na mafunzo kwa mujibu wa sheria mwaka 2024 wasikubali kutapeliwa kwa kutozwa fedha.

Vijana waliomaliza kidato cha sita mwaka huu, wametakiwa kuripoti katika kambi za JKT kuanzia Juni Mosi hadi 7, 2024.

Akizungumza leo Mei 24, 2024, Mkuu wa Tawi la Utawala wa JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema wanachotakiwa kufanya vijana hao ni kuangalia kambi walizopangiwa kupitia tovuti ya JKT ambako watapata kila kitu.

“Kijana awe na nauli ya kumfikisha kwenye kambi alikopangiwa na kumrejesha nyumbani. Watu wameenda mbali zaidi wanasema vijana wananunua chakula. Chakula haikinunuliwi. Jeshi la Kujenga Taifa linalima mazao ya chakula,” amesema.

Amesema kwa bidhaa nyingine ambazo hazipatikani ndani ya JKT, Serikali inatoa fedha kwa ajili ya kununua pamoja na matibabu kwa vijana hao.

Brigedia Jenerali Mabena amesema wazazi wenye watoto wanaotaka kujiunga na JKT wamekuwa wakitapeliwa fedha tasilimu na kutozwa gharama kubwa ya kuandaa vifaa vinavyohitajika wawapo mafunzoni kitu ambacho siyo sahihi.

Amesema vitendo hivyo vinafanywa na watu wenye nia ovu, jambo ambalo halikubaliki kwa kuwa Jeshi haliuzi nafasi hizo wala halifanyi biashara yoyote.

Amesema Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele, anawaita vijana waliohitimu  kidato cha sita mwaka 2024 kutoka shule zote za Tanzania Bara kuhudhuria mafunzo ya jeshi hilo kwa mujibu wa sheria kwa mwaka huu.

“Tunaishukuru Serikali kwa jitihada zake za kuliwezesha jeshi kuendesha mafunzo ya vijana hao wa kujitolea na kwa mujibu wa sheria, kwa kutenga bajeti ambayo imewezesha pia kuongeza miundombinu na kuweza kuchukua vijana wengi zaidi,” amesema.

Amesema maandalizi yote ya kuwapokea vijana hao yamekamilika na kwamba, wakufunzi wameendelea kupatiwa mafunzo na semina elekezi ya namna ya kuwafundisha vijana hao watakapowasili.

Ametaja kambi wanazotakiwa kuripoti ni Rwamkoma mkoani Mara, Msange (Tabora), Ruvu na Kibiti (Pwani), Mpwapwa na Makutupora (Dodoma).

Nyingine ni Mafinga (Iringa), Mlale (Ruvuma), Mgambo na Maramba (Tanga), Kanembwa, Bulombora na Mtabila (Kigoma), Itaka (Songwe), Luwa na Milundikwa (Rukwa), Nachingwea (Lindi), Oljoro na Makuyuni (Arusha).

Related Posts