Dar es Salaam. Wajumbe wa mkutano mkuu wa kanda nne za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wana kibarua kigumu cha kuamua kina nani wawe viongozi wa kanda hizo katika uchaguzi unaoanza leo.
Kanda ya Victoria yenye mikoa ya Mwanza, Kagera na Geita inafungua pazia la uchaguzi leo.
Kanda zingine ni Serengeti yenye mikoa (Mara, Shinyanga na Simiyu), Magharibi (Tabora, Katavi na Kigoma), na Nyasa (Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe na Rukwa).
Uchaguzi unafanyika baada ya wagombea wanaowania uenyekiti, makamu wake, na mabaraza ya mikoa ya chama hicho, yakiwemo ya Baraza la Wanawake (Bawacha), Baraza la Wazee (Bazecha) na Baraza la Vijana (Bavicha) kupenya katika usaili uliofanyika Mei 11 hadi 14.
Wajumbe watakaoamua uchaguzi huo ni wa kamati za utendaji za kanda husika, wenyeviti wa Chadema wilaya na majimbo katika mikoa inayounda kanda, na wajumbe wa Baraza la Uongozi la mikoa ya kanda.
Ibara ya 7.6.3 katika vifungu vidogo vya a, b, c, d, e, f, na g vya katiba ya Chadema ya mwaka 2006 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019 inaeleza mchakato wa uchaguzi wa kanda.
Hata hivyo, kuna baadhi ya wajumbe (wabunge) hawatakuwapo kwa sababu Chadema hakina wawakilishi bungeni.
Kwa mantiki hiyo wajumbe wa mkutano mkuu wa kanda watatoka katika ibara ya 7.6.3 kifungu kidogo cha a, c na e.
Uchaguzi wa kanda safari hii unatajwa kuwa na ushindani mkali kutokana na kuwapo wagombea wenye sifa, uzoefu, wanaojuana na ambao wanawania nafasi moja.
Kanda ya Victoria inafungua pazia la uchaguzi huo leo kuwapata viongozi watakaohudumu katika kipindi cha miaka mitano.
Mchuano upo nafasi ya uenyekiti inayowakutanisha Ezekia Wenje anayetetea nafasi yake na John Pambalu ambaye ni mwenyekiti wa Bavicha.
“Nimejiandaa kushinda, nimefanya kampeni na kuzungumza na wajumbe, narudia nimejiandaa kushinda,” alisema Wenje.
Pambalu alisema, “Nimefanya maandalizi ya kutosha, nipo tayari kwa matokeo yoyote, ila ninaamini nitashinda kutokana na maandalizi nilioyafanya hadi sasa, sehemu iliyobaki nawaachia wajumbe.”
Katibu wa Kanda ya Victoria, Zakaria Obadi alisema uchaguzi huo utafanyika katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera na maandalizi yanaenda vizuri, ikiwemo wajumbe kuwasili mkoani humo.
Miongoni mwao ni wabunge wa zamani Mchungaji Peter Msigwa na Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ ambao watachuana katika uchaguzi wa kanda ya Nyasa utakaofanyika Mei 29.
Wawili hao waliingia bungeni mwaka 2010 wakitumikia vipindi viwili katika majimbo ya Iringa Mjini na Mbeya Mjini. Walikuwa wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, nafasi ambayo Msigwa bado anaitumikia.
Inadaiwa mchuano kati ya wawili hao umewagawa hadi baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema waliojipambanua kumuunga mkono mgombea fulani wengine kwa kificho na wengine wakiweka hadharani.
Akizungumza na Mwananchi Mchungaji Msigwa alisema kila kitu kinakwenda vizuri katika uchaguzi huo, ikiwemo maandalizi, akisema hana wasiwasi katika mchakato huo.
“Mambo yanakwenda vizuri sina shaka na kesho (Jumamosi) nitakuwa Dar es Salaam, katika mjadala kuhusu suala hili,” alisema Mchungaji Msigwa.
Hivi karibuni Sugu aliliambia Mwananchi kuwa yupo vizuri kuelekea katika uchaguzi huo, utakaofanyika katika Mji wa Makambako mkoani Njombe ambapo wajumbe zaidi ya 100 wataamua hatima yao.
Mchuano mwingine utakuwepo katika Kanda ya Magharibi yenye wagombea wanne ambao ni Dickson Matata, Gaston Garubindi, Mussa Martine na Ngassa Mboje wanaouwania uenyekiti.
Wanaowania nafasi ya makamu ni Masanja Katambi na Rhoda Kunchela, uchaguzi wa kanda hiyo utafanyika mkoani Tabora.
Kwa mujibu wa katibu wa kanda hiyo, Ismail Kangeta watakaopiga kura katika nafasi ya mwenyekiti na makamu ni 81.
Kanda ya Serengeti itawakutanisha vigogo wengine Gimbi Masaba ambaye kwa sasa ni makamu mwenyekiti wa kanda hiyo na Lucas Ngoto aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mara.
Katibu wa Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawani alisema uchaguzi huo utafanyika mkoani Shinyanga na wapigakura takribani 90 wanatarajiwa kupiga kura.