Katwila, Mwangata wapewa ‘thank you’ Mtibwa

MABOSI wa timu ya Mtibwa Sugar umewapiga chini, Kocha mkuu wa timu hiyo,  Zuberi Katwila pamoja na wasaidizi wawili,  Kocha wa Makipa, Patrick Mwangata na Meneja, Henry Joseph kutokana baada ya timu na mwenendo mbaya katika michezo ya Ligi kuu Bara ikiwa inaburuza mkia kwa sasa.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Mtibwa kimesema, Bodi ya Wakurugenzi imefikia hatua hiyo baada ya kutoridhishwa na matokeo ya uwanjani ambapo timu hiyo iko kwenye presha ya janga la kushuka daraja.

Makocha hawaambatana na timu mjini Kigoma kwa mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ambao kama timu hiyo itapoteza itashuka rasmi.

“Ni kweli bodi ya Wakurugenzi imefanya maamuzi ya kuwasimamisha watatu hao kwenye benchi la ufundi la timu hiyo na kuna changamoto ambazo zimewafanya wasiaminiwe tena, hawajavunjiwa mikataba moja kwa moja naamini baada ya mechi ya Mashujaa tutajua kwa undani kama wataondoka moja kwa moja au la!” Kimesema chanzo hicho.

Chanzo hicho kinasema mchezo wa kesho utakuwa chini ya kocha msaidizi, Awadh Juma ‘Maniche’.

Katwila alikabidhiwa mikoba ya kuinoa Mtibwa kama kocha mkuu akichukua nafasi ya KlHabib Kondo aliyeondolewa baada ya timu hiyo kuwa na mwenendo usioridhisha Oktoba 23, 2023.

Tangu  wakati huo Mtibwa haijazinduka kwani iko katika ombwe la kushuka daraja.

Mwanaspoti limejaribu kuwasiliana na Kocha Katwila kwa njia ya simu lakini ilikuwa ikiita bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe kwa njia ya meseji haukujibiwa.

Alipotafutwa Ofisa Habari wa klabu hiyo,Thobias Kifaru ili kuthibitisha taarifa hizo alisema yuko msibani baada ya kiwanda hicho kupata hitilafu na kuua watu 11 ambapo atazungumza Jumatatu.

“Niko msibani kwa sasa, kuna wafanyakazi wenzetu walifariki kwa ajali, hivyo kuhusu taarifa hizo nitazungumza Jumatatu baada ya kuonana na viongozi. Huu ni msiba mkubwa kwetu, ” amesema Kifaru.

Related Posts