Dar es Salaam. Mauaji ya Penina Method, mkazi wa Goba jijini Dar es Salaam yanaongeza orodha ya matukio ya wenza kuuawa kutokana na kinachoelezwa kuwa, wivu wa mapenzi.
Penina (27) ameuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali kinachodhaniwa kuwa panga chanzo kikidaiwa ni wivu wa mapenzi.
Tukio hilo linalodaiwa kutendwa na mpenzi wake Joseph Ngosha (31), lilitokea asubuhi ya Mei 23, 2024 eneo la Goba Centre wilayani Kinondoni anakofanya biashara Penina.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema wamemkamata Ngosha kwa tuhuma za mauaji hayo.
Amesema tukio hilo lilitokea saa moja asubuhi ya Mei 23 mwaka huu katika eneo la Penina Pub.
“Uchunguzi wa awali wa polisi unaonyesha kulikuwa na mgogoro wa kimahusiano kati ya mtuhumiwa na marehemu kabla ya kushambuliwa kwa panga na mtuhumiwa. Upelelezi unakamilishwa ili mtuhumiwa afikishwe mahakamani haraka,” amedai Kamanda Muliro.
Mmoja wa madereva wa bodaboda aliyekuwa karibu na Penina amedai siku nne kabla ya kuuawa, Penina na mpenzi wake walikuwa na mvutano uliosababisha kurushiana chupa katika eneo lake la biashara.
“Kabla ya jana walipigana hapa baa wakarushiana chupa za kutosha kwa kuwa ni wapenzi wakamaliza tofauti zao na kwenda nyumbani kwao,” amedai bodaboda ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Amedai kuwa, mtuhumiwa alishamkataza Penina kufanya biashara ya pombe licha ya kuchangia kiasi cha pesa cha kufungua biashara hiyo na alimtaka ashinde nyumbani kwa kuwa alishaweka wasaidizi wanne wa kumsaidia kufanya biashara hiyo.
Kwa mujibu wa bodaboda huyo, Penina alitakiwa na mpenzi wake awe anachukua hesabu na kurudi nyumbani.
Siku ya tukio mwanamume huyo alikodi bodaboda na kufika eneo la tukio, alimkuta Penina akiwa katika maandalizi ya kurudi nyumbani baada ya kufunga biashara.
“Mwanamume alishamkataza asiwe anakuja katika hii biashara na kukesha, baada ya kuona hajarudi nyumbani akaamua kumfuata ofisini kwake na alipofika alitoa panga na kuanza kumkatakata,” amedai.
Kwa kuwa kilikuwa kitendo cha haraka, bodaboda aliyedai alimbeba mwanamume huyo alishuka na kukimbilia Kituo cha Polisi Goba akifikiri panga lile lilitolewa kwa ajili yake, waliporejea walikuta tukio limetendeka.
“Baada ya kitendo hicho, anawaambia watu haamini kama ameua, hivyo alitaka watu wamuangalie mara mbili kwa kuwa haikuwa dhamira yake kumuua mpenzi wake,” amedai.
Ziada Mnyoo, mama mdogo wa Penina amesema tangu wamfahamu mwanamume huyo hawajawahi kusikia wana ugomvi, hivyo kwao limekuwa jambo la kushtukiza.
“Sijui kitu gani kimetokea maana hatujawahi kusikia wala kuwaona wakigombana walikuwa wanapendana, hatuelewi chanzo ni nini,” amesema Ziada.
Amesema Penina ameacha watoto wawili, mmoja wa miaka 10 na mwingine wa miaka mitano.
Ziada amesema wanatarajia kumzika Penina katika makaburi ya Goba.
Amina Salum, jirani wa Penina amesema wakati mwingine watu wanatakiwa kuishi kutokana na mazingara waliyokutana, hivyo ni ngumu kukuta mtu baa na kutarajia aishi maisha tofauti na waliyokutana.
“Mwanamume amekosea kuchukua sheria mkononi kwa madai kuwa mwanamke atakuwa na wanaume wengine kwa sababu ya kushinda kwenye eneo lake la kazi ambapo linawapatia kipato,” amesema.
Kwa mujibu wa ripoti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ya mwaka 2023, vifo vya wenza vimeongezeka kwa kukusanya matukio 50.
Kati ya hayo 45 yalikuwa ya wanawake sawa na asilimia 90, huku matano yalikuwa ya wanaume sawa na asilimia 10.
Ripoti hiyo inaeleza wivu wa mapenzi ni sababu kuu kwa asilimia 40 ya matukio ya mauaji ya wenza yaliyoripotiwa mwaka 2023.
Kwa mujibu wa utafiti huo, wanawake walipata madhara mikononi mwa wapenzi wao kwa kuchomwa visu, kuchomwa moto, kukatwa kichwa, kunyongwa, kupigwa na kuingizwa kitu chenye ncha kali sehemu za siri.
Getrude Dyabene, wakili na mwanasaikolojia wa LHRC, akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Mei 24, 2024 amesema mauaji ya wenza hayatokei ghafla kama inavyofikiriwa bali jambo hilo huanza kidogokidogo na baadaye kukomaa na kuonekana la kawaida.
“Kwa kawaida mtu anaanza kidogo kama hakuwa na tabia ya kukupiga na ikatokea akaanza kukupiga hata kofi na ikachukuliwa ni kawaida inajijenga kwenye akili na kuzoea kupiga na hatimaye kuua,” amesema.
Amesema kuendelea kwa matukio ya vifo vya wenza kunasababishwa na kukosekana kwa uwajibikaji katika ngazi zote.