Dodoma. Serikali imeingiza maudhui ya elimu ya uraia na uzalendo katika mitaala mipya ya mwaka 2023, kupitia somo jipya la Historia ya Tanzania na Maadili.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omar Kipangaa ameyasema hayo leo Mei 24, 2024 wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Najma Giga.
Najma amehoji ni kwa nini Serikali isiweke kwenye mitaala somo la uraia na uzalendo ili kizazi kijacho kiwe na uelewa wa haki na wajibu wa raia nchini.
Akijibu swali hilo, Kipanga amesema Serikali kwa kutambua umuhimu wa kutoa elimu ya uraia na uzalendo kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Amesema Serikali ilifanya maboresho ya mitalaa ya elimu mwaka 2023 ambapo katika maboresho hayo, tayari maudhui kuhusu elimu ya uraia na uzalendo yameingizwa katika mitaala hiyo.
Aidha, amesema maudhui hayo yameingizwa kupitia somo jipya la Historia ya Tanzania na Maadili, litakalofundishwa kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita.
Amesema somo la Historia na maadili litabeba maudhui yanayolenga kumjenga Mtanzania kuwa mzalendo na muwajibikaji anayefahamu historia, desturi, mila na maadili ya nchi yake.
Katika swali lake la nyongeza, Najma amehoji iwapo mtaala huo umeshaanza kutumika.
Pia amehoji kwanini Serikali haioni umuhimu wa kurudisha vitabu vilivyokuwa vikitumika zamani.
Amevitaja vitabu hivyo kuwa ni pamoja msichana jifahamu ambacho kinamjenga kijana wa kiume na kike kuweza kujikinga na mahusiano yasiyo rasmi katika umri mdogo ambayo yanasababisha kuharibikiwa kimasomo pamoja na kupotoka kwa maadili.
Akijibu swali hilo Kipanga amesema mitaala mipya imeanza kutekelezwa mwaka huu kwa awamu ambapo mwaka huu wameanza na elimu ya awali, la darasa la kwanza na la tatu.
Kuhusu kurejesha vitabu vya zamani, Kipanga amesema vipo vitabu vya zamani ambavyo vinatumika hivi sasa lakini pia yapo baadhi ya maudhui yameingizwa kwenye vitabu vinavyotumika hivi sasa.