Mfanyabiashara atishia kuliburuza Jiji la Arusha kortini, adai Sh63 milioni

Arusha. Mfanyabiashara wa vipuri vya magari,  ametishia kuiburuza Halmashauri ya Jiji la Arusha Mahakamani,  kwa madai ya kushindwa kumlipa deni lake la Sh63 milioni kwa zaidi ya miaka tisa sasa.

Amesema atafikia uamuzi huo endapo jiji hilo litashindwa kulipa deni hilo ndani ya siku 30 zilizotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Felician Mtahengerwa.

Mfanyabiashara huyo, Prosper Kessy anayemiliki Kampuni ya Proskes Enterprises ameyasema hayo leo Alhamisi Mei 23, 2024 kwenye kliniki ya kusikiliza kero za wananchi iliyoandaliwa na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mtahengerwa.

Akizungumza mbele ya mkuu huyo wa wilaya,  Prosper amesema amefika kutoa kero yake mbele ya kiongozi huyo ili azungumze na uongozi wa Jiji la Arusha juu ya madai yake.

“Nimekuja hapa kutoa malalamiko yangu mbele yako na watu wote waliojitokeza hapa juu ya dhulma ninayotaka kufanyiwa na Halmashauri ya Jiji la Arusha,” amesema Prosper.

Amesema alifanya biashara na Jiji hilo ya kuleta vipuri vya magari ya Serikali vyenye thamani ya Sh63 milioni mwaka 2015, lakini mpaka sasa hajalipwa fedha zake.

Amedai alianza kudai ofisi ya mhasibu na ya mkurugenzi wanampiga tarehe wakidai malipo yake yanashughulikiwa.

“Baada ya miaka miwili baadaye wakaanza kunigeuka wakisema hawaoni kumbukumbu ya deni langu, hivyo nilete nyaraka, nilipopeleka nikaambiwa subiri wiki moja Mkuu (DED) apitie mafaili yote atakutana na la kwangu, amesema na kuongeza;

“Nimekanyaga ofisi hizo kila siku hadi leo majibu ni hayo hayo, huku wakurugenzi wanakuja na kuondoka mimi bado nasota tu, sasa mkuu nimeona kabisa hapa hakuna dalili ya kulipwa deni langu, naomba utoe tamko kwao wanilipe fedha zangu,” amesema Prosper.

Mkuu huyo wa wilaya alimuita Kaimu  Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Shaban Manyama kutoa majibu juu ya madai ya mfanyabiashara huyo.

Naye akajibu kuwa hajawahi kuliona faili lenye madai hayo na akamuomba Proper awasilishe  nyaraka zake zinazothibitisha deni lake.

“Hakuna deni ambalo Serikali hailipi, nimuombe ndugu Prosper awasilishe nyaraka za deni lake ikiwemo mkataba wa kazi na makubaliano yote na kama ikionekana ni kweli na anastahili kulipwa, atalipwa,” amesema Manyama.

Baada ya majibu hayo, mkuu wa wilaya ametoa siku 30 kwa Halmashauri ya Jiji la Arusha kuhakikisha inalipa deni hilo.

“Acheni ubabaishaji bwana, ina maana huyu mtu mzima atatoka huko kote aje hapa aseme anawadai kwa uongo, hebu lipeni madeni ya watu, nataka ndani ya hizi siku 30 kuanzia leo muwe mmemlipa mfanyabiashara huyu deni lake la sivyo tutaonana wabaya,” amesema Mtahengrwa.

Akizungumza nje ya ukumbi, Prosper amesema deni hilo ni la mda mrefu na amepeleka mashtaka ngazi mbalimbali za uongozi bila msaada hivyo mwishowe atalazimika kwenda mahakamani kudai haki yake.

Naye Dominic Massawe amemwambia mkuu wa wilaya anakusudia kulishitaki Jiji kwa sababu halitaki kumlipa deni lake la Sh900,000.

Maasawe amesema Aprili 5, 2023 alifanya kazi ya kupaka rangi jengo zima la halmashauri kwa makubaliano ya kulipwa kiasi hicho cha fedha, lakini mpaka sasa ni zaidi ya miezi 11 hajalipwa.

“Mkuu naomba nisaidie maana juzi nilienda kliniki ya mkuu wa mkoa lakini sikupata nafasi ya kuonana naye na kila kitu kiko kwenye maandishi, lakini kila nikienda wananipiga tarehe ya kurudi wakidai wanashughulikia lakini hadi leo hakuna matumaini,” amesema Massawe.

Katika hilo Mtahengerwa alijumlisha deni hilo na la Prosper akilitaka jiji hilo kuhakikisha linalipa madeni hayo ndani ya siku 30.

Related Posts