KAIMU kocha mkuu wa Simba, Juma Mgunda amesema hana wasiwasi kwa mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC, kwani tayari ameshaliandaa jeshi alililonalo kushuka Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini hapa ili kuzisaka pointi tatu mbele ya wapinzani wao hao waliotoka nao sare ya 2-2 katika mechi ya kwanza.
Mchezo huo utakaopigwa kesho unatazamiwa kuwa mgumu kutokana na mahitaji ya timu zote,Simba SC ikihitaji ushindi ili kujitengenezea mazingira mazuri ya kumaliza nafasi ya pili,KMC FC nao wakiiwazia nafasi ya nne.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Bara,Simba inashika nafasi ya tatu kwa alama 63 sawa na Azam FC iliyopo nafasi ya pili huku zikitofautiana magoli ya kufunga na kufungwa.
Mnyama katika mechi 28 ilizocheza hadi imeshinda 19, sare sita na kupoteza tatu huku ikifunga magoli 56 na kuruhusu nyavu zao kuguswa mara 25 na rekodi zinaonyesha katika mechi tano za mwisho imeshinda nne na kupata sare moja. Mechi hizo ni dhidi ya Geita Gold iliyoshinda 4-1, Dodoma Jiji (0-1), Kagera Sugar (1-1), Azam (0-3), Tabora United (2-0) na Mtibwa Sugar 2-0.
Kwa upande wa KMC inayoshika nafasi ya tano ikiwa na pointi 36 tofauti ya alama tano na zile ilizonazo Coastal Union iliyopo juu yao na alama 41, imeshinda mechi nane sawa na ilizopoteza, ikitoka sare 12 baada ya kufunga mabao 27 na kufungwa 38.
Wakizungumzia mechi hiyo itakayopigwa saa 10:00 jioni sambamba na mechi nyingine saba za ligi hiyo, makocha wa timu zote waliweka mipango yao, huku Mgunda akisema maandalizi kuelekea katika mchezo huo yamekamilika kikubwa mashabiki wanatakiwa kujitokeza kwa wingi kesho ili kutoa sapoti kwa wachezaji.
“Maandalizi yote ya kucheza mechi ngumu,nzito yenye kuhitaji matokeo yamekamilika,”amesema Mgunda, huku kipa wa timu hiyo, Ally Salim aliongeza kwa kusema kama wachezaji wana morali ya juu kuhakikisha mchezo huo muhimu ambao utaendelea kutoa dira ya kumaliza nafasi ya pili wanashinda.
Kwa upande wa kocha msaidizi wa KMC, John Matambala ameweka wazi nyota wawili wa timu hiyo, Awesu Awesu na Fred Tangalo waliokuwa majeruhi pamoja na kipa Wilbrod Maseke aliyekosa mechi iliyopita watakuwepo katika mchezo huo wa kesho, japo Andrew Vincent na Ismael Gambo watakosekana kesho.
“KMC tunahitaji kushinda mchezo wa kesho ili kujitengenezea mazingira mazuri ya kumaliza nafasi ya nne,” amesema Matambala.
Katika mchezo huo wa kesho nyota wa kuchungwa zaidi na mabeki wa timu zote ni Waziri Junior wa KMC mwenye mabao 12 na Saidi Ntibazonkiza wa Simba, aliyefunga tisa hadi sasa akiwa ndio kinara wa timu hizo.
Mara ya mwisho timu hizo kukutana ilikuwa ni Desemba 23, 2023 na zilishindwa kutambiana kwa kufunga mabao 2-2