Motsepe atua Zanzibar kushuhudia fainali ASFC

Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf), Patrice Motsepe ametua Zanzibar leo kushuhudia fainali za mashindano ya African Schools Football Championship Kwenye Uwanja wa Amaan leo.

Motsepe ambaye kwa mara ya mwisho alitua hapa nchini mwaka jana kwenye ufunguzi wa michuano mipya ya African Football League kati ya Simba na Al Ahly amepokelewa na mwenyeji wake Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia.

Rais huyo ataanza kuushuhudia mchezo wa kwanza wa fainali ya wanawake kati ya Morocco na Afrika Kusini kuanzia saa 9:30 alasiri na baada ya hapo ataangalia ule wa timu ya Tanzania wanaume ambayo itavaana Guinea kuanzia 10:30, zote zikipigwa kwenye Uwanja wa Amaan kwa dakika 40 kila mmoja.

Akizungumza baada ya kutua Zanzibar, Motsepe alisema anafurahi kuja tena nchini na anaamini vijana hawa wanaokwenda kucheza fainali atawaona kwenye timu ya Taifa ya Tanzania miaka michache ijayo.

“Leo ninafuraha sana kwa kuwa tupo hapa kwa ajili ya kuwekeza kwa ajili ya soka la baadaye, vijana wengi ambao tunawaona hapa baadaye watacheza kwenye timu ya Taifa ya Tanzania.

“Hapa Tanzania ukiona timu ya Taifa inacheza nafahamu kuwa mashabiki wa Simba na Yanga wanakuwa kitu kimoja kuiunga mkono timu hiyo, huku ni kuwekeza kwa ajili ya maisha ya soka ya baadaye na naamini kila mmoja anafarahia hatua hii,” alisema Motsepe raia wa Afrika Kusini.

Tanzania iliingia fainali baada ya kuichapa Benin mabao 2-0, huku Guinea ikitinga fainali baada ya kuichapa Senegal kwa penalti 4-3, baada ya kutoka suluhu.

Related Posts