Naibu Spika Zungu auliza swali kwa mara ya kwanza

Dodoma. Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu ameshauri Serikali kutumia kipengele cha dharura katika Sheria ya Manunuzi ya Umma, ili kuharakisha mchakato wa barabara zilizoharibiwa na mvua kwenye majiji ikiwemo jiji la Dar es Salaam.

Hii ni mara ya kwanza kwa Zungu kuuliza swali akiwa katika kiti chake cha ubunge tangu alipochaguliwa kushika nafasi hiyo.

Akiuliza swali la nyongeza leo Mei 24, 2024, Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu amesema Mkoa wa Dar es Salaam unachangia pato la Taifa kwa zaidi ya asilimia 75, lakini miundombinu yake ya barabara na mifereji imeharibika sana.

“Kutokana na shida hii mapato ya nchi yanaweza kupungua kwa sababu ya miundombinu hii kuchelewesha kuendesha uchumi kwa haraka,” amesema.

Amehoji ni kwa nini Serikali isitoe kauli wakurugenzi wote wa Dar es Salaam kuzingatia kanuni na sheria ya ununuzi kwa kutumia kipengele cha dharura ili barabara zitengenezwe kwa fedha za Serikali, ambazo zimechangia kuletwa kutoka katika halmashauri nchini na mapato ya ndani ambayo wameyatenga.

Ametoa mfano wa Manispaa ya Ilala ambayo imetenga mapato yake na kwamba mchakato kuwapata makandarasi inachukua muda mrefu na hivyo kuchelewesha maendeleo ya Dar es Salaam yanayochangia mikoa mingine nchini.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Zainab Katimba amesema Serikali inatambua umuhimu wa barabara za wilaya katika maendeleo ya kiuchumi kwenye Taifa.

“Ni dhahiri kumekuwa na mvua nyingi ambazo zimeleta madhara mbalimbali katika miundombinu. Serikali pamoja na kwamba kuna fedha zimetengwa na zinaendelea kutengwa, inakusudia kuhakikisha kuwa inaboresha miundombinu.

Amesema kutokana na mvua ambazo zinaendelea kunyesha kwenye kipindi hiki, hatua za ununuzi zinaendelea huku wakisubiri  mvua imalizike na Tamisemi ilishatoa maelekezo kwa baadhi ya halmashauri hasa za majiji zitenge fedha kutoka kwenye mapato yao ya ndani kwa ajili ya marekebisho mbalimbali ya barabara.

Ameongeza kuwa kuna barabara nyingine hazina mawasiliano kabisa, hivyo kwa kuzingatia maelezo yaliyokwishatolewa huko awali na Waziri wa Tamisemi,  amezikumbushia halmashauri zichukue hatua kwa sababu wameshatenga fedha kwenye mapato yao ya ndani.

Amesema hatua hiyo itawawezesha kufanya marekebisho hasa kwa maeneo ambayo barabara hazipitiki kabisa.

Related Posts