Ni wikiendi ya Chasambi na Waziri junior

SIMBA wana Ladack Chasambi wamoto na KMC wanatambia Wazir Junior. Shughuli ipo kesho kwenye Uwanjwa Sheikh Amri Abeid.  Ni wachezaji wawili wazawa ambao katika wiki za hivikaribuni takwimu zao zinavutia viwanjani na leo wanaingia uwanjani kiloa mmoja akibeba ramani ya timu yake.

 Hii itakuwa mechi ya 12 kwa Simba kukutana na KMC katika ligi huku picha iliyopo kwa wadau na mashabiki wa timu hizo ni matokeo ya mzunguko wa kwanza ambapo Mnyama alivutwa shati kwa kutoka sare ya mabao 2-2 na kusanya mapata hao wa Manispaa ya Kinondoni huku Wazir aking’ara kwa kufunga mara mbili.

Simba inayopambana kumaliza msimu katika nafasi ya pili, itaingia katika mchezo huo ikiwa katika kiwango bora kwa kushinda mechi tano na kutoa sare mbili chini ya kaimu kocha mkuu, Juma Mgunda pamoja na msaidizi wake, Seleman Matola tangu walirithi mikoba ya Abdelhak Benchikha aliyeachana na timu hiyo baada ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Muungano visiwani Zanzibar.

Katika michezo hiyo, miongoni mwa wachezaji walioibuka na kufanya vizuri kwenye kikosi hicho ni pamoja na Chasambi ambaye alifunga mabao mawili katika mchezo uliopita ambao Simba iliibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Geita Gold hapo kabla hakuwa akipata nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Chasambi mwenye uwezo wa kushambuliaji nyuma ya mshambuliaji na hata katika maeneo ya pembeni (winga), alikuwa msaada kwa Simba kwenye uwanja wa Kaitaba katika mchezo ambao walivuna pointi moja wakati wakitoka sare ya bao 1-1, nyota huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar alicheka na nyavu.

Kasi na maarifa ni miongoni mwa mambo ambayo yanambeba kiasi cha kumfanya kuwa na madhara kwa wapinzani hivyo mabeki wa KMC, wanatakiwa kuwa naye macho, Mgunda amekuwa akimpa uhuru wa kuisogeza timu mbele.

Mbali na Chasambi mwenye mabao manne katika ligi  lakini pia Mgunda anawigo mapana wa machaguo katika kikosi chake cha kwanza, anaweza kuendelea kumtumia Edwin Balua naye mwenye mabao manne katika moja ya maeneo yake ya pembeni na amekuwa na mchango mzuri katika kikosi hicho.

Huku Saido Ntibazonkiza mwenye mabao tisa naye akitarajiwa kuongoza vijana hao wakati mbele akitarajiwa kusimama Freddy Michael mwenye mabao sita ambaye naye amekuwa katika kiwango bora huku akionekana kuwa hana mpinzani katika kikosi hicho kwa sasa katika eneo la mwisho la ushambuliaji.  

Wakati hizo zikiwa miongoni mwa silaha muhimu kwa Simba kwa upande wa kocha wa KMC, Abdihamid Moalin anajivunia kuwa na Wazir ambaye anashika nafasi ya tatu katika orodha ya nyota ambao wanawania kitu cha ufungaji bora akiwa na mabao 12 nyuma ya Stephane Aziz KI (17) wa Yanga na Feisal Salum (16) wa Azam FC.

Uwezo wa kukaa katika maeneo sahihi ni miongoni mwa vitu ambavyo vinambeba Wazir ambaye anamlima wa kufunga mabao matano ili kumfikia Aziz KI, hivyo mabeki wa Simba wanatakiwa kuwa naye macho vinginevyo yanaweza kutokea yale kama ilivyokuwa katika mzunguko wa kwanza.

Simba yenye pointi 63 sawa na Azam FC, inahitaji ushindi katika mchezo huo ili kuweka hai matumaini yao ya kumaliza msimu katika nafasi ya pili ili wapate tiketi ya msimu ujao kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.

Sio tu kupata ushindi katika mchezo huo, Simba inatakiwa pia kutafuta mtaji mzuri wa mabao ili kuweka akiba ya baadae kutokana na kulingana kwao pointi na wapinzani wao Azam katika nafasi hiyo.

Ikoje? Kwa sasa Azam inashika nafasi ya pili kutokana na kuruhusu kwao mabao machache 20, Mnyama ameruhusu mabao 25, wote wamefunga mabao sawa 56.

Kwa upande wa KMC, wao wamejikakikishia kusalia katika ligi ambacho wanapambania kwa sasa ni kumaliza msimu katika nafasi nne za juu jambo ambalo linawezekana kutokana na utofauti wa pointi uliopo (5) baina yao ambao wapo nafasi ya tano na Coastal Union ya Tanga huku zikisalia mechi mbili.

Katika michezo 11 ambayo wamekutana ndani ya msimu sita, Simba imeonyesha ukubwa wake kwa kutopoteza hata mara moja, ilichoambulia KMC ni kupata sare tu na wamefanya hivyo katika michezo miwili tu na yote ilikuwa ya mabao 2-2.

Achana na sare ya mzunguko wa kwanza, Septemba 7,2022 napo walitoshanga nguvu kwa matokeo ya aina hiyo.

Simba imeshinda mara tisa dhidi ya KMC na miongoni mwa vipigo vikubwa kutoa ni kile cha Desemba 12,2021 Mnyama alishinda kwa mabao 4-1 katika mchezo huo, Kibu Denis alifunga mabao mawili huku mengine yakifungwa na Mohammed Hussein na Joash Onyango ambaye kwa sasa yupo Ihefu.

Kaimu kocha wa Simba, Juma Mgunda anaamini kuwa mchezo utakuwa mgumu kutokana na ubora wa KMC hivyo wamejinga kuhakikisha wanapata pointi tatu katika mchezo huo ili kuendelea na safari yao ya kumaliza vizuri msimu.

“Vijana wapo tayari kwa mchezo tunajua ubora wa wapinzani wetu kwa hiyo tutatumia madhaifu yao kuwaadhibu, naamini tunaweza kumaliza msimu katika nafasi ya pili bado nafasi tunayo,” alisema kocha huyo.

Kwa upande wake, Moalin alisema,”Ni mechi ngumu kutokana na wapinzani wetu kuwa bado na hesabu za kutaka nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa kwetu tunahitaji kufanya vizuri pia kama ilivyo kwao kwa sababu itakuwa jambo jema kumaliza msimu katika nafasi za juu zaidi, tunawaheshimu Simba na sote tumeona namna walivyoimarika lakini tumejianda kukabiliana nao.”

Related Posts