NA filimbi ya mwisho itapigwa na mwamuzi wa pambano la baadaye leo kati ya Manchester United na Manchester City. Mwamuzi atakayepuliza filimbi hiyo ni Andrew Madley. Baada ya filimbi yake ndio tutajua kwamba Erik Ten Hag wa Manchester Utd ataendelea kubaki kibaruani au vinginevyo.
Kuna wanaosema kwamba haijalishi ambacho kitatokea leo Wembley, huenda Ten Hag atafukuzwa. Kuna wengine ambao wanasema hatafukuzwa hata kama United haitafuchukua Kombe la FA.
Vyovyote ilivyo, mashabiki wa Liverpool ndio tumbo joto zaidi. Baada ya Jurgen Klopp kusimamia pambano lake la mwisho la Liverpool nyumbani dhidi ya Wolves wikiendi iliyopita, yeye mwenyewe alisimama na kumtangaza kocha mpya wa Liverpool, Arne Slot.
Liverpool wameletewa kocha kama Erik Ten Hag. Anatoka nchi ileile, ana kichwa kama kilekile ambacho kina upara. Ana wasifu kama uleule ambao Ten Hag alikuja nao England. Wakati Ten Hag alitamba na Ajax na kuipa ubingwa wa Uholanzi, Slot ametamba na Feyernood na ameipa ubingwa wa Uholanzi msimu uliopita.
Sio kila mwenye upara ni Pep Guardiola na ndio maana kwa kupitia upara wake mashabiki wa Liverpool watakuwa wanajiuliza, Slot ni Ten Hag mpya au Pep mpya? jibu lake ni gumu. Hata hivyo kuna kitu mashabiki wa Liverpool watakuwa hawaombei.
Labda huu ni mwanzo mpya wa mahangaiko baada ya kufaidi vilivyo utawala wa Klopp. Utawala wa soka safi ambao ulirudisha taji la Ligi Kuu England (EPL) baada ya miaka 30. Utawala wa soka safi ambapo inawezekana bila Guardiola, basi wangeweza kuchukua hata mataji matano mfululizo ya EPL.
Utawala wa Klopp ambao haukuwaacha hivihivi bila taji la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya ambalo ni miongoni mwa mataji ambayo hayawapi shida kuyachukua. Utawala uliowapa utatu mtakatifu wa Sadio Mane, Mo Salah na Roberto Firmino. Kikosi kizima kilikuwa cha moto.
Na sasa kikosi kimepotea na kocha ameondoka. Inanikumbusha namna ambavyo Sir Alex Ferguson aliondoka zake Old Trafford jioni ile ya Mei 2013 na kuanzia hapo wamekuwa wakiishi katika majuto hadi leo. Wamepita wengi hadi wakafika katika kipara cha Ten Hag ambaye leo anawaacha katika nafasi ya nane katika msimamo wa ligi.
Liverpool inaanza mwendo huu au Slot anaweza kufanya maajabu pale Anfield. Hofu inakuja kwamba anatoka katika ligi ambayo sio ngumu. Wakati mwingine kuanzia mchezaji hadi kocha, anaweza kutoka katika Ligi Kuu Uholanzi au Ubelgiji lakini akachemsha England.
Ni rahisi kuipima kwa macho Ligi Kuu England, lakini ukiingia uwanjani unagundua kwamba hii ndio ligi ngumu zaidi duniani. Ni ligi ya machozi, jasho na damu. Ten Hag yule aliyetamba na Ajax ndiye huyuhuyu ambaye anaweza kufukuzwa kazi huku United ikishika nafasi ya nane katika msimamo. Timu tajiri zaidi England.
Wakati huohuo, Slot ana kazi ya kukijenga upya kikosi cha Klopp. Hajaachiwa timu mbaya sana lakini ukweli ni kwamba bado ipo katika mpito. Tazama namna walivyochapwa mabao 4-0 palepale Anfield na ndugu zetu Atalanta. Tazama namna ambavyo walichoka mwishoni katika mbio za ubingwa wa England na kuwaacha Guardiola na Mikel Arteta wakikimbizana.
Wakati huohuo, kuna uamuzi mkubwa unapaswa kufanyika Anfield. Mo Salah anaweza kwenda kuchukua pesa za Waarabu wenzake kule Saudia. Hakuna anayeweza kumlaumu kwa sababu hata Mane na Firmino walikwenda na kupewa mkono wa baraka na mashabiki wa Anfield kwa sababu umri ulikuwa umesogea na walikuwa wameacha alama kubwa Anfield. Salah anaweza kufuata nyayo.
Wakati huohuo, Virgil Van Dijik hawi kijana tena. Umri unasogea. Julai mwanzoni anatimiza miaka 33. Slot atakuwa anakwenda katika kambi ya maandalizi ya msimu mpya akiwa na VVD mzee tofauti na ilivyokuwa katika zama za Klopp.
Kuna vijana wabichi ambao Klopp aliwaingiza. Kuna washambuliaji ambao mashabiki wa Anfield wana wasiwasi nao. Darwin Nunez na Cody Gapko. Slot anaweza kufanya nao kazi kutengeneza utatu mwingine mtakatifu kama ule wa kina Salah, Mane na Firmino?
Majibu tutaanza kuyapata msimu ujao. Slot anakwenda kuvaa viatu vizito. Tukimuweka kando Don Caro Ancelotti ambaye anajulikana kwa miaka mingi, sisi wengine tunaamini kwamba makocha bora zaidi duniani kwa sasa ni Guardiola na Klopp. Kuvaa viatu vyao ni kazi ngumu.
Hakuna makocha wengi bora duniani. Hauwezi kuwalaumu Liverpool kwa sababu wasingeweza kumpata Pep kuwa mbadala wa Klopp wala wasingeweza kumpata Mikel Arteta. Ilibidi wampate mtu mwingine kutoka kwingineko. Mtu ambaye bahati mbaya au nzuri kwao ametoka katika ligi nyingine, tena ambayo sio miongoni mwa ligi tano bora Ulaya.
Kama wamecheza Kamari au vinginevyo wakati utatuambia. Hata hivyo, ukweli ni kwamba Slot anakwenda katika matanuri mawili ya moto. Anfield yenyewe ni tanuri la moto. Timu ambayo ina mashabiki wehu na wanasimama nyuma ya timu yao. Bahati mbaya kwake ni kwamba baada ya kusuasua kwa miaka mingi Klopp alifanikiwa kuwarudishia Liverpool yao. Lakini ligi yenyewe pia ni tanuri la moto. Upinzani uliopo mkubwa na pambano la Liverpool dhidi ya West Ham ni la moto mkubwa kuliko pambano la Feyernood dhidi ya FC Twente. Kazi anayo.
Wakati utatuambia kwamba huu utaendelea kuwa mwendelezo wa Klopp au mwanzo wa mahangaiko mengine ya Liverpool kama ambavyo maadui zao United wamekuwa wakihangaika tangu kuondoka kwa Sir Alex.