Idadi ya Wahitimu katika Mahafali ya katikati ya mwaka kwa masomo katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) imeongezeka kutoka Wahitimu 274 kwa mwaka 2023 hadi 777 kwa mwaka 2024 ambapo kati ya hao watunukiwa wanawake ni 284 sawa na asilimia 36.5 ya wahitimu wote.
Amebainisha hayo Makamu wa Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda wakati akitaja takwimu za Wahitimu katika Mahafali hayo yaliyofanyika Mei 23, 2024 katika viwanja vya Michezo vya Kampasi Kuu ya Edward Moringe ambayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Chuo hicho Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba ambapo amesema wahitimu hao wametokana na programu 72 za masomo zinazofundishwa chuoni hapo.
Prof. Chibunda amesema wanastahili kujipongeza kwa mafanikio ambayo wameendelea kuyapata kila mwaka ya kuongeza idadi ya nguvu kazi yenye Taaluma stahiki, ujuzi na weledi ambayo ni chachu ya kuongeza maendeleo katika nchi na mafanikio hayo yanatokana na ufanyaji kazi mzuri wa viongozi, wahadhiri na wafanyakazi wote wa Chuo hicho ambao wamewezesha kupiga hatua zaidi mwaka hadi mwaka.
Aidha, Prof. Chibunda amewaasa wahitimu kuendelea kuwa na bidii, uaminifu na moyo wa kujituma waliokuwa nao wakati wa masomo kwenye sehemu zao za kazi ili na huko waweze kufanikiwa vilevile kuwa mabalozi wazuri wa Chuo chao kwa kutumia maarifa na ujuzi walioupata chuoni hapo kutatua changamoto katika jamii kwa maendeleo yao binafsi na Taifa kwa ujumla.
“Mahafali ni tukio la kipekee sana popote pale duniani kwa wahitimu, tukio hili ni muda mahsusi wa kusheherekea, ni muda pekee wa kutathmini na kutafakari mafanikio ya miaka kadhaa katika kufikia malengo waliojiwekea, juhudi walizozionesha katika masomo yao, uaminifu na moyo wa kusoma na kufanya kazi waweze kuonesha katika mahala pao pa kazi”, amesema Prof. Chibunda.
Ameongeza kuwa Chuo kimeendelea kutekeleza malengo na majukumu yake kupitia katika Ndaki zake zote, Shule Kuu ya Elimu, Kurugenzi na Taasisi zake tangu Mahafali ya 42 Novemba 2023 ikiwemo utekelezaji wa shughuli za mafunzo ambazo zimeendelea kufanyika chuoni hapo kama ilivyopangwa katika Kampasi zote tatu kwa maana ya Edward Moringe, Solomon Mahlangu pamoja na Kampasi ya Katavi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Jaji Mstaafu Mohamed Chande Othman amesema wahitimu hao wanapohitimu masomo yao hawamalizi tu kama wahitimu bali viongozi watarajiwa, wavumbuzi na vijana walio tayari kuchangia katika maendeleo ya nchi hususani katika Sekta ya Kilimo na fani nyinginezo.
“Mzitumie elimu na mafunzo mliyopata kuwa wabunifu na kufanya uvumbuzi wa Maendeleo endelevu kwa ustawi wa jamii niwakumbushe tu dhamira ya Chuo chetu ni kukuza maarifa, uvumbuzi na kukuza maendeleo endelevu ya ustawi wa jamii hivyo mkawe mabalozi wazuri”, amesema Jaji Mohamed Chande.