PIRAMID YA AFYA: Maini, figo chanzo kikuu cha viinilishe mwilini

Upo uvumi wa miaka mingi duniani kuhusu ulaji maini na figo za ng’ombe, mbuzi na kuku kuwa una madhara kutokana na ogani hizo kufanya kazi ya kuondoa sumu mwilini.

Kiujumla minofu ya nyama ya wanyama wanaoliwa ni moja ya vyakula ambavyo huwa na virutubisho mbalimbali, ikiwamo protini nyingi, iliyo muhimu kwa afya zetu.

Katika nyama hiyo, moja ya sehemu ambazo zina virutubisho vingi zaidi kuliko unavyoweza kupata katika minofu ni ogani ya ini. Sehemu hii ina protini nyingi zaidi kuliko ile inayopatikana katika minofu.

Ini ni ogani kubwa kuliko nyingine ndani ya tumbo, lina kazi kubwa na muhimu katika mwili, ikiwamo kuvunjavunja na kuchakata sumu, kemikali na dawa zenye usumu.

Vitu hivyo bila kuchakatwa na ini vikiingia katika mfumo wa damu na kusambaa maeneo mbalimbali ya mwili moja kwa moja zinaweza kudhuru.

Hapa unapata picha kuwa ini inafanya kazi hiyo tu, halifanyi kazi ya kuzihifadhi sumu hizo. Kazi hiyo ambayo kitabibu hujulikana kama detoxication.

Ikiwa utakula kitu chenye sumu au hata dawa lazima itapita katika ini, itavunjwa vunjwa hatimaye kufifishwa au kuondolewa sumu, aidha kwa kubadilishwa kuwa katika hali isiyo na madhara.

Baadaye baada ya uchakataji huo huweza kufika katika figo, ambazo zenyewe huchuja damu na kuondoa takasumu na mabaki yasiyohitajika mwilini kwa njia ya mkojo.

Figo nayo ina kazi nyingi, lakini kazi kuu mbili huwa ni kuondoa takasumu mwilini na kuweka usawa wa maji na madini.

Mkojo unaotengenezwa na figo ni salama, ambao huhifadhiwa katika kibofu mpaka pale mwili utakapohisi haja. Mkojo umebeba sumu za urea na nyingine zinazokuwa sumu endapo tu zitabaki ndani ya mwili kwa kiwango kikubwa.

Na wenyewe siyo sumu unapokuwa nje ya mwili. Kwa hiyo ile imani potofu ambayo unaweza kuikuta mtaani au mitandaoni kuwa ulaji wa maini na figo si sahihi, hawana ufahamu wa kina juu ya kazi za ini na figo kisayansi.

Kama ini na figo zingekuwa zinahifadhi sumu, ina maana kuwa ulaji wake ungelikuwa si salama. Maana makali ya sumu hizo yangekuwa palepale na ingeliweza kumdhuru yule atakayekula ogani hizi.

Ini huwa na kazi nyingi mwilini, ikiwamo kuhifadhi viini lishe, uundwaji wa protini, kudhibiti sukari ya mwili, kudhibiti joto la mwili, kuzalisha nyongo ambayo inahusika kusaga vyakula vya mafuta.

Kutokana na kazi zake, ndiyo maana huwa limesheheni virutubisho vingi vyenye faida kubwa kiafya kwa mlaji, ikiwamo madini kama kopa, chuma, patasiamu na vitamini kama A, B na D.

Protini inayopatikana katika ini huwa ni nyingi, ikiwa katika ubora wa juu ukilinganisha na ile ya minofu.

Kwa upande wa madaktari wa mifugo, wanashauri kutokula mnyama mgonjwa au ambaye amekula kitu na kumfanya aumwe.

Ndiyo maana inashauriwa kula nyama ambayo imekaguliwa na mabwana afya, ambazo ndizo zinazouzwa katika masoko ya nyama au machinjio maalumu.

Ulaji wa figo na maini ni salama kwa sababu zinavunja vunja, kufifisha sumu na hatimaye kuziondoa mwilini. Ogani hizi hazihifadhi sumu yoyote mwilini. Ni salama kuliwa na ni chanzo kikubwa cha viinilishe.

Related Posts