Serengeti. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi amepiga marufuku tabia ya baadhi ya wasaidizi wake pamoja na watumishi katika ofisi yake kuwasikiliza wananchi wenye kero na changamoto kwa niaba yake badala yake ameagiza kila mwananchi mwenye kero anayefika ofisini kwake aruhusiwe ili aweze kumskiliza yeye mwenyewe kwanza.
Mtambi ametoa maagizo hayo leo Mei 24,2024 wilayani Serengeti alipokuwa akizungumza na watumishi wa halmashauri hiyo ambapo amesema mojawapo ya kipaumbele chake ni kutatua kero za wananchi.
“Wananchi ndio mabosi wetu, tumeajiriwa na wengine kuteuliwa kwaajili ya kusaidia kutatua kero zao sasa itakuwa ajabu mimi napokea mshahara huku wao wakikosa kusikilizwa eti kuna mtu anawasikiliza kwa niaba yangu,”amesema
Amesema kumekuwepo na utaratibu wa wananchi wanaofika katika ofisi yake kwaajili ya kero tofauti kulazimika kueleza kero zao kwa wasaidizi wake au watumishi wengine kabla ya kuruhusiwa kuonana naye huku wengine wakizuiliwa kwa maelezo kuwa kero zao hazina sifa za kusikilizwa na mkuu wa mkoa.
Amesema hali hiyo imepelekea baadhi ya wananchi kutokupata nafasi ya kuonana naye na badala yake kuelekezwa sehemu zingine jambo ambalo amedai sio sawa kwa maelezo kuwa mwananchi anapofunga safari na kwenda ofisini kwake kwaajili ya kumuona mkuu wa mkoa hakuna sababu ya kuwekewa pingamizi.
“Nataka hawa wananchi wakija nionane nao mimi mwenyewe kwanza nisikilize kero zao kisha nitaamua hiyo kero niagize idara gani ishughulikie huku nikifanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa maagjzo niliyotoa,” amesema
Amesema kwa muda mchache aliokaa mkoani Mara akiwa kama mkuu wa mkoa huo amebaini kuwa wananchi wengi wana changanoto ambazo zingine zinashindwa kutatuliwa kwasababu ya baadhi ya watumishi kutokuwajibika.
“Inatia huruma sana mtu anazungushwa zaidi ya miaka mitano bila msaada wowote, tena unakuta jambo lenyewe ni dogo tu lakini kwavile sio ndugu yako au mzaI wako unaamua kumuacha ahangaike bila msaada, hili halikubaliki lazima tuwe mstari wa mbele kutatua kero za wananchi wetu,” amesema Mtambi
Amesema suala la migogoro ya ardhi ni moja ya changamoto kubwa inayowakabili wakazi wa mkoa huo huku akisema kati ya watu watano wenye kero anao kutana nao wanne kati yao wana migogoro ya ardhi.
Amesema suala hilo lazima liwekewe mikakati maalum kwaajili ya kupambana nalo ambapo ameagiza halmashauri zote mkoani humo kuweka mipango ya matumizi bora ya ardhi na kusimamia utekelezaji wake.
Baadhi ya wakazi wa Mji wa Mugumu wilayani Serengeti wemepongeza hatua hiyo ya mkuu wa mkoa kupiga marufuku wananchi kuzuiliwa kuonana naye kwa maelezo kuwa hali hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kwenye utatuzi wa kero zao.
“Mimi nilikuwa na shida mwaka jana nikaenda ofisi ya mkuu wa mkoa lakini sikufanikiwa kumuona kwani katibu wake alinitaka nirudi huku nionane na mtendaji wa kata kwakweli nilisikitika sana,” amesema Mobare Warioba
Agnes Richard amesema tabia ya baadhi ya watumishi na wasaidizi wa viongozi kutaka kusikiliza kero za wananchi badala ya kuwaruhusu wananchi kuonana na viongozi moja kwa moja ni sababu nyingine inayoplekea kuwepo kwa kero nyingi za wananchi mtaani.
“Wengi sasa hivi wamekata tamaa ya kuwaona viongozi kwasababu wanajua wakifika maofisini watazuiliwa na wasaidizi hivyo wanaamua kukaa na kero zao tu,” amesema
“Yaani mtu unatumia nauli yako unapoteza muda kwenda kwenye ofisi ya kiongozi ukifika muhudumu anaanza kukuhoji halafu anasema hiyo sio shida ya kumpelekea mkuu, naomba viongozi wengine nao waweke utaratibu kama huu wa mkuu wa mkoa wetu,” ameongeza Abisai James