RC Mbeya atoa neno wafanyabiashara waliogoma Soko la Mwanjelwa

Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amewataka wafanyabiashara mkoani humo, kuachana na migomo kabla ya kufanya mazungumzo na viongozi wa mamlaka.

Amesema kufanya hivyo ni kutaka kuichafua  Serikali. Kauli hiyo ya Homera inakuja ikiwa ni siku moja  tangu wafanyabiashara wa maduka katika soko la Mwanjelwa kugoma kufungua maduka yao, wakidai kunyanyaswa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani humo, kukamatwa kwa biashara zao, kufungiwa maduka na utitiri wa kodi.

Mapema leo Ijumaa Mei 24, baadhi ya wafanyabiashara wameiambia Mwananchi Digital kuwa wanamtaka Mkuu wa Mkoa  kusikiliza na kutatua changamoto zao, vinginevyo wataendelea kugoma kutoa huduma.

Akizungumza katika ufunguzi wa maonesho ya biashara, Homera amesema wafanyabiashara wanapaswa kufanya mazungumzo na uongozi kupata suluhisho kabla ya kuanzisha mgomo.

Amesema hakuna vita yoyote iliyoshindwa kumalizika mezani, hivyo hata wafanyabiashara wanapaswa kuanza kukutana na viongozi na iwapo watashindwana ndio waingie mtaani kugoma.

“Niwaombe wafanyabiashara wasigome halafu ndio wapate suluhisho, bali wapate suluhisho ikishindikana ndio wagome na kuwasilisha ujumbe, vinginevyo ni kuichafua Serikali” amesema na kuongeza:

“Mei 10 Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji alikaa na viongozi kusikiliza kero za wafanyabiashara hapa Mbeya, hii ni katika kuthamini mchango wao, hivyo kuanza kugoma na kuanza kuomba kuonana na Mkuu wa Mkoa, Waziri au Rais huu siyo utaratibu kuleta taharuki,” amesema Homera.

Amesema mbali na Waziri kukutana na wafanyabiashara, Serikali mkoani humo pia ilishakaa na kumuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji kutoa miezi sita kuhusu ‘Service Levy’ kulipwa kidogo kidogo.

“Mkoa wetu umetulia watu wafanye biashara zao vizuri, lakini mazungumzo haya yamekuwa yanafanyika mara kwa mara kuhakikisha biashara inafanyika, ukitaka kuruka agana na nyonga,” amesema Homera.

Mkuu huyo wa Mkoa amewaamba pia vijana kuchangamkia fursa akieleza kuwa tafiti zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 61 mkoani Mbeya inamilikiwa na watu wazima na nyingine ni vijana.

“Sekta binafsi inaajiri watu wengi nchini, utafiti zinaonesha kuwa ni asilimia nane tu biashara zote zinamilikiwa na vijana huku zaidi ya asilimia 61 zikiwa kwa watu wazima, hivyo tujitahidi kubadilika kuchangamkia fursa” amesema kiongozi huyo.

Related Posts