Mwanza. Ili kukabiliana na changamoto ya ajira nchini, Serikali kupitia Wizara ya Uvuvi na Mifugo, imetenga Sh10.5 bilioni kwa ajili ya kuwezesha mitaji na miradi ya vijana.
Kauli hiyo imetolewa leo Mei 24, 2024 na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi kwenye hafla ya kufunga mafunzo kwa vitendo ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji kupitia programu ya jenga kesho iliyo bora (BBT) iliyofanyika jijini Mwanza.
Katambi amesema fedha hizo zinatarajiwa kuwainua vijana na kuchangia katika pato la Taifa kupitia sekta ya uvuvi na mifugo.
“Serikali kupitia Wizara ya Uvuvi na Mifugo imetenga Sh10.5 bilioni kwa ajili ya mitaji na miradi ya vijana. Huu ni mwendelezo wa Serikali wa kuwainua kiuchumi vijana na kukabiliana na changamoto ya ajira,” amesema Katambi.
Mbali na fedha hizo, amesema vijana wanapaswa kutengeneza vikundi na kuandika maandiko ya miradi ya kuomba mikopo ya asilimia 10 inayotarajiwa kuanza kutolewa tena katika halmashauri zote nchini kuanzia Juni 2024.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Riziki Shemdoe, amesema baada ya mikopo hiyo kuanza kutolewa kijana mmoja atakuwa na uwezo wa kukopeshwa kuanzia Sh1 milioni mpaka Sh50 milioni huku kwa upande wa wenye vikundi ikiongezeka.
“Lakini pia katika bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi 2024/2025 iliyopitishwa Mei 14, 2024 tumetenga fedha kwa ajili ya kukopesha boti 390 za uvuvi na vizimba 490 kwa ajili ya ufugaji wa samaki. Tunaeleza haya kwa sababu tunajua mmeunda vikundi vyenu kwa hiyo tutakapo tangaza nafasi za kuomba mikopo hii changamkieni fursa,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi akimwakilisha Mkuu wa Mkoa Mwanza, Said Mtanda, amesema mpaka sasa Halmashauri ya Jiji hilo imetenga Sh2.3 bilioni za asilimia 10 kwa ajili ya kuwawezesha vijana na makundi mengine wanufaika wa mikopo hiyo.
“Tayari Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ameelekeza kila halmashauri kutenga fedha za mikopo ya asilimia 10 kwa hiyo jiandaeni ili pindi ikifunguliwa muanze kuomba ili kunufaika nayo. Naamini changamoto ya ajira tutaitatua na kuishinda,” amesema Makilagi
Katika hafla hiyo jumla ya vijana 291 kati ya 300 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wamehitimu mafunzo ya muda mfupi yaliyoendeshwa kwa miezi mitatu tangu Februari 16 mwaka huu.
Akisoma risala ya wahitimu hao, Muhsin Mohamed kutoka Kagera, amesema kupitia mafunzo hayo wamejifunza namna ya kutunza fedha, uundaji na usajili wa vikundi, uandishi wa maandiko ya miradi na jinsi ya kuendesha miradi hiyo huku yakiambatana na mafunzo kwa vitendo.
“Kabla ya mafunzo haya akili za sisi vijana unao tuona hapa zilikuwa ni kuajiriwa ili kufanikiwa katika maisha yetu, lakini kupitia mafunzo haya tumebadili mtazamo wetu na tumegundua kuwa tunaweza kujiajiri na kuajiri vijana wengine kupitia sekta ya uvuvi,” amesema.
Mmoja ya washiriki wa mafunzo hayo, Nuriya Hamad ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kikundi cha Mwani Hadhina kutoka Mkoa wa Kaskazini Pemba, amesema uwekezaji wa ufugaji wa vizimba nchini utasaidia kupunguza uvuvi haramu wa mazao ya samaki.